Friday, 26 September 2014

PROGRAMU YA PANDA MITI KIBIASHARA YAANZA KUTEKELEZWA KATIKA WILAYA SITA


Moja ya kitalu cha kuotesha miche ya miti kilichopo katika kijiji cha Kifanya wilayani Njombe; kitalu hicho ni cha wakulima wanaounda umoja wa wapanda miti Kifanya
Meneja Mawasiliano wa Mradi, George Matiko akifafanua jambo kwa wanahabari; aliyeketi ni Mkurugenzi wa Programu hiyo, Dk Maria Tham
Dk Maria Tham katika mahojiano na wanahabari ndani ya ofisi zao zilizopo mjini Njombe
Mwenyekiti wa kikundi cha wapanda miti wa kijiji cha Kifanya akitoa ufafanuzi wa shughuli zinazofanywa na kikundi chao
PROGRAMU ya Panda Miti Kibiashara imeanza kutekelezwa katika wilaya mbalimbali za mikoa ya Iringa, Njombe na Morogoro.
Wilaya hizo kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Programu hiyo yenye makao yake makuu mjini Njombe, Dk Maria Tham ni pamoja na Makete, Njombe na Ludewa kwa mkoa wa Njombe.
Wilaya zingine ni Kilolo na Mufindi kwa mkoa wa Iringa na Kilombero kwa mkoa wa Morogoro.
Dk Tham alisema lengo kuu la program hiyo iliyoanza Januari mwaka huu ni kuongeza kipato vijijini kutokana na kupanda miti kitaalamu kwa kutumia mbegu bora na kuhudumia mashamba ipasavyo kwa kuzingatia mipango ya matumizi endelevu ya ardhi.
 “Uwezo wa kufikia lengo kuu la program ni mkubwa kwa kuwa katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuna udongo unaofaa kukuza miti, mvua za kutosha, ardhi ya kutosha na wakazi wake wanapenda kupanda miti,” alisema.
Alisema kwa kupitia program hiyo mipango ya matumizi endelevu ya ardhi itatengenezwa huku wananchi wanaopanda miti wakihamasishwa kuunda vikundi vya wakulima wa miti kwa nia ya kufanikisha shughuli za upandaji miti.
Katika kipindi cha miaka minne kuanzia sasa wananchi katika wilaya hizo watahamasishwa kupanda miti katika eneo lenye ukubwa wa hekta 15,000.
“Huku wakihimizwa kuanzisha shughuli mbalimbali za kujiongezea kipato wakati wakisubiri miti yao ikue na kufikia umri unaofaa kuvunwa,” alisema.
Alisema biashara ya miti itaongezeka kwa kuzingatia kwamba ifikapo mwaka 2025 inatarajiwa mahitaji ya malighafi viwandani na kuni yataongezeka kutoka mita za ujazo milioni 1.5 hadi milioni 3.7.
Baadhi ya wakulima wasema wameupokea mradi huo kwa mikono miwili na wakaahidi kutoa ushirikiano ili malengo yake yafanikiwa kwa faida yao na Taifa kwa ujumla. (BONGOLEAKS)

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...