|
Jesca Msambatavangu, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa |
PAZIA la
kinyang’anyiro cha ubunge jimbo la Iringa Mjini katika Uchaguzi Mkuu wa
2015 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) linaelekea kufunguliwa baada ya
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu kuthibitisha
kuwania nafasi hiyo.
Akizungumza na wanahabari wakati akitoa taarifa ya ziara ya Katibu Mkuu
wa CCM Taifa, Abdulaman Kinana mkoani hapa, Msambatavangu ambaye pia ni
diwani wa Kata ya Miyomboni mjini Iringa alisema; “nitagombea.”
Alitoa
jibu hilo baada ya kuulizwa na wanahabari hao kama ana azma hiyo
kufuatiwa kuwepo kwa tetesi zinazomuhusisha na kinyang’anyiro hicho
kinachotarajiwa kuwa na mchuano mkali ndani ya chama hicho.
Kama
atatimiza azma yake hiyo, Msambatavangu atakuwa anaingia kwa mara ya
pili katika kinyang’anyiro hicho ikikumbwa kwamba katika kura za maoni
za chama hicho za mwaka 2010 zilizoshirikisha wagombea 12 alishika
nafasi ya nne baada ya kujipatia kura 916, nyuma ya Frederick
Mwakalebela aliyepata kura 3,897, Monica Mbega 2,989 na Dk Yahaya Msigwa
aliyepata kura 1,217.
Wengine
walioshiriki kinyanganyiro cha 2010 na kura zao kwenye mabano ni Fadhili
Ngajilo (536), Addo Mwasongwe (383), Zuberi Mwachula (324), Benigus
Mpete (242), Thomas Kimata (201), Chelestino Mofuga (192), Dk Raphael
Kalinga (169) na John Kiteve (136).
Katika
kinyang’anyiro cha mwakani mbali na Msambatavangu aliyethibitisha
kuwania nafasi hiyo wengine wanaotajwatajwa ni pamoja na Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM, Mahamudu Madenge ambaye hata hivyo amenukuliwa
mara kadhaa akisema; “muda haujafika, hayo ni mambo ya mwakani kama
tutakuwa hao, kazi tunayoendelea nayo sasa ni ya kuimarisha chama.”
Mbali na
Madenge, makada wengine wanaotajwatajwa ndani ya chama hicho ni pamoja
na Nuru Hepautwa anayefanya kazi zake zikiwemo biashara jijini Dar es
Salaam na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) Frederick Mwakalebela.
Pamoja
nao yupo pia Dk Yahaya Msigwa, Fadhili Ngajilo na Mbunge wa Viti Maalumu
Mkoa wa Iringa, Ritta Kabati ambaye amenukuliwa mara kadhaa akisema
atajitosa katika jimbo la Iringa Mjini au Kilolo kama viti maalumu
vitafutwa.
Katika
mkutano wa hadhara alioufanya Januari 27, mwaka jana, Makamu Mwenyekiti
wa CCM Tanzania Bara, Phillip Mangula atoa ruksa kwa wana CCM wanaotaka
ubunge na udiwani katika majimbo na kata zinazoshikiliwa na wapinzani
kuanza kupitapita ili kutafuta ushawishi.
Wakati
akitoa ruksa hiyo, Mangula aliuliza “…Iringa tulishindwaje jimbo hili,
alitokea pepo gani, naomba mkemee pepo hao waliosababisha tushindwe ili
2015 turudishe jimbo letu.”
Akizungumzia ukomo wa ruksa hiyo, Mangula alisema haihusu nafasi ya Rais na majimbo na kata zinazoongozwa na wana CCM.
“Nimeambiwa wapo walioanza kujenga makundi ndani ya chama kwa ajili ya
Uchaguzi Mkuu ujao. Napenda kurudia tena ni marufuku kwa wanaCCM
kuwabugudhi wanaCCM wenzao waliopo madarakani,” alisema.
Katika
mkutano huo uliofanyika katika uwanja wa Mwembetogwa, Mangula alisema
wanaCCM wanaojipitisha kwenye maeneo yanayoongozwa na viongozi wa CCM,
wataenguliwa hata kama watashinda kura za maoni kwa ajili ya Uchaguzi
Mkuu wa 2015.
Alisema kujipitisha katika maeneo wanayoyaongoza kunakibomoa chama hicho kwasababu ni chanzo kikubwa cha makundi.
“Mgogoro
mkubwa ndani ya CCM ni makundi, makundi haya hujengwa kipindi cha
kuelekea uchaguzi, hayana la maana zaidi ya kutubomoa. Hivi sasa
nimeambiwa wapo walioanza kujenga makundi,” alisema.
Kinana
na ujumbe wake wanatarajia kufanya ziara ya siku tatu mkoani Iringa
ambayo pamoja na mambo mengi inalenga kukiimarisha chama hicho kwa
kupokea na kuwaapisha wanachama wapya wakiwemo wanaotaka kujitoa kutoka
vyama vya upinzani.
Ziara
hiyo kwa mujibu wa Msambatavangu itaanzia wilayani Mufindi Oktoba 6,
mwaka huu na kuendelea katika wilaya ya Kilolo na Iringa Vijijini kabla
ya kuhitimishwa Iringa Mjini. (BONGOLEAKS)
No comments:
Post a Comment