Thursday, 25 November 2010

WAKONSOLATA NA HARAKATI ZA KULETA MAENDELEO HAPA NCHINI

UJIO WA WAMISIONARI WA SHIRIKA LA WAKONSOLATA NA HARAKATI ZA KULETA MAENDELEO HAPA NCHINI;

Ujio wa wamisionari wa shirika la Wakonsolata hapa nchini mwishoni mwa karne ya 18, umetoa changamoto kubwa katika nyanja za maendeleo pamoja na kuleta chachu muhimu kwa jamii ya wananchi wa hapa nchini kutokana na wamisionari hao kujikita zaidi katika shughuli za kijamii na kuifanya jamii ya wananchi katika maeno ambayo walifika ambapo mkoa wa Iringa ni mmoja ya sehemu ambazo mabadiliko ya kimaendeleo hayo yamesababishwa na ujio huo.

Wamisionari hao wa shirika la wakonsolata waliofika hapa nchini hususani mkoani Iringa, walikuwa ni mapadre, mabruda, masista na walei ambao kwa mara ya kwanza walifika kijiji cha Tosamaganga ambapo walifanya masikani yao na pia wote kwa pamoja walikuwa na lengo la kumkomboa binadamu wa kiafrika wa Tanzania na pamoja na shughuli zingine zote walizofanya za kijamii kiuchumi, kielimu, afya, mawasiliano walizingatia roho yao ya sala na kazi.

Ingawaje shughuli zao zote walizozifanya ni za kijamii tunaweza kuzigawanya katika makundi makubwa mawili ambayo ni shughuli za kimwili na kiroho, kutokana na kuwa wamisionari hao walijali zaidi kumhubiria mwanadamu ambaye anaelimu, afya na kujua vizuri kile atakachokiamini kwa na hivyo shughuli zao kuleta changamoto kubwa ya kimaendeleo kiroho, kiuchumi, kiutamaduni na mtazamo mpya kwa jamii ambayo ilikuwa inaaza kuchanganyikana na wageni.

Katika shughuli walizofanya, Wakonsolata katika jimbo katoliki la Iringa, walizingatia kutoa elimu, afya, mawasiliano, kilimo, utunzaji wa mazingira, ujenzi wa nyumba za kisasa, maadili mema katika jamii pamoja na maisha safi ya kiroho, ambapo wamisionari hao walijishughulisha bila kuwabagua wananchi kwa mila, desturi, makabila wala hali zao ambazo waliwakuta nazo, walijali zaidi nia na malengo yao ya kuiendeleza jamii.

Maeneo ambayo kwa mara ya kwanza ya yalianza kujengwa shule za msingi ni pamoja na Tosamaganga, Madibila, Nyabula, Wasa na Ifunda ambapo katika shule za sekondari za mwanzo ni ya Tosamaganga na Malangali ambapo pia walihakikisha kuwa watu wanafundishwa mitaala mbalimbali ya elimu ikiwa ni pamoja na elimu dunia, uuguzi, elimu ya ufundi wa umeme, makaniksi, bomba, ufundi vyuma, seremala pamoja na ufundi wa kufyatua matofari na kuweza kujenga nyumba za kisasa na vigae vya kuezekea nyumba hizo ambapo swala la sala na kazi lilipewa kipaumbele zaidi.

Shule za mara ya kwanza ambazo zilianzishwa na Wamisionari wa Shirika la Wakonsolata zilileta chachu kubwa kwa jamii kimtazamo, kimaendeleo, kiuelewa na kiimani ambapo matokeo ya ujio wa wamisionari hao, hautaweza kusahaulika kamwe katika historia nzima ya kanisa katoliki, kujikomboa kwa Tanzania kutoka mikononi mwa wakoloni pamoja na kupata chachu mpya kabisa ya kimaendeleo ambayo iliwafanya wazinduke kutoka katika mila, desturi na utamaduni ambao walikuwa wamezamia.

Wamisionari Wakonsolata katika sekta ya afya, walijenga hospitali, zahanati na kufungua kiliniki ndogondogo katika maeneo ya vijijini ambako walikuwa wanatembelea kila mwezi na kuiwezesha jamii ya wenyenji wa Mkoa wa Iringa ambao ni Wahehe kubadilika kutoka matumizi ya madawa ya jadi na kuingia katika ulimwengu mpya wa matibabu ya kusomea.

Katika kila eneo walipojenga shule kutokana na kuwafundisha wananchi, waliwezesha watu kuwasiliana kutoka ukoo mmoja hadi mwingine, Kabila la wahehe na makabila mkoani Iringa na makabila mengine ambako wamisionari wengine kutoka bara la ulaya walifika pamoja na kuifanya Tanzania kuingia katika ramani ya dunia kwa kuwa na mawasiliano na nchi nyingine za ulaya zikiwemo Italia, Ujerumani, Hispania pamoja na kuijua vema nchi ya Israeli ambako ndiko chimbuko la historia ya ukristo duniani.

