Thursday, 16 December 2010

MADIWANI SIMAMIENI UTUNZAJI MAZINGIRA- DR. HOVISA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – (Mazingira) Dr. Terezya Luoga Hovisa amewataka madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma kusimamia kwa karibu sana masaula ya utunzaji mazingira katika kata zao zote, kwa kuwa uharibufu wa mazingira ni tatizo la dunia nzima na kuongeza kuwa tunakoelekea ni kubaya zaidi kwa kuwa madhara ya uharibifu wa mazingira yanaonekana zaidi katika jamii.


Hayo yalisemwa na waziri wa mazingira huyo alipokuwa akizungumza na madiwani walipokuwa katika kikao cha kamati cha madiwani kilichofanyika Songea mjini katika Ukumbi wa Tumbaku (NGOMATI).


Waziri huyo alisema kwamba atahakikisha na atasimamia kwa nguvu na juhudi zake zote suala la uharibifu wa mazingira na hivyo madiwani wahamasishe wananchi katika maeneo yao wanakotoka. Aliwataka madiwani hao kuwashauri wananchi wao ambayo sehemu kubwa ni wakulima wadogo wadogo kwamba tabia ya kukata miti yote katika mashamba yao wakati wa kulima na kufanya palizi basi watunze miti kadhaa katika mashamba yao.


Dr. Hovisa alidokeza kwamba wameanza na anaendelea kuwashawishi wahisani mbalimabli kusaidia katika upatikanaji wa nishati mbadala (alternative source of energy), kwa kuwa tatizo la nishati ndiyo chanzo kikubwa cha uharibufu wa mazingira.


Waziri huyo alifika Songea kufuatia taarifa aliyopewa kwamba tarehe 15/12/2010 ingekuwa ni siku ya kuaapishwa kwa madiwani na kuzinduliwa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Songea na badala yake siku ya kuaapishwa kwa madiwani itafanyika kesho Ijumaa.


Wakati huo huo, Chama cha Mapinduzi (CCM) Halmashauri ya Songea vijijni wamemchagua Bw. Rajabu Hassani Mtiula diwani wa Kata ya Mpitimbi kuwa mwenyekiti wa halmashauri katika uchaguzi wa kura za maoni uliyofanyika jana. Bw. Mtiula alipata kura 19 dhidi ya mpinzani wake Bw. Jumanne Alex Nyingo diwani wa Kata ya Litisha aliyepata kura tatu tu.


Msimamizi wa uchaguzi Bi. Lidya Gunda Jonh ambaye pia ni Katibu wa CCM Wilaya ya Songea Vijijini alisema kuwa idadi ya waliopiga kura ilikuwa ni 22 ambapo walikuwa ni madiwani wa kata, madiwani viti maalumu pamoja Mhe. Mbunge Jenister Mhagama (MB Peramiho).


Alisema kuwa kura zilikuwa za siri kubwa kwani walitumia karatasi maalum na kuongeza kuwa wagombea wa nafasi ya mwenyekiti walikuwa wagombea wawili tu waliojitokeza.


Kwa upande wa makamu mwenyekiti, msimamizi wa uchaguzi alimtangaza Bw. Theofani Tadei Mbelwa kuwa makamu mwenyekiti baada ya kupata kura 20 za ndiyo katika kinyang’anyiro ambapo mwenzake alijitoa dakika ya mwisho na kumuunga mkono mwenzake kwa kuwa alikuwa na hoja ya msingi kuliko yeye.


Wakipewa nafasi ya kushukuru wagombea hao kwa pamoja walisema kuwa madiwani wanapaswa kuvunja makundi katika baraza la madiwani na badala yake kujenga umoja na mshikamano na kuachana na sera za kujenga mpasuko katika baraza hilo la Halmashauri ya Songea (W).


Halmashauri ya Wilaya ya Songea vijijni ina jumla ya madiwani 24 wakiwemo madiwani wawili kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...