Wednesday, 3 August 2011

WAFANYABIASHARA SOKO KUU LUDEWA WAMETELEKEZWA VYOO VICHAFU, HAVINA MAJI SOKO HALINA ULINZI.

Wengi sasa wafanyia biashara mtaani na majumbani.
WAKATI Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa ikilalamikia ufinyu wa Bajeti na kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo na huduma muhimu za jamii kwa kukosa raslimali fedha, wafanyabiashara katika soko kuu la mjini hapa wamelikimbia soko na kuamua kufanyia majumbani bila kulipa ushuru kutokana na soko hilo kukosa huduma muhimu za kiutu kama vile choo safi, maji na mlinzi.
Wakizungumza katika soko jipya wafanyabiashara wa mbogamboga, nyanya, vitunguu na matunda walisema wanalazimika kukimbilia majumbani kwao hata kama ni mbali kwa ajili ya kwenda kujisaidia kutoka na soko hilo kuwa na vyoo vichafu vya zamani huku soko jipya nalo likikosa maji wakati vyoo ni vya kuflashi.
”Ndugu mwandishi hebu angalia na uingie wewe mwenyewe ndani ya vyoo hivyo kama unaweza kujisaidia na kuvumilia hali ya uchafu kila siku tunalazimika kwenda majumbani kujisaidia na kisha kurudi kuendelea na biashara.ni hatari sana inasikitisha,” alisema mmoja wa wafanyabiashara kwa masharti ya kutotajwa jina kuhofu kufuatiliwa.
Kwa upande wake Bi Jovita Haule na Neema Haule walisema ni kutokana na adha zilizopo katika soko hilo sasa hivi wafanyabiashara wengi wameondoka na kwenda kufanyia biashara majumbani na kuwafuata wateja waliko mitaani ambako kulipa ushuru ni nadra tofauti na sokoni ambako wanatozwa ushuru hata kama hawajauza.
Bi Auleria Mtitu (mama Grady) aliulaumu uongozi wa kiji na Kata wao ndiyo chanzo cha kuikosesha Halmashauri mapato kwa sababu wameshindwa kulisimamia soko kukidhi haja na kuruhusu watu kufanya biashara mitaani na majumbani ambako siyo rahisi kufuatilia ushuru ukuzingatia kwa sasa wengi wanalima mboga.
Mama Grady na wenzake walisema kuwa hakuna haja ya kulima mboga kama hali itaendelea kuwa kama ilivyo na kuongeza kuwa wakati umefika sasa wa viongozi wenye mamlaka kuwakusanya wafanyabiashara walioko mitaani na majumbani kuja sokoni ili kuleta ushindani wa kweli.””sisi tunalipa ushuru kila siku lakini wenzetu hawalipi mitaani hakuna usawa angalia mwandishi soko liko wazi halina watu kabisa walilalamika wafanyabiashara hao””.
Afisa Mtendaji Kata ya Ludewa Bw Onesmo Haule kwa upande wake alikiri kuwepo kwa wafanyabiashara kuzagaa mitaani na kusema kuwa watu wote wanatakiwa kuleta bidhaa zao sokoni, lakini akajitetea kuwa soko limejaa hakuna nafasi jambo ambalo lilipingwa vikali na wachuuzi hao kwa sababu soko liko wazi sasa limejaa watu wasioonekana? Waliuliza wachuuzi hao
Kuhusu ulinzi wa soko Bw Haule alisema hilo siyo jukumu la Halmashauri bali ni wajibu wa wafanyabiashara wenyewe kutafuta mlinzi wa kulinda mali zao na kwamba utaratibu huo walishakubaliana katika vikao vilivyopita chini ya uongozi wa soko hilo.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara sokoni hapo mzee Masopola kwa upande wake alisema kwa upande wa vyoo hiyo ni hadithi ya muda mrefu sana na viongozi wamekuwa wakiahidi kila wanapoomba kura lakini hakuna kinachoendelea na wala hawatembelei kuona hali ilivyo.
Masopola alisema vyoo vilivyopo vimechoka mpaka vimechakaa na sasa vimezungushwa na mabati machakavu na kuongeza viongozi wamalazimisha watu kuingia katika soko jipya lakini huduma za msingi kama maji, vyoo na mlinzi hakuna hivyo watu wanalazimika kujitwisha mizigo kila siku kuleta sokoni na kurudisha na kushauri kuwa kama kuleta maji ni vigumu ni bora vichimbwe vyoo vya shimo.
”Mapungufu yapo pande zote kwa serikali na kwa wafanyabiashara hivyo kuna haja ya kukaa pamoja kuwaelimisha watu wajibu na haki zao lakini kwa upandewa serikali ijue wajibu zake na kuziweka bayana ama sivyo soko litabaki wazi kwa sababu mapungufu haya yalianza wakati wa kulikabidhi soko jipya hapakuwa na maandaliza wala utaratibu,”alisisitiza mzee masopola
                               

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...