Aidha waliwezesha kuwepo kwa mawasiliano ya barabara, kukua kwa lugha kama Kiswahili ambacho kilisaidia kuleta uhuru kwa kuwa walitumia lugha hiyo kufundishia, kuhubiria Injili Takatifu ambapo lugha zingine zilizotumika ni kilatini, kiingereza, kiitaliano na kuiwezesha jamii ya watu kuwasiliana na ulimwengu mwingine na kupata mafanikio ambayo yapo hadi leo hii.

Wamisionari wa shirika la Wakonsolata, hawakuwa nyuma katika kuifundisha jamii sekta ya kilimo kwa kulima mashamba ya mahindi, ngano, maharagwe, alizeti, miti ya mbao ambapo katika bustani watu walifundishwa barabara kilimo bora cha matunda, mbogamboga zikiwemo nyanya, kabeje, vitunguu, miwa na viazi mviringo ambapo kwa kufanya hivyo waliikomboa jamii kwa kupata chakula bora na kuwa na lishe mbadala.

Kati ya mambo makubwa na ya maana ambayo katika historia ya maendeleo ya kanisa na watu wake hayatasahaulika ni kuwa Wamisionari, Wakonsolata walianzisha mashirika ya kitawa ya wanawake na wanaume. Mashirika hayo ni Shirika la Masista wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu wanaoitwa ‘Watheresina’ ambalo lilianzishwa mwaka 1935 na Mwasisi wake ni Monsinyole Padre Fransico Cagrielo ambaye kwa wakati huo alikuwa ndiye msimamizi wa Jimbo Katoliki la Iringa.

Nia na lengo kuu la mwasisi wa shirika hilo, Monsinyole Fransico Cagrielo kwa kuanzisha shirika la Watheresina ilikuwa ni kuendeleza mapambano dhidi ya Imani Takatifu ya Yesu Kristo, ujinga, maradhi na umasikini ambavyo watu wanakabiliana navyo kwa namna tofauti kwa vipindi tofauti kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ambapo dunia kama watu wake wasingepata elimu wangeyumba.

Viongozi wa Kanisa Katoliki Wanasemaje kuhusu Watheresina wa leo:
Mhashamu Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Askofu Mkuu Norbet Mtega alifafanua kinagaubaga kwa nini, wamisionari walifika Tanzania, kwanini walianzisha Shirika la Watheresina pamoja na kufundisha Imani ya Biblia Takatifu, elimu katika mitaala mbalimbali, hoja za Mhashamu Askofu Mkuu, Norbet Mtega ziligusa moja kwa moja mioyo ya waumini waliofika katika sherehe ya Jubilei ya miaka 75 toka kuanzishwa kwa shirika hilo na mahusiano yake katika historia nzima ya kanisa katoliki hapa duniani.

Mhashamu, Askofu Mkuu, Mtega anasema, “Shirika la Masista Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu yaani Watheresina, ni sehemu ndogo sana katika historia ya kanisa toka lilipoanzishwa hapa duniani, lakini shirika la Watheresina ni sehemu muhimu sana na ambayo haitasahaulika kamwe katika historia ya ujio wa Wakonsolata na historia nzima ya kanisa la Kristo hapa Iringa, Afrika na duniani kote kwa kuwa chachu yake sasa imeenea ulimwenguni kote.

“Mwasisi wa shirika la Watheresina, Baba Monsinyole Fransico Cagrielo amepanda mbegu kwa kuanzisha shirika hili ambalo kwa mara ya kwanza walijiunga masista 14, saba wakitokea parokia ya Madibila na saba wengine walitoka parokia ya hapa Tosamaganga, na leo hii tunao mashuhuda wawili waliobakia hai ambao ni Sr Getrude Kagali na Sr Agness Mhavile”, alisema huku akiwasimamisha watawa hao na umati kushangilia.

Askofu Mkuu, Mtega anaendelea, “Wamisionari Wakonsolata waliingia katika nchi iliyoitwa Tanganyika kwa wakati huo, kwa kabila la wahehe, mkoani Iringa katika kilima cha Tosamaganga mwishoni mwa karne ya 18 kati ya mwaka 1896 na kuanza mara moja shughuli zao za kuelimisha yamii kiimani, elimu ya kujikomboa kifikira ambapo pamoja na kufundisha kazi walisisitiza zaidi sala na kazi ndiyo roho ya kukuza maadili matakatifu ya Kristo.

