PINGAMIZI la awali la kutaka kuondolewa mahakamani kesi ya kutoa hongo katika mchakato wa kura za maoni, inayomkabili aliyewahi kuwa Waziri katika serikali za awamu zote nne, Joseph Mungai (66), imeshindwa kuanza kusikilizwa baada ya upande wa mashitaka (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa), kuomba pingamizi hilo liwasilishwe mahakamani kwa njia ya maandishi.
Mungai pamoja na makada wengine wawili wa CCM, akiwemo Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Mufindi, Fidel Cholela (39) na Moses Masasi wanakabiliwa na mashtaka 15 ya kutoa rushwa kinyume na sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa ya mwaka 2007 na sheria ya gharama za uchaguzi ya mwaka 2010.
Mawakili wanaomtetea Mungai,aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini (CCM), Alex Mgongolwa na Basil Mkwata, LEO walifika katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Iringa, kuwasilisha pingamizi hilo kwa lengo la kuanza kusikilizwa.
Wakiwa mbele ya hakimu anayesikiliza kesi hiyo namba 5 ya mwaka 2010, Mary Senapee, mawakili hao waliiomba mahakama hiyo kuruhusu pingamizi hilo kuwasilishwa na kuanza kusikilizwa kama ilivyopangwa, kwakuwa kesi hiyo ina mvuto kwa jamii.
“ Mheshimiwa, kesi hii kama unavyoiona ina public interest, hivyo kama itaendeshwa kwa njia ya maandishi, umma hautaweza kufahamu maendeleo ya shauri lenyewe linavyokwenda”alisema mmoja wa mawakili wa Mungai, Basil Mkwata huku,
Wakili Alex Mgongolwa, akiieleza mahakama hiyo kuwa pingamizi zinazowasilishwa mahakamani hapo zinatokana na maandalizi ya kesi hiyo ya Takuku na kwamba hakuna kitu kipya, hivyo ni vyema upande wa mashitaka , wakajipa nafasi ya kusikiliza pingamizi hizo ni zipi badala ya kutaka kuchelewesha kusikilizwa kwa shauri hilo kwa kuomba upande wa utetezi tuwasilishe pingamizi kwa njia ya maandishi.
Awali, mwendesha mashitaka wa Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Iringa (Takukuru), Bw. Imani Nitume aliiomba mahakama hiyo, kuamuru upande wa utetezi uwasilishe pingamizi hilo mahakamani hapo kwa njia ya maandishi na si kama ilivyokusudia kuliwasilisha kwa njia ya kawaida (Oral) na kutaka ianze kusikilizwa.
“Mheshimiwa,tunakuomba kama ikikupendeza tupate pingamizi hili kwa njia ya maandishi, sipingani na hoja iliyotolewa na upande wa utetezi kwamba shauri hili lina public interest lakini bado upande wa mashitaka tunasisitiza wawasilishe pingamizi kwa njia ya maandishi… kwakuwa kesi hii inahitaji umakini mkubwa katika kusikiliza na kuiendesha ”, alisema mwendesha mashitaka huyo wa Takukuru.
Baada ya mabishano ya muda mrefu ya kisheria, hakimu Mary Senapee alisema anakubaliana na hoja za pande zote mbili lakini hoja hizo haziwezi kuzuia mahakama hiyo kuendelea na hivyo akakubaliana na ombi la upande wa mashitaka katika shauri hilo kwamba pingamizi hilo liwasilishe kwa njia ya maandishi.
Mfululizo wa mabishano ya hoja hizo za kisheria, uliishia kwa upande wa utetezi kukubaliana na mahakama hiyo kuwasilisha pingamizi lao Oktoba 22 mwaka huu, huku upande wa mashitaka nao ukiiomba mahakama hiyo ya hakimu mkazi Mkoa wa Iringa, nao wajibu pingamizi hilo Novemba 05 mwaka huu.
Baada ya ombi hilo Hakimu Senapee alisema shauri hilo litafikishwa tena mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa Novemba 12 mwaka huu kwa ajili ya kupanga tarehe ya kuanza kusikilizwa kwa pingamizi hilo.
Inadaiwa kuwa Julai 08, mwaka huu, katika kata ya Ihalimba, Wilaya ya Mufindi, Mungai akiwa mmoja wa makada wa CCM waliokuwa wanawania kupitishwa katika kura za maoni kugombea ubunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini, kwa pamoja na watuhumiwa wenzake, walitoa hongo ya Sh.10,000 kwa Mwenyekiti wa CCM tawi la Vikula kama kishawishi cha kumpigia kura wakati wa zoezi la upigaji wa kura za maoni.
Katika shitaka la pili, inadaiwa kuwa watuhumiwa wote kwa pamoja, siku na katika eneo hilo walitoa hongo ya Sh.10,000/- kwa Konjesta Kiyeyeu ambaye alihudhuria kikao cha kamati ya CCM Kijiji cha Vikula.
Katika shtaka la tatu, nne, tano na sita, watuhumiwa wanadaiwa kutoa hongo ya Sh.10,000/- kwa Aldo Lugusi, Ezekiel Mhewa, Tulaigwa Kisinda na Jiston Mhagama kwa lengo hilo hilo la kuwashawishi wampigie kura za maoni.
Katika shitaka la saba,watuhumiwa hao wanadaiwa kutoa hongo ya Sh.20,000/- kwa Maria Kihongosi na shtaka la nane kutoa hongo ya Sh.5,000/- kwa Lurent Mdalingwa wakati shtaka la tisa wanadaiwa kutoa hongo ya Sh.20,000/- kwa Victory Kalinga ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Kijiji cha Ugessa.
Katika mashtaka namba kumi hadi 12 washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa walitoa hongo ya Sh.2,000/- kwa Francis Chonya, Alfred Kisinga na Issac Tewele wakati shtaka la 13 wanadaiwa walitoa hongo ya Sh.10,000/- kwa Sosten Kigahe.
Mashitaka mengine, namba 14 watuhumiwa wanadaiwa kutoa hongo ya Sh.10,000/- kwa Raphael Lutumo na shitaka la mwisho walitoa hongo ya Sh.20,000/- kwa Andrew Mkiwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...
Na Friday Simbaya, Mufindi Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...
-
KIKUNDI cha Upendo ni kikundi cha kina mama 20 walioamua kujiunga kwa pamoja na kuanz...
-
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini MIEMBE hulimwa karibu katika nchi zote zilizoko kwenye ukanda wa joto, na hasa tropiki. Nchini ...
-
The most deadly form of tuberculosis is one that lies in wait inside the body for years, attacking at the first sign of weakness. Abou...
No comments:
Post a Comment