Na Benedict Liwenga, MAELEZO-DSM.
TEHAMA ni moja kati ya Sekta zinazokua kwa
kasi hapa nchini na duniani kote na imekuwa ikichangia kikamilifu katika
maendeleo ya Taifa na pia imekuwa ikiwezesha sekta nyingine kukua na kuboresha
maisha ya wananchi na huduma za jamii kwa ujumla.
Kutokana na ukuaji wa Sekta hii, jitihada
za makusudi zinahitajika katika kusimamia na kuratibu shughuli za TEHAMA ili
nchi iweze kunufaika zaidi kwani mchango wa sekta hiyo unaweza kuwa mkubwa kama
TEHAMA na matumizi yake yataratibiwa, kusimamiwa na kuendelezwa vyema zaidi
kuliko hali ilivyo sasa.
Katika kuhakikisha masuala ya TEHAMA nchini
yanaratibiwa, kusimamiwa na kuendelezwa vyema, Serikali iliona ni vema ikaundwa
Tume ya TEHAMA (ICT Commission).
Tarakilishi “Computer”
katika lugha ya Kiswahili ni kifaa ambacho kimebadilisha
mfumo wa maisha ya binadamu katika miongo takribani sita iliyopita.
Kutokana na kuwepo kwa
kifaa hiko dunia imejikuta katika maendeleo makubwa kabisa kuliko kipindi
chochote kile katika historia ya kuwapo kwake.
Bila shaka kila
mwanadamu katika dunia hii anafahamu ukuaji mkubwa na uwezo wa mawasiliano
ambao umeleta mapinduzi makubwa katika ukuaji wa chumi za nchi na mwingiliano
wa jamii moja kutoka jamii nyingine.
Ni maendeleo haya ya
kiteknolojia ambayo yamesababisha utandawazi ambao hakika umeifanya dunia
kuonekana kama kijiji kidogo kilicho na jamii nyingi zenye taratibu, maendeleo,
mila na desturi na siasa tofauti.
Kwa kimombo Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano inafahamika kama Information
Technology au IT kwa kifupi na Kwa
Kiswahili teknolojia hiyo inafahamika kama TEKNOHAMA.
TEHAMA duniani imeanza
kupiga hatua ya kasi sana toka mwishoni mwa Karne ya ishirini na imeleta
mabadiliko makubwa katika nyanja za mawasiliano, uchumi, tafiti na ukusanyaji
wa takwimu mbalimbali.
Pamoja na uwepo wa
sheria ya 1974 iliyokuwa ikipinga uagizwaji wa vifaa vya tarakilishi zenyewe na
seti za runinga, mfumo wa mabadiliko mbalimbali ndio uliopelekea Tanzania
kupiga hatua ya kutosha katika kuboresha mfumo wa habari.
Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2003 inaelekeza
kuundwa kwa chombo cha TEHAMA ikiwemo juhudi na programu mbalimbali
zinazoendelea hapa nchini zinazohitaji utaratibu wenye ufanisi.
Jitihada za kuanzisha Tume zililenga
kutekeleza Sera ya Taifa ya TEHAMA pamoja na maazimio mbalimbali ya kitaifa na
kimataifa ikiwemo maagizo ya Mkutano wa Dunia wa Jamii Habari (World Summit on Information Society).
Aidha, jitihada mbalimbali zimefanywa na
Serikali katika kuhakikisha Sekta ya TEHAMA inakua nchini na miongoni mwa
jitihada hizo ni pamoja na uanzishwaji wa vituo vya Mawasiliano vya Jamii (Community Telecentres), ujenzi wa
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (National ICT Broadband Backbone-NICTBB),
Uanzishwaji wa Wakala wa Serikali wa Mtandao, Uanzishwaji wa Vituo vya Kutunzia
kumbukumbu za TEHAMA (Data centres), na Mradi wa Anwani za Makazi na Simbo za
Posta.
Tume hii inalenga
kutambua na kuvutia fursa za uwekezaji katika TEHAMA, kutoa ushauri, kuendeleza
rasilimali watu kitaifa kwenye sekta ya TEHAMA, kuendeleza program za kitaifa
za TEHAMA na kushiriki katika kuendeleza miundombinu mbalimbali ya TEHAMA yenye
sura ya kitaifa kwa kushirikisha wadau wa sekta zote.