“Watheresina, hawa tunao waona leo wameanza kama mbegu ndogo sana ya watu 14, baada ya miaka mine walifunga Nadhiri Takatifu na hadi leo hii tunaadhimisha Jubilei ya miaka 75 masista Watheresina wapo zaidi ya 650 na wanaendeleza wimbi la maendeleo yaleyale na roho ileile na mtazamo uleule wa Mwasisi wao na jamii ya watu wanaoishi nao hawataweza kusahau mchango wa Watheresina kwa kuwa unaonekana”, alisema.

Lakini Askofu Mkuu Mtega anatanabaisha kuwa, elimu waliyokuwa wanapata kwa wakati huo hailingani na elimu ya sasa, hata hivyo anawataka Watheresina ili waweze kuendana na kuuhudumia ulimwengu wa mwananchi wa sasa waende shuleni, wasome na kupata Astashahada, Shahada na Stashahada pamoja na elimu nyingine mbalimbali ili waendane vema na nia na lengo la mwanzilishi wa shirika lao.

Anasema kuwa Watheresina wanafanya kazi mbalimbali za kitume katika nyanja tofauti za afya, elimu ya shule za chekechea, msingi, sekondari, vyuo mbalimbali vya ufundi, kuwafundisha watu Katekesi mafundisho ya dini yenye mizizi kamili ya kiroho ambapo huko wanaleta chachu kubwa ya kuwa na roho njema ya maadili, uaminifu, unyenyekevu na changamoto zingine zote za maendeleo kwa waumini na wananchi kwa ujumla.

Hata hivyo, Askofu Mkuu, Norbet Mtega anawakumbusha watawa hao, wa shirika la Watheresina kuwa wanatakiwa kuwaomba radhi, kutubu kwa jamii ya watu ambao wanaishi nayo kwa kuwa katika kuishi nao kwa namna moja ama nyingine waliwakosea haki za msingi, waliwakwaza na pengine kuleta madhara ya moyoni kwa baadhi ya watu ambayo waliguswa nayo.

“Dunia ya leo inawataka watu watendakazi ambao watakao wafundisha watu kweli na haki namna ya kuwa waaminifu, wanyenyekevu, wapole na wasema ukweli, wanaotambua maana halisi ya sala na kazi na roho hiyo inapatikana kwa Watheresina, lakini mkumbuke kwenda kusoma zaidi kwa kuwa ulimwengu wa leo ni tofauti na ule wa wakati shirika lenu lilipoanzishwa”, anamalizia mahubiri yake Mhashamu Askofu Mkuu, Norbet Mtega.

Mama Mkuu wa Shirika la Watheresina anasemaje kuhusu shirika hilo toka lianzishwe na malengo yake endelevu:
Mwandishi wa Makala haya, alihojiana na Mama Mkuu wa shirika la Watheresina, Sr Bernadetha Kitindi, ambaye hakuficha kueleza bayana uyakinifu wa dhamira ya shirika hilo na malengo yake kwa wanajamii ambapo kila Mtheresina anaishi kuwa anatakiwa kuwa na roho ya sala na kazi, kuelimisha jamii wanayoishi nayo katika nyanja ile aliyopo na kuonesha utukufu wa Kristo kwa watu kwa kuishi kitakatifu zaidi.

Mama Mkuu wa Shirika la Masista Wamisionari la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu hapa nchini na duniani, Sr Bernadetha Kitindi, anasema kuwa ingawaje shirika hilo lilianza sehemu moja ya kijiji cha Tosamaganga, leo hii limeenea katika parokia zote zaidi ya 34 za jimbo Katoliki la Iringa na kutoka masista 14 wa mwanzo sasa wapo zaidi ya masista 650 na wanafanya kazi sehemu mbalimbali.

Mama Mkuu, Sr Bernadetha Kitindi, anafafanua maeneo wanayofanyia kazi kuwa ni pamoja na jimbo katoliki la Njombe, Mbeya, Mpanda, Geita, Tabora, Dar es Salaam na Mwanza ambapo masista wametawanyika kufanya kazi za kitume kwa nia na lengo lilelile la Mwasisi wao katika mataifa tofauti ya nje ya Tanzania ambayo anayataja kuwa ni taifa la Italia na Haiti ambako huku nako Watheresina wanaendelea na kazi yao ya sala na kazi na kuelimisha jamii wanayoishi nayo.

“Ni malengo ya hata vizazi vingine vijavyo tunayo imani kubwa kuwa siku moja Watheresina wataeneo duniani kote na kile alichokitaka Yesu Kristo kupitia mwa Mwasisi wa shirika letu Baba Monsinyole Fransico Cagrielo, lengo hilo lifanikiwe na dunia nzima ipate kushuhudia ukweli wa Kristo na maisha matakatifu tunayotamani hapo baadaye”, alimalizia kusema Sr Bernadetha Kitindi.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...