Friday, 26 September 2014

SERIKALI YAZINDUA KAMPENI YA UPIMAJI VVU MAHALI PA KAZI

Katibu Mkuu Utumishi George Yambesi(kulia) akipewa ushauri nasaha kabla ya kupima VVU kwa hiari wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Kuhamasisha Upimaji VVU Mahali pa Kazi uliofanyika mjini Njombe juzi
Akitoa nasaha zake kwa wawakilishi wa mikoa ya Iringa na Njombe walioshiriki uzinduzi wa kampeni hiyo
Hilda Kapanda mmoja wa watumishi wa halmashauri ya Njombe anayeishi na VVU akitoa ushuhuda wake

Huyu Anjela Kayombo ambaye pia ni mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe anayeishi na VVU tangu mwaka 1999
Baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo wakiwa katika foleni wakisubiri kupima afya zao wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo
KAMPENI ya kuhamasisha Upimaji wa Virusi vya Ukimwi mahali pa kazi imezinduliwa kitaifa mkoani Njombe huku baadhi ya watumishi wenye maambukizi hayo wakilalamika kutelekezwa.
Kauli Mbiu ya kampeni hiyo iliyoanza Septemba 23 na itakayofanyika hadi Desemba 1, mwaka huu inasema “mfanyakazi jitambue, pima mapema, epuka maambukizi mapya, ubaguzi na unyanyapaa, zuia vifo vitokanavyo na Ukimwi.”
Alipokuwa akiizindua kampeni hiyo Katibu Mkuu Utumishi, George Yambesi alisema kampeni hiyo inalenga kutoa msukumo wa utekelezaji wa mikakati ya kudhibiti Ukimwi kitaifa na kimataifa ili kufikia azma ya sifuri tatu.
“Sifuri tatu kwa maana ya maambukizi mapya sifuri, vifo sifuri na unyanyapaa sifuri ifikapo mwaka 2015,” alisema mbele ya wawakilishi wa mikoa ya Njombe na Iringa waliohudhuria uzinduzi huo.
Wakati mkoa wa Njombe unaongoza kitaifa kwa kuwa na asilimia 14.8 ya maambukizi, mkoa wa Iringa ni wa pili kitaifa kwa kuwa na asilimia 9.1 ya maambukizi.
Alisema kampeni hiyo inahimiza utekelezaji wa dhati wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) na maazimio yaliyowekwa kwenye Mkutano Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu UKIMWI uliofanyika mwaka 2001 Jijini New York, Marekani.
Mbali na Virusi vya Ukimwi (VVU), Yambesi alisema kwa kupitia kampeni hiyo watumishi na wananchi wengine watapata fursa ya kupima magonjwa sugu yasio ya kuambuzwa kama kisukari, shinikizo la damu, moyo, saratani, pumu na kupooza.
Alisema magonjwa hayo ambayo zamani yalikuwa yakihesabika kama magonjwa yanayowaathiri zaidi watu wenