Na Friday Simbaya, Iringa
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Fortunatus Musilimu akiongozana na Mkuu wa usalama barabarani mkoa wa Iringa (RTO) Yusuf Kamotta, amefanya ukaguzi wa kushtukiza katika baadhi ya mabasi ya abiria na malori mkoani iringa kwa kukagua liseni za madereva.
Kamanda Musilimu alikuwa mkoani iringa ikiwa ni sehemu yake ya kufanya ukaguzi wa magari ya abiria pamoja na magari mengine usiku na mchana katika operesheni yake ya 'nyakua nyakua' ya kukamata madereva wanaofanya makosa.
Operesheni hiyo jana ilifanikiwa kumnyakua dereva mmoja wa mabasi ya New Force mkoani baada ya wananchi kutoa taarifa kuwa dereva huyo alikuwa akiendesha basi kwa mwendo kasi kwa kuwekwa lupango.
Hivi karibuni jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, limezindua operesheni 'Nyakua Nyakua' ambayo itahusisha kuwakamata madereva wanaofanya makosa, kuwaweka mahabusu kabla ya kufikishwa mahakamani.
Kwenye operesheni hiyo, askari wa usalama barabarani hawatawatoza faini madereva watakaokutwa na makosa ikiwamo kuzidisha mwendo na badala yake watawaweka mahabusu na kisha kuwafikisha mahakamani siku inayofuata.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, SACP Fortunatus Musilimu, aliliambia Nipashe jana kuwa, operesheni hiyo inafanyika kwa kuondoa mipaka ya kimikoa ambapo sasa askari wa kikosi hicho watakuwa wakishirikiana kukamata madereva wasiotii sheria.
Musilimu akiwa mkoani Iringa, aliagiza askari wake kuwakamata na kuwaweka mahabusu kisha kuwapeleka mahakamani madereva wote watakaobainika kwenda mwendo hatarishi.
“Wito wangu kwa madereva wa magari ni kuwa msiipuuzie kauli hiyo, bali muichukulie kwa uzito mkubwa katika kuhakikisha sheria za usalama wa barabarani zinafuatwa ili kuepusha ajali, nyingi zikisababishwa na uzembe wa madereva,” alisisitiza Kamanda Musilimu.
Pia waliwataka madereva wote waende kusoma ili muda utakapofika wa miezi mitano waliopewa na mamlaka madereva wote ambao hatafanya hivyo watafungiwa liseni zao.
Hata hivyo, kamanda musilimu amewataka askari kuachana na tabia ya kusubiri makondakta kuwapelekea ratiba ya mabasi kwenye vibanda vyao vya kupumzikia lakini askari wanatakiwa kuuingia ndani basi ya kukagua hati zote ndani ya basi huku abiria wanaona.
Alisema kuwa baada ya kukaa kikao na wamiliki wa mabasi TABOA na kueleza kwamba askari wamekuwa wakichelewesha mabasi walikubaliana kuwa makondakta wasipeleke hati kwenye vibanda vya askari isipokuwa askari aingie ndani ya basin a kukgaua hati zote mbele ya abiria.
Katika hatua nyingine, kamanda huyo alisema kuwa ili kupunguza malalamiko kuchelewesha ratiba ya mabasi kikosi cha usalama barabarani nchini kwa kushirikiana na TABOA wataainisha vituo maalum vya kufanyia ukaguzi wa mabasi pamoja na magari mengine ili kupunguza utitiri wa vituo vya ukaguzi barabarani.
Aliongeza kuwa kwa kufanya hivyo kutaongeza ufanisi wa kazi ya ukaguzi pamoja na kuwafanya madereva waendesha magari kuligana na muda uliopangiwa kufika katika maeneo mbalimbali na kufika salama.
Kwa upande wake, Mkuu wa usalama barabarani mkoa wa Iringa (RTO) Yusuf Kamotta kuwa kuna changamoto ya ajali kwa hivyo amewataka wananchi kufanya ulinzi shirikishi barabarani ili kupunguza ajali.
RTO Kamotta alisisitiza kuwa ulinzi shirikishi barabarani ni pamoja na kutoa taarifa mapema kabla ya ajali kutokea, na hiyo ndio njia pekee ya kupunguza changamoto za ajali na kuongeza kuwa Tanzania bila ajali inawezekana.
Hata hivyo, kamanda kikosi cha usalama barabarani nchini SACP Fortunatus Musilumu na mkuu wa usalama barabarani mkoa wa iringa (RTO) Yusufu kamotta waliwashukuru wananchi na madereva kwa kutoa ushirikiano katika kupambana na jail za barabarani.
Mwisho
No comments:
Post a Comment