Friday, 24 August 2018

Tanzania kuwa mwenyeji mkutano wa Makampuni ya Bima ya nchi za Mashariki na kusini mwa Afrika



Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa 41 wa umoja wa kikanda wa makampuni ya bima ya nchi za Mashariki na kusini mwa Afrika (OESAI) ukiwa na lengo la kuendeleza vipaumbele vya kukuza soko la bima.

Hayo yameelezwa jijini Dar es salaam na kamishna wa bima wa mamlaka ya usimamizi wa shughuli za bima nchini (TIRA) Dkt. Baghayo Saqware wakati akitoa taarifa ya mkutano huo amesema kuwa mkutano huo utaleta manufaa kwa taifa kutokana na kuwa na wageni zaidi ya 350 kutoka mataifa zaidi ya 30 yanayohudhuria mkutano huo.

“Makampuni ya bima, wafanyabiashara na watoa huduma changamkiani fursa hizo haswa wale waliopo Kwenye jiji la Arusha ili msaidie katika kukuza uchumi wa taifa letu.” Amesema Saqware.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mkutano huo Khamis Sulemani amesema kuwa uwepo wa mkutano huo hapa nchini utasaidia kutoa elimu na uzoefu kwa makampuni ya ndani kujua jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza Kwenye sekta hiyo.

Aidha ameongeza kuwa kuzorota kwa biashara ya mabenki hapa nchini kumechangia kwa kiasi kikubwa kuathiri sekta ya bima kutokana na uwekezaji wao mkubwa kutegemea benki hivyo kwa sasa watajitahidi kuwekeza kwenye vitu visivyohamishika.

Pia amesema kuwa lengo la mamlaka hiyo ni kuhakikisha kuwa ifikakapo mwaka 2020 asilimia 50 ya watanzania wawe na aina yeyote ya bima ambapo kwa sasa Tanzania iko nafasi ya pili kwa nchi za Afrika Mashariki kwa kutoa huduma za bima.

Mkutano huo unatarajiwa kufanyika Agosti 27_29 mwaka huu jijini Arusha ukiwa na kauli mbiu ya “Kuimarisha na kufanya mageuzi katika sekta ya bima kwa maendeleo endelevu” ikiwa imepita miaka 23 tangu mkutano huo ufanyike Tanzania mwaka 1995.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...