Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza akizungumza na wanafunzi wa Shule mbalimbali katika Manispaa ya Iringa wakati wa maadhimisho ya siku ya hedhi duniani yaliyofanyika mkoani Iringa jana. Julia kwake ni mganga mkuu wa mkoa wa Iringa Dkt Robert Salim na kushoto kwake ni mkurugenzi wa shirika la Afya Plus Suzan Yumbe. (Picha na Friday Simbaya)
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza (mwenye hijab ya jano na miwani) akicheza muziki na wanafunzi wakati wa maadhimisho ya siku ya hedhi duniani waliofanyika mkoani Iringa jana. (Picha Friday Simbaya)
SERIKALI mkoa wa Iringa umelenga kuwawezesha wasichana kutimiza ndoto za maisha yao kwa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowafanya wabaki nyuma katika kuhudhuria masomo kipindi wakiwa katika hedhi.
Hayo yamezungumzwa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza wakati wa kuelekea maadhimisho ya Siku ya Hedhi Duniani ambapo kimkoa yalifanyika kwa mara ya kwanza jana katika Bustani za Manispaa na kuhudhuriwa na wanafunzi wa kike kutoka shule mbalimbali za sekondari za mjini hapa ambapo kila mwaka yanaadhimishwa Mei 28.
Alisema kuwa changamoto kubwa ambayo wanakabiliana nayo watoto wa kike wengi walioko mashuleni ni kipindi cha hedhi ambapo baadhi yao wamekuwa hawana elimu, kutojiamini na utoro mashuleni wanapokuwa kwenye vipindi vya hedhi hali inayosababisha utoro.
Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano inayo dhamira ya dhati kuhakikisha elimu bure inapatikana kwa jinsia zote hivyo basi suala la hedhi salama kwa wa kike ni jambo la msingi katika ngazi ya familia, jamii, na hata mashuleni kuwapatia elimu itakayowezesha kuwa na ufahamu wa masuala ya hedhi.
Masenza alisema kuwa ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kuwa mtoto wa kike anahudhuria masomo yake kwa mwaka mzima pasipo kuwa na vikwazo vinavyosababishwa ama na mazingira duni au ukosefu wa bajeti katika kupata taulo hizo maalum za hedhi.
Aliwataka wadau na wananchi kwa ujumla kuvunja ukimya juu ya suala la hedhi salama kwa mtoto wa kike na kuwezesha mtoto wa kike kupata taulo maalum kila mwezi na mkoa wa Iringa una mkakati maalum wa kumaliza changamoto hizo.
“Changamoto mbalimbali zinazowakabili wasichana wanapokuwa kwenye vipindi vya hedhi yanapaswa kujadiliwa na kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu kwa kuwa yanachangia kurudisha nyuma jitihada za kuwainua watoto wa kike nchini na kuwataka mabinti kuondoka na aibu ya katika suala la hedhi hivyo mkakati upo kumaliza kwa kuwapatia bure mataulo maalum watoto wa kike” alisema
Awali Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Afya Plus, Suzan Yumbe ambao ndio waratibu wa maadhimisho hayo mkoa, alisema kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuvunja ukimya juu ya masuala ya hedhi ikiwemo kuondokana na dhana potofu kwamba hedhi ni ugonjwa pamoja na namna bora ya kuhakikisha mtoto wa kike anajiweka katika hali ya usafi ili abaki shuleni badala ya kukosa masoko kila apatapo hedhi.
Alisema ukosefu wa mazingira bora kama vyoo, maji safi na salama pamoja na vyumba mahsusi vya kubadilishia nguo , hasa kwa watoto wa kike wanapokua katika hedhi mashuleni kuna changia utoro.
Alisema kuwa shirika hilo tangu limeanza kutoa elimu ya hedhi wamekwisha gawa zaidi pedi 600 kwa wanafunzi wa kike mbalimbali katika shule mbalimbali mjini hapa na kuwezesha kupunguza kwa kiasi kikubwa utoro mashuleni.
Yumbe alisema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanaambatana na kauli mbiu ya ‘Hakuna vikwazo zaidi wezesha wanawake na wasichana kupata hedhi salama’ hivyo shirika hilo lina mikakati ya kuwezesha watoto wa kike kupata taulo maalum za kufua na kuzitumia tena ambazo ni salama na zitamwezesha mtoto kike kuhudhuria masomo.
No comments:
Post a Comment