Saturday, 26 May 2018

MAWAKILI WA BILIONEA WA ESCROW WACHACHAMAA MAHAKAMANI,WALIA NA UPANDE WA SERIKALI



Didas Respicius, wakili wa utetezi katika kesi inayomkabili Harbinder Seth na mfanyabiashara James Rugemalira, wamekiamsha baaada ya kuwasilisha malalamiko Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa washtakiwa hao wamefikisha mwaka mmoja gerezani na upelelezi wa kesi inayowakabili bado haujakamilika.

Wakili huyo ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Mei 24, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Iman Mizizi kueleza upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Didas amedai kuwa washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani Juni 19, 2017 wakiwa na mashtaka ambayo yanadhaminika lakini wakiwa katika kuwasilisha maombi ya dhamana, walibadilishiwa mashtaka ambayo hayana dhamana.

Amesema tangu mwaka jana hadi sasa upande wa mashtaka unadai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, kwamba kuwa kwa mujibu wa hati ya mashtaka washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo, mwaka 2013. 

Amebainisha kuwa walifikishwa mahakamani miaka minne baadae lakini mpaka sasa bado inadaiwa upelelezi haujakamilika.

Ameomba upande wa mashtaka ufanye kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na Katiba kwa kujali haki za washtakiwa ili kesi iendelee mbele, kuutaka upande wa mashtaka ndani ya siku 14 ueleze upelelezi umekamilika, kama haujakamilika washtakiwa waachiwe huru.

Wakili Mizizi alidai suala la Seth kupatiwa matibabu bado linashughulikiwa na kwamba wanasubiri jopo la madaktari litakapokamilika atapatiwa matibabu.

Amesema Katiba ndiyo inayotumika kutunga sheria na ndiyo iliyotumika kuwafunguliwa mashtaka washtakiwa .

Baada ya kusikiliza hoja zote, Hakimu Shaidi amesema amezingatia hoja zote na akashauri upande wa utetezi kupeleka maombi Mahakama Kuu kwa ajili ya kupata maelekezo ya sheria ambazo zinalalamikiwa na zile zinazowafunga mikono.

Hakimu Shaidi aliiahirisha kesi hiyo hadi Juni 7, 2018 kwa ajili ya kutajwa.

Sethi na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola 22 milioni za Marekani.
Chanzo ni Mcl Online

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...