Thursday, 11 September 2025

 IRINGA WAANZA MAANDALIZI YA MPANGO MKAKATI WA KUTOKOMEZA UKATILI WA KIJINSIA



 

Iringa. Katika juhudi za kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia (GBV), Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali umeanza kuandaa rasimu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake, Watoto na Wanaume (MTAKUWA II) ngazi ya mkoa, kwa lengo la kuhakikisha ukatili unatokomezwa kwa kiwango cha juu kabisa.

 

Kikao kazi cha maandalizi ya mpango huo wa kitaifa wa miaka mitano (MTAKUWA II 2024/25 – 2028/29), kiliongozwa jana na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Saida Mgeni, ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Jamii mkoani humo.

 

Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa MTAKUWA/NPA-VAWC mkoa wa Iringa, Grace Simalenga, alisema mpango mkakati wa awamu ya pili umejumuisha pia wanaume na wavulana ili kuhakikisha mapambano dhidi ya ukatili yanagusa makundi yote.

 

“Leo tumekutana kupitia maandalizi ya mpango mkakati wa mkoa kwa ajili ya kupambana na ukatili dhidi ya wanawake, watoto, wanaume na wavulana. Tulihusisha waratibu wa halmashauri, viongozi wa dini, taasisi mbalimbali, pamoja na waandishi wa habari ili kuhakikisha mpango huu unatekelezeka kwa ufanisi,” alisema Simalenga.

Aliongeza kuwa kikao hicho kimewezeshwa na Shirika la SOS Children’s Villages kupitia ushirikiano wa serikali na sekta binafsi (PPP). Shirika hilo limekuwa mstari wa mbele katika kupinga mimba za utotoni na kuwawezesha wasichana waliojaliwa watoto wakiwa katika umri mdogo.

 

Meneja Miradi wa SOS Mkoa wa Iringa, Victor Mwaipungu, alisema shirika hilo limeamua kuunga mkono juhudi za serikali kwa kujenga uwezo wa kamati za MTAKUWA II kuanzia ngazi ya mkoa, halmashauri hadi kata.

 

“Kamati hizi zikijengewa uwezo na uelewa wa kutosha kuhusu maeneo ya kipaumbele ya MTAKUWA II, mapambano dhidi ya ukatili yatakuwa rahisi na yenye tija,” alisema Mwaipungu.

 

Kwa upande wake, Mchungaji Upendo Koko kutoka KKKT Dayosisi ya Iringa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Idara ya Wanawake na Jinsia kwa Jumuiya ya Makanisa ya Kikristo Tanzania mkoani Iringa, alisema rasimu hiyo ikikamilika itasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya ukatili katika jamii.

 

Naye Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto mkoani Iringa, Elizabeth Swai, alisema jukumu kubwa la wajumbe wa kamati hiyo ni kutoa elimu na kuhakikisha makosa yote yanayohusiana na ukatili wa kijinsia yanashughulikiwa ipasavyo.

 

Aidha, Afisa Ustawi wa Jamii na Mratibu Mwenza wa MTAKUWA II mkoa wa Iringa, Martin Chuwa, alisema mpango mkakati wa awamu ya pili umeboreshwa kwa kuongeza maeneo mapya, ikiwemo ukatili wa kimtandao na kuhusisha zaidi wanaume na wavulana.

“Takwimu zinaonesha kuwa ukatili dhidi ya wanaume nao unaongezeka mwaka hadi mwaka. Pia mpango huu umeongeza ushirikiano wa taasisi binafsi katika nafasi za uratibu,” alisema Chuwa.

 

MTAKUWA wa awamu ya kwanza ulikamilika, na sasa awamu ya pili (MTAKUWA II) inaanza kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano, 2024/25 – 2028/29, kwa lengo la kuhakikisha Tanzania inakuwa taifa lisilo na ukatili wa kijinsia.

Mwisho










No comments:

MKUU WA MAJESHI YA ULINZI NCHINI AWASILI MKOANI IRINGA

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jenerali Jacob John Mkunda, amewasili mkoani Iringa leo kwa ziara ya kikazi.  ...