Sunday, 1 August 2010

MWAKALEBELA.................1

Bw. Fredrick Mwakalebela (Kulia) akiwa na Mkewe Bi. Selina Mwakalebela wakati wa mkutano na waandishi wa habari mijini Iringa jana.




FREDERICK Mwakalebela mmoja wa wanaCCM anayetafuta ridhaa ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwania ubunge jimbo la Iringa Mjini amekanusha vikali madai ya rushwa yaliyotolewa dhidi yake na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).



Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mwakalebela alisema hajawahi kukamatwa kwa madai hayo, lakini akakiri kuhojiwa na Takukuru ili atoe ufafanuzi kuhusu taarifa zilizotolewa dhidi yake kwa taasisi hiyo.



Akinukuu taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Iringa, Donasian Kessy kwamba Julai 20 katika kijiji cha Mgongo aliitisha kikao nyumbani kwa Gwido Sanga ambacho kilihudhuriwa na wana CCM 22, Mwakalebela alisema alikutana na wana CCM hao na kutangaza nia yake ya kuwania ubunge katika jimbo hilo, na kwamba katika kikao hicho hakutoa rushwa ya aina yoyote kama ilivyodaiwa.



"Nilikutana kweli na wanachama hao nikawaleza historia yangu, na nikatangaza nia ya kuwania ubunge katika jimbo hili la Iringa Mjini na baadaye nikawaleleza malengo yangu endapo azma yangu hiyo itafanikiwa,baada ya hapo nikaondoka" alisema.



Hata hivyo alisema katika mkutano huo, mkewe Selina Mwakalebela anatuhumiwa na Takukuru kwa kutoa sh 100,000 kwa wanachama hao.



"Sifahamu chochote kuhusiana na madai ya mke wangu kutoa kiasi hicho cha fedha kwa wanachama hao, na malengo ya kufanya hivyo," alisema.



Alisema anashangaa kwanini Takukuru wamemuhusisha katika madai hayo ya mkewe kutoa kiasi hicho cha fedha, hususani katika kipindi hiki ambacho wanaCCM wanaenda kufanya maamuzi magumu ya kumpata mgombea wao.



"Mke wangu ni mke wangu, lakini kama kuna ushahidi wa yeye kufanya kosa, hilo lisichukuliwe kosa la familia," alisema.



Katika taarifa yake aliyoitoa juzi kwa waandishi wa habari Kessy alisema pamoja na Mwakalebela, aliyekuwa waziri katika serikali za awamu karibu zote Joseph Mungai anayewania ubunge Mufindi Kaskazini na Mkuu wa Wilaya ya Hai, Dk Norman Sigalla anayetafuta ridhaa hiyo jimbo la Makete na Fadhili Ngajilo jimbo la Iringa Mjini,walihojiwa kwa madai ya kuhusishwa na vitendo vya rushwa katika majimbo wanayogombea.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...