Kwa sasa, Idara za Serikali,
Mashirika, na Asasi za aina zote zimejitahidi kuwa na tovuti zao, ili wananchi
wapate habari za vyombo hivyo kupitia mtandao huo wa kompyuta.
Serikali
imeanzisha uhamasishaji na uendelezaji wa wataalam wa TEHAMA (ICT Professionals) katika taasisi za
Serikali na sekta binafsi ili kujenga rasilimali watu nchini itakayowezesha
kutumia fursa na rasilimali za TEHAMA vizuri na kwa manufaa zaidi.
Kwa
upande wa Serikali, Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine wa TEHAMA imekamilisha
Muundo wa Utumishi wa teknohama ambao tunaamini utatoa fursa mahsusi katika
kuendeleza watumishi wa fani hiyo ambao ina jukumu kubwa sana katika maendeleo
ya nchi yetu katika zama hizi za TEHAMA.
Mafanikio katika jitihada hizo yamekabiliwa
na changamoto nyingi ikiwemo kutokuwepo kwa chombo mahususi kinachoratibu,
kusimamia na kuendeleza TEHAMA nchini.
Ni dhahiri kuwa sekta ya Mawasiliano
inakuwa kwa kasi kubwa sana duniani kote na hapa nchini kwetu, na hivyo kufanya
baadhi ya mambo kuwa na changamoto katika utekelezaji wake hususan kutokuwepo
na uratibu wa kitaifa katika miradi na program zenye sura ya kitaifa.
Kukosekana kwa mpango wa Kitaifa wa
usimamizi wa kuhakikisha kuwa mifumo ya TEHAMA inawasiliana na hatimaye kuepuka
upotevu wa rasilimali unaotokana na taasisi mbalimbali kufanya kitu kile kile.
Changamoto nyingine ni kutokuwapo na
usimamizi, usajili wa kitaifa wa kuendeleza weledi kwa wataalamu wa TEHAMA na
kuhakikisha utoshelevu wa rasilimali watu utakaokidhi mahitaji ya maendeleo ya
TEHAMA, pia kutokuwepo chombo mahususi chenye majukumu ya kisheria.
Tume ya Teknolojia, Habari na Mawasiliano
itasaidia kukuza uchumi wa Taifa kutokana na kukua kwa sekta ya TEHAMA na
kuchochea uzalishaji, ukuaji wa sekta zingine kiuchumi na usambazaji wa huduma
za jamii; kuwa na taifa la jamii habari, lenye wataalam wanaotambulika kitaifa
na Kimataifa, na wajasiriamali katika Nyanja mbalimbali za TEHAMA kuendana na
kasi ya ukuaji wa teknolojia duniani; kuwa na uhakika wa usalama katika
matumizi ya TEHAMA na kuwepo na mfumo unaoainisha na kuendeleza uwekezaji
katika sekta ya TEHAMA kitaifa.
Tume hii inatarajia
kuondoa changamoto nyingi na kujenga mfumo utakaowezesha uwekezaji wa
kushirikisha sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano na
TEHAMA yenye sura ya kitaifa; Kuwepo mfumo utakaowezesha wabunifu na
wajasiriamali kuendeleza sekta ya TEHAMA; na kuweka utaratibu na miongozo ya
namna bora ya kuhifadhi vifaa chakavu vya TEHAMA (e-waste management).
“Miongoni mwa mambo muhimu na
ya msingi katika kuratibu sekta ya TEHAMA nchini, tume ya TEHAMA inatakiwa
ihakikishe inaunda Bodi ya Wataalamu wa TEHAMA ambao watasajiliwa na kufahamika
kisheria ili kulinda weledi na maadili ya usambazaji na ubora wa huduma za
TEHAMA zinazotolewa kwa jamii”, alisema Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia Mhe. January Makamba alisema
Kwa namna hiyo, tume itakuwa
imesaidia kuwa na Taifa Habari lenye wataalam waliounganishwa na chombo kimoja
na hivyo basi kuongeza wigo na dhamana ya uwajibikaji kwa huduma zitolewazo kwa
jamii.
Mhe. Makamba aliongeza kuwa
Tume ya Teknnolojia ya Habari na Mawasiliano pamoja na mambo mengine itatakiwa
iendelee kuleta mabadiliko na maboresho
katika nyanja ya mawasiliano na habari kwa kuhakikisha inafuta na kuondoa uwepo
wa vyuo visivyo na hadhi (feki) vinavyotoa elimu ya sayansi na teknolojia
isiyokidhi viwango vinavyotakiwa katika kuboresha sekta ya TEHAMA.
