HAYATI DIETRAM HOFMANN OSB
Na Friday Simbaya, Songea
ABASIA ya Peramiho ya Mtakatifu Benedkto
imepata pingo baada ya aliyekuwa Padri Dietram (Alfred) Hofmann OSB kufariki
dunia jana mnamo saa 5.45 asubuhi.
Kwa mujibu wa Abate Anastasius Reizer OSB alisema kuwa marehemu Padri
Hofmann alifariki dunia katika nyumba ya kutunzia wazee watawa (infirmary) hapa
Peramiho akiwa na umri wa miaka 83.
Marehemu alizaliwa tarehe 13 Oktoba 1929
huko Weisbrunn katika Jimbo la Würzburg / Ujerumani katika familia ya wakulima
wadogo akiwa mmoja kati ya watoto 9. Kaka yake, Hayati Pd. Ludger, alimtangulia
kuingia Abasia ya Münsterschwarzach. Baada ya kuhitimu masomo yake ya sekondari
kijana Alfred naye alijiunga na Abasia ya Münsterschwarzach na kupewa jina
Dietram alipoingia unovisi mwaka 1948. Tar. 8 Septemba 1949 alifunga nadhiri
zake za kwanza.
Baada ya
kusoma falsafa katika Chuo Kikuu cha Abasia ya Mt. Ottilien alitumwa Roma
kuendelea na masomo ya teolojia katika Chuo cha Mt. Anselmo. Tar. 4 Julai 1954
alipata daraja la upadre huko Münsterschwarzach. Baadaye aliendelea na masomo
ya Biblia huko St. Anselmo na katika Chuo cha Biblicum akajipatia shahada ya
juu (udaktari) katika fani ya Maandiko Matakatifu.
Mwaka
1959 P. Dietram aliteuliwa kwa ajili ya kazi ya umisionari katika Abasia
Peramiho. Baada ya kipindi cha kujifunza lugha ya kiingereza huko London
aliwasili hapa Peramiho tarehe 23 Februari 1960. Alitumwa Parokia Matimira
alikohudumia kwa mwaka mmoja wakati anajifunza lugha ya Kiswahili. Kisha
alitumwa katika Chuo cha Makatekista Mgazini na kufundisha huko mpaka 1965.
Hapo ndipo alipoanza huduma yake kwa muda wa miaka 25 katika Seminari Kuu hapa
Peramiho (1965-1990). Muda wote huu alikuwa mwalimu hodari wa Maandiko
Matakatifu /Agano la Kale kwa vizazi vya waseminari. Pia alifundisha masomo
mengine kama vile katekesi na namna ya kuhubiri. Hayati Askofu Mkuu J.J. Komba
mara nyingi alitumia utaalamu wa P. Dietram katika kuandaa barua zake za
kichungaji. Aidha, alitumikia katika kamati mbalimbali za jimbo.
Mwaka
1990 P. Dietram alitumwa na wakubwa wake Uwemba kwa ajili ya kuwasaidia ndugu wa
huko kama procurator(mhasibu). Kwa muda fulani alisaidia pia katika nyumba ya
Wabenediktini huko Kurasini / Dar es Salaam. Muda wote alipokuwa mwalimu au
kufanya kazi ya procura, marehemu alisaidia pia kazi za uchungaji akiwa mhubiri
hodari aliyefundisha Neno la Mungu kwa ufasaha.
P.
Dietram alikuwa mpenda amani, mpatanishi. Daima alisimama kwenye ukweli. Pia,
alikuwa makini sana kusali Sala ya Kanisa na kushika kanuni mbalimbali za
liturjia.
No comments:
Post a Comment