Monday, 15 November 2010

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais Jakaya Mrisho Kikwete afanye maamuzi magumu na mazito katika uteuzi wa waziri mkuu wa serikali ya Tanzania kwa kipindi chake cha mwisho cha urais kwa mujibu wa katiba ya CCM.


Kama ilivyofanyika maamuzi magumu ya kumuondoa spika wa bunge lililopita Mh. Samuel Sitta na hatimaye Mh. Anna Makinda kuwa spika wa kwanza mwanamke katika historia ya Tanzania. Huu ulikuwa uamuzi mgumu na mzito kwa chama cha mapinduzi na mwenyekiti wake ambae pia ndiye rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania.


Kabla sijazungumzia ni kwanini mh. Kikwete afanye maamuzi mazito na magumu, nichukue nafasi hii kuwapongeza kipekee baadhi ya watanzania kwa nafasi zao:


1. kipekee nimpongeze mh. Anna Makinda kwa kuchaguliwa kwake kuwa spika wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kipindi cha 2010 – 2015. hongera sana. Nina uhakika hatawaangusha wanawake wa Tanzania kama sio Afrika nzima. Mh. Makinda amechaguliwa kuwa spika katika kipindi kigumu sana kwa mstakabali wa uhai wa taifa letu, kuna mawazo ambayo huamini kuwa mh. Makinda amepata uspika baada ya njia za kijasusi za kumdondosha spika aliyemtangulia. Na njama hizo za kijasusi zimefanyika na kupangwa na moja ya makundi yaliyosigana sana katika medani za siasa na ufisadi katika bunge lililopita. Kama mawazo haya yana ukweli japo kidogo, basi mh. Makinda ana kazi ngumu ya kujiondoa na kujinasua kwenye kundi hilo linalodhaniwa kupanga mipango hiyo ya kijasusi, kwani bila hivyo, watanzania na dunia yote inaweza kumtamfisiri mh. Makinda kuwa miongoni mwa kundi hilo kitu ambacho kinaweza kuhatarisha uhai wa bunge na mstakabali mzima wa taifa la Tanzania.






2. kipekee nimpongenze mh. Slaa aliyekuwa mgombea wa kiti cha uraisi kwa tiketi ya chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) pamoja na chama chake kwa kuyakubali matokeo ya tume ya uchaguzi kama yalivyotangazwa na kuruhusu wabunge wake kuingia bungeni. Sina uhakika sana kama mh. Slaa kwa kukaa kimya kwake ni tafsiri ya “kubali yaishe ama anatunga sheria” katika hili siri yake anayo mwenyewe mh. Slaa na chama chake, lakini yatosha kumpongeza hata kwa hatua hii ya kufanya wabunge waapishwe kukiwa na usalama na utulivu. Hongera sana Dr. slaa na chama chako.






1






3. Mwisho kipekee nimpongeze mh. Samuel Sitta kwa kukubali yaliyomkuta, katika hili nisingependa kuongea mengi kwani siri ya mtungi aijuae kata, siri ya kuenguliwa kwake kwenye nafasi ya kugombea uspika kwa awamu ya pili kamati kuu ya CCM na mheshimiwa Sitta wanaijua wenyewe, iwe ni ujasusi ama demokrasia ndani ya chama cha mapinduzi ni siri yao wenyewe. Hata hivyo yatosha kumpa hongera mheshimiwa Sitta kwa hatua aliochukua ya kubali yaishe, kama wahenga wasemavyo wajenzi tusigombanie fito wakati nyumba tuijengayo ni moja na ni yetu sote.






Maamuzi mazito na magumu yanayostahili kuchukuliwa na mheshimiwa Kikwete pengine na bunge zima la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


1. kama imewezekana kwa maamuzi ya magumu na mazito yaliyofanywa na kamati kuu ya CCM kumpata spika mwanamke tena nje ya taratibu na kanuni za chama za kuongoza vipindi viwili kama ilivyo kwa mgombea urais, yawezakana kabisa pia waziri mkuu akateuliwa toka kambi ya upinzani. Nashauri hivi kwa sababu, siri ya matokeo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi wanaoijua ni tume ya uchaguzi yenyewe, usalama wa taifa, pamoja na mh. Kikwete na Slaa na vyama vyao. Ninauhakika matokeo yaliyotangazwa CHADEMA na CCM wanajua undani wake kwani kila chama kina matokeo ya wagombea urais katika kila jimbo. Ni kwa msingi huu naomba hekima na busara zitumike kufikia maamuzi hayo magumu na mazito ya uteuzi wa waziri mkuu toka kambi ya upinzani, linalowezekana leo lisingoje kesho, tusingoje hadi damu imwagike kuleta mabadiliko hati miliki ya Tanzania ni ya watanzania wote.






2. Pili, kama Zanzibar imewezekana kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa Tanzania bara tunasubiri nini? Je tunasubiri watu waende shimoni? Tunasubiri damu imwagike? Tusisubiri kufika huko, serikali ya umoja wa kitaifa haina budi lazima iwe, hati miliki ya Tanzania ni kwa watanzania wote tena mikoa yote, katika historia ya Tanzania inaonekana uongozi wa juu wa serikali umemilkishwa kwa baadhi ya mikoa kama sio kikanda, hata mikoa iliyosahauliwa ni sehemu ya Tanzania na ni wamiliki wa Tanzania tusisubiri maafa yatokee. Tunashukuru Mungu marais wametoka kaskazini, mashariki, visiwani, na kusini ninaamini safari nyingine nyanda za juu kusini watakumbukwa kwenye nafasi hiyo nyeti. Lakini pia tumekuwa na mawaziri wakuu toka kaskazini, kanda ya kati, mashariki, na kusini na kiraka toka nyanda za juu, bado inaonekana nyanda za juu ni






2






wasindikizaji tu katika uongozi taifa hili la Tanzania. Tunahitaji serikali ya umoja wa kitaifa na kwamba Tanzania ni yetu sote, lazima tubadilike na wakati ni huu, mheshimiwa Kikwete afanye maamuzi magumu na mazito ili aje akumbukwe na mikoa iliyosahaulika.






3. Mwisho ni kwa bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania, kama kwa matokeo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi asilimia 39 ya wapiga kura imekubali mabadiliko ndani ya nchi, na narudia tena matokeo yaliyotangazwa ni ya kikatiba zaidi kuliko maamuzi ya wananchi, niwaombe waheshimiwa wabunge waache ushabiki wa vyama kwani wao ni wawakilishi wa watanzania, wafike mahali naibu spika atoke upinzani ili ile asilimia 39 ya watanzania iwakilishwe vyema kwenye maamuzi ya bunge na hapo tutakuwa tunajenga umoja wa kitaifa. Pia tuzingatie kuwa matokeo yaliyotangazwa na idadi ya wapiga kura waliopiga kura ni asimia 27 tu ya watanzania wenye sifa na stahiki ya kikatiba ya kupiga kura, maana yake hata viongozi waliotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi wametangazwa kimakosa, kwani wamechaguliwa na watanzania wenye haki ya kupiga kura chini ya nusu, kuna haja ya kulitazama zaidi suala hili, tupate bunge lenye sura ya umoja wa kitaifa na uwakilishi sawa kwa watanzania wote.






Imetolewa na: Kimbombo Andrew Uswege TAREHE 14/11/2010


Chuo Kikuu Mkwawa – Iringa


Simu: 0754/0715/0786 - 261870

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...