Mratibu wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Mkoa wa Ruvuma Bwana
Emmanuel Petro amesema kuwa ili kupunguza kasi ya maambukizo ya Virusi
Vya Ukimwi mkoani hapa halmashauri na wadau wengine wa Ukimwi hazina
budi kufanya kazi kwa pamoja.
Alisema kuwa ili kufanikisha mkakati wa taifa wa kinga dhidi ya VVU
halmashauri na wadau wengine wanapaswa kufanya kazi kwa karibu na
hatimaye kuweza kupunguza maambukizo haya.
Mratibu TACAIDS (M) huyo alitoa rai jana katika kikao cha kupitia
mipango ya shughuli za Ukimwi za Halmashauri kilichofanyika Peramiho
kikihusisha Waratibu wa Ukimwi Kinga Wilaya (CHAC) na Waratibu wa
Ukimwi-Tiba katika ngazi ya wilaya yaani (DACC) wa kutoka Halmashauri
zote za Wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma yaani Songea Manispaa, Songea
Vijijini, Namtumbo, Mbinga na Tunduru.
Alisema kuwa lengo la kikao hicho cha siku mbili ni kupima shughuli
za Ukimwi za halmashauri kama zinaendana na miongozo ya kitaifa,kama vile
vile Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi-2009-2012 na Mkakati wa
Taifa wa Kinga ya Virusi Vya Ukimwi.
“Mkakati wa Taifa wa Kinga ya VVU unaweka fursa na mwongozo wa
kuongeza maradufu juhudi za taifa za kuzuia idadi ya maambukizo ya
VVU. Dira inatokana na ile ya mkakati wa taifa wa kudhibiti
UKIMWI-Tanzania bila ya maambukizo ya VVU- kwa kupunguza kiwango na
idadi ya mambukizo ya VVU kwa asilimia 25 ifikapo mwaka 2012. Mkakati
huu ni matokeo ya ushirikiano wa sekta ya umma, binafsi na vyama vya
kiraia, kwa kuidhinishwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS),” kwa
mujibu wa taarifa kutoka TACAIDS.
Bw. Petro aliongeza kuwa lengo la hatua zote hizo ni kuhakikisha
kwamba harakati za mapambano dhidi ya vvu na ukimwi zinaendeshwa kwa
kuzingatia miongozo ya serikali kwa kuwashirikisha wadau wote na
wananchi kwa ujumla, kwa kupitia utaratibu wa uandaaji wa mipango
shirikishi jamii kwa mfumo wa fursa na vikwazo kwa maendeleo ambayo
ndio dhana ya kuishirikisha jamii katika kushiriki kikamilifu katika
kuibuia matatizo na fursa zilizopo katika kuwa na mipango mizuri
katika kudhimbiti UKIMWI katika mkoa wetu.
“Janga la UKIMWI limedhihirika kugusa sekta zote za jamii na hivyo
kuwa suala mtambuka katika shughuli zote za kiuchumi, kijamii na
kiutamaduni.”
Lakini pia Mratibu huyu ameziagiza halmashauri pamoja na wadau wengine
wanaoshuhulikia masuala ya Ukimwi zitenge fedha katika bajeti zao za
kwa ajili ya masuala ya Ukimwi badala ya kutegemea wafadhili peke yao
ambapo kwa kufanya hivi watakuwa wamepunguza kasi ya maambukizo mapya
ya ugonjwa huu.
Katika kufanikisha azma wananchi na viongozi wanapaswa kuwa mstari wa
mbele katika kujitokeza katika vituo mbalimbali vya kupima na kupokea
ushauri nasaha ili kuweza kujua afya zao na hatimaye kupanga mikakati
stahiki ya maisha yao, ambapo kwa wote wanaokutwa na Virusi vya Ukimwi
Serikali inatoa bure dawa ya kurefusha na kupunguza makali ya virusi
vya Ukimwi (ARVs) katika vituo vya kutolea huduma hiyo.
Mkoa wa Ruvuma una maambukizi ya virusi vya Ukimwi asilimia 5.8%
wakati kitaifa ni 5.7% ambapo kasi ya maambukizi ya ugonjwa huu kimkoa
inazidi ile ya Taifa kwa asilimia 0.1% kutokana na utafiti wa
viashiria vya VVU/UKIMWI na Malaria ya kitaifa uliyofanyika mwaka
2007/2008 (THIS).
No comments:
Post a Comment