Tuesday, 8 January 2013

WANACHAMA 150 WA CCM PERAMIHO WATIMKIA CHADEMA



Na Friday Simbaya, Songea
Jumla ya wanachama 150 wa Chama cha Mapinduzi (CCM), vijana kwa wazee wa Kata ya Peramiho wamekata shauri na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kati yao 130 wamerudisha kadi za CCM na wengine 20 ni wanachama wapya, wakati wa mkutano wa hadhara  uliofanyika eneo la Namihoro sokoni, Wilaya ya Songea (V) mkoani Ruvuma juzi.

Kada na mpigadebe wa CCM maarufu, Margret Ndomba (kushoto) akipeana mkono na Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa (NEC CHADEMA), Edson Mbogolo baada aliyakurudisha kadi tatu za CCM, yaani kadi ya UVCCM, kadi ya UWT na CCM wakati wa mkutano wa hadahra wa chama hicho uliyofanyika Namihoro katika Kata ya Peramiho Wilaya Songea, Mkoani Ruvuma juzi.


Miongoni mwa wanachama waliorudisha kadi za CCM na kuamua kujiunga na Chadema ni Mwenyekiti mstaafu wa CCM wa Tawi la Peramiho, Bruno Mwitumba pamoja na kada wa CCM Margret Ndomba aliyerudisha kadi tatu; kadi ya UVCCM, kadi ya UWT na CCM.

Akiwakabidhi na kuwapokea wanachama hao, Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa (CHADEMA), Edson Oswald Mbogolo alisema kuwa wanachama hao waliohamia Chadema wamefanya hivyo kwa maamuzi sahihi kwa kuchagua maendeleo, na kuongeza kuwa wameamua kutoka ‘analojia kwenda digitali.’

“Wananchi hawa waliojiunga na Chadema kwenda ‘digitali kutoka analojia’ kwa maana ya kutoka CCM kwenda Chadema kama nchi yetu na nchi za Afrika Mashariki mzima ilivyoamia digitali wanajitambua…”, aliongeza Edson Mbogoro.

Alisema kuwa mwaka 2014 utachukuliwa kama ni mwaka wa Chadema na kipimo tosha cha kuchukua dola katika chaguzi za serikali za mitaa kwa nafasi mbalimbali katika ngazi zote na hatimaye Uchaguzi Mkuu 2015.

Alidai kuwa wananchi wa Kata ya Peramiho wameamua kujiunga na Chadema kwa sababu Mbunge wao wa Jimbo la Peramiho, Jenister Mhagama amewatelekeza.

Aliwambia wakazi wa Jimbo la Peramiho kujiunga na Chadema ili waweze kuunganisha nguvu kwa pamoja kuondoa watawala pamoja na mbunge wa jimbo hilo.

“Ndugu zangu wanaPeramiho siasa sio usanii kama wanavyofanya kina Majuto kumbe siasa ni uhai wetu, siasa ni maisha yetu…” alisisitiza mjumbe huyo wa kamati kuu taifa.

Naye Katibu waChadema Wilaya ya Songea Mjini, Masumbuko Mbogolo alisema kuwa wananchi  wake kwa wanaume wa Jimbo la Peramiho kuwa wanabudi  ya kuchagua upinzani kwa maendeleo ya jimbo lao, kwa sababu kwa muda mrefu jimbo hilo liko nyuma kimaendeleo.

Alisisitiza kuwa mahala ambapo wananchi wamechagua upinzani pana maendeleo kwa kutoa mifano michache ya Moshi mjini, Karatu  na Kijiji cha Liweta ambacho kipo kilometa chache kutoka Peramiho, ambacho kina maendeleo kwa sasa baada ya kuchagua upinzani na mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho ni wa Chadema.

“Kijiji cha Liweta ambacho kipo kilometa chache kutoa hapa Peramiho waliamua kuchagua upinzani baada ya miaka mingi ya kutawaliwa na CCM, kwa sasa wananchi wa kijiji hicho wana maendeleo, wamepata maji safi na salama baada ya kuchimbiwa visima, wamechongewa barabara na wanasubiri kujengewa zahanati kutokana na kelele za Chadema,” alisema Masumbuko Mbogolo.

Kuhusu mbolea, Katibu wa Wilaya ya Songea Mjini alisema kuwa wananchi wa Jimbo la Peramiho na kwingineko hawawezi kuwa na kilimo chenye tija kwa sababu gharama za pembejeo na mbolea ziko juu ukilinganisha na Malawi na Zambia wakati wote wanaagiza mbolea hizo kutoka China na Japan.

Alitoa mfano kuwa, kule Malawi mfuko moja wa mbolea unauzwa shilingi elfu nane tu wakati Tanzania mfuko mmoja wa mbolea unauzwa kati ya shilingi elfu 65 hadi 70, wakati Malawi na Zambia wanapitisha mbolea kupitia Tanzania na wanalipa kodi kwa Tanzania kwa kupitisha mizigo yao.

Katika hatua nyingine, Katibu huyo wa Wilaya ya Songea Mjini alipata nafasi ya kufafanua maana ya rangi nne za bendera ya chama hicho (Chadema) kwa wananchi wa Jimbo la Peramiho.

 Alifafanua kuwa rangi nyeupe kwenye bendera ya chama hicho ni alama na ishara ya amani, rangi nyeusi katika bendera hiyo ni alama ya watu, rangi ya Bluu inaonyesha alama ya utajiri wa asili wa nchi ya Tanzania  na rangi nyekundu ni alama ya damu iliomwagika kutoka kwa baadhi ya wapigania Uhuru wa nchi hii kama vile Mkwawa na wengineo.

Mwisho

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...