ALIYEKUWA Katibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Frederick Mwakalebela na mkewe Selina Mwakalebela wamefikishwa mahakamani na Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) Mkoa wa Iringa huku wakisindikizwa na umati mkubwa wa makada wa Chama cha cha Mapinduzi (CCM) na wananchi wa Manispaa ya Iringa.
Umati ulifurika mahakamani hadi kupelekea wasikilizaji wengine kusikilizia kesi inayowakabili huku wakiwa nje ya mahakama ya hakimu mkazi wa mkoa wa Iringa.
Umati huo unakuja siku chache baada ya Halmashauri kuu ya CCM (NEC) kumuengua Mwakalebela aliyeshinda kwa kupata kura 3,897 dhidi ya Mbunge aliyepita Monica Mbega aliyepata kura 2989 ambaye ameteuliwa na NEC.
Akisoma mashtaka hayo mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya Mkoa wa Iringa, Gladys Barthy, waendesha mashtaka wa Takukuru,Prisca Mpeka na Imani Mizizi walisema mshitakiwa namba moja na mbili kwa pamoja walitoa hongo ya sh. 100,000 kwa Gwido Sanga ili awagawie wajumbe ambao waliitwa kwenye kikao.
Mpeka alisema Julai 20 katika kijiji cha Mgongo Mwakalebela anadaiwa kuitisha kikao nyumbani kwa Sanga ambacho kilihudhuriwa na wajumbe wa CCM 22 ambapo baada ya hotuba Selina Mwakalebela alitoa Sh100,000 kwa Sanga ili awagawie wajumbe waliohudhuria.
Mpeka alisema washtakiwa hao kwa pamoja, walitoa rushwa kinyume cha sheria ya kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007 kifungu cha 15(1)(b) kinachokwenda sambamba na sheria ya gharama za uchaguzi namba 6 ya mwaka mwaka 2010 kifungu namba 21 (1) (a) na kifungu cha 24(8).
Washitakiwa wote walikana shitaka na kuachiwa kwa dhamana baada ya wadhamini kutimiza masharti yaliyowekwa na Mahakama.
Baada ya mabishano ya muda mrefu kati ya upande wa Mshaki ukiongozwa na Mizizi na wakili wa Mshakiwa, Basil Mkwata mahakama iliridhia sifa za wadhamini baada ya wadhamini wawili taarifa zao kutofautiana.
Alisema baada ya wadhamini kukamilisha masharti mahakama ilitoa dhamana ambayo masharti yake yalikuwa walitakiwa kuwa na Sh500,000, mali isiyohamishika na mmoja wapo kuwa mtumishi wa serikali au taasisi inayotambulika.
Katika kesi nyingine iliyotajwa kwa mara ya pili, Mwakalebela anadaiwa kutoa hongo ya Sh100,000 kwa Mwenyekiti wa CCM kijiji cha Mkoga, Hamis Luhanga ili awagawie wajumbe 30 waliohudhuria kikao alichoitisha.
Akisoma shitaka hayo mbele ya hakimu, mahakama ya Mkoa wa Iringa, Festo Lwelu, waendesha mashtaka wa Takukuru, Prisca Mpeka na Imani Mizizi walisema Juni 20 mshitakiwa Mwakalebela anadaiwa kutoa hongo ya sh. 100,000 kwa Hamis Luhanga ambaye ni mwenyekiti wa kijiji cha Mkoga ili awagawie wajumbe wa CCM 30 ambao waliitwa kwenye kikao.
Mshitakiwa alikana shitaka na aliachiwa kwa dhamana baada ya wadhamini wake wawili kutimiza masharti yote yakiwemo ya kuwa na Sh5m, kutoa ahadi ya sh5m na mmoja kuwa mtumishi wa Serikali au taasisi inayotambulika.
Mpeka alisema mshitakiwa anadaiwa kutoa rushwa kinyume cha sheria ya kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007 kifungu cha 15(1)(b) kinachokwenda sambamba na sheria ya gharama za uchaguzi namba 6 ya mwaka mwaka 2010 kifungu namba 21 (1) (a) na kifungu cha 24(8).
Frederick Mwakalebela akiwa mahakani leo.Wakazi wa Manispaa ya Iringa wakiwa wamefurika nje ya Mahakama baada ya kutoka kusikiliza kasi ya Mwakalebela leo
Kesi zote mbili zimeahirishwa mpaka Septemba 15 zitakaposikilizwa tena. Mwakalebela anatetewa na wakili Mkwata kutoka Mkwata Law Chamber.
No comments:
Post a Comment