Tatizo la kuwepo na uanzishwaji
wa vyuo vya masuala ya habari ambavyo kimsingi havina ubora na havifuati Sera
ya Habari na Mawasiliano iliyoanzishwa 2003 na hivyo basi kutengeneza wataalamu
wasioweza kuendana na kasi ya mabadiliko katika nyanja ya mawasiliano nchini.
Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ilikabidhiwa dhamana ya kuhakikisha kwamba Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano, Sayansi, Teknolojia na Ubunifu vinachangia kikamilifu
katika maendeleo ya nchi yetu.
Pamoja na jukumu hilo,
Wizara hii imepewa dhamana ya kusimamia Taasisi, Mashirika, Tume na Kampuni ambazo zinachangia juhudi za Wizara
katika kuyafikia malengo na matarajio ya
wananchi. Taasisi hizo ni: Taasisi ya
Teknolojia Dar es Salaam (DIT); Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Mbeya (MIST),Taasisi
ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela - Arusha (NM-AIST); Tume ya Nguvu za
Atomiki Tanzania (TAEC); Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH);
Shirika la Posta Tanzania (TPC); Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL); Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA); na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCAF).
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara hiyo, Serikali imeendelea kujenga
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, ujenzi ambao ulianza rasmi mwezi Februari 2009.
Awamu ya Kwanza ya ujenzi wa mkongo wa mawasiliano imekamilika na huduma za
mawasiliano zimeanza kutolewa. Katika awamu hii, jumla ya kilometa 4,300 za
Mkongo katika Mikoa 16 zimejengwa. Mikoa hiyo ni: Dar es Salaam, Pwani,
Morogoro, Iringa, Mbeya, Dodoma, Singida, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga,
Shinyanga, Mwanza, Tabora, Mara na Kagera.
Taarifa zilisema kuwa, kabla ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
kuwepo na kabla ya Mikongo ya Baharini kuunganishwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano,
gharama za simu kwa sekunde moja zilikuwa kati ya shilingi 2.50 na shilingi
3.00.
Aidha, gharama za mtandao wa intaneti zilikuwa shilingi 12,400,000
kwa kiwango cha sita (6) mega bits/sec dedicated internet bandwidth
ambapo hivi sasa, gharama ya simu na matumizi ya mtandao zimepungua.
Serikali
kupitia wizara husika imekamilisha tathmini ya uanzishwaji wa Mtandao wa Elimu na
Utafiti (National Education and Research
Network-NREN) utakaounganisha vyuo vikuu na vituo vya utafiti 27 katika
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kupitia Mradi wa Sayansi Teknolojia na Elimu ya
Juu unaofadhiliwa na Benki ya Dunia katika
jitihada za Serikali kupeleka huduma za mawasiliano hadi vijijini, Serikali
imeanzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCAF).
Madhumuni
ya Mfuko huu ni kusaidia juhudi za upelekaji mawasiliano ikiwa ni pamoja na
kutoa ruzuku kwa wawekezaji watakaokuwa tayari kupeleka huduma za mawasiliano
maeneo ya vijijini na baadhi ya maeneo ya mjini yasiyokuwa na mvuto kibiashara.
Hadi
sasa Mfuko umeainisha vijiji 239 katika mikoa 17 ambayo ni Dodoma, Arusha,
Tanga, Morogoro, Pwani, Lindi, Ruvuma, Iringa, Mbeya, Singida, Tabora, Rukwa,
Shinyanga, Kagera, Mara, Manyara na Kigoma (Kiambatisho Na.10). Aidha, vijiji 139
vimechaguliwa kwa ajili ya mradi wa majaribio (pilot project). Uhakiki wa
maeneo mengine unaendelea.
Mabadiliko
na maboresho katika teknologia ya habari na mawasiliano Tanzania yametokana
juhudi madhubuti zilizofanywa na serikali sambamba na hitaji na malengo ya
millenium na Dira yake ni kuhakikisha
maisha bora kwa kila Mtanzania katika nyanja mbali mbali yanafikiwa ifikapo
2025.
-MWISHO-
No comments:
Post a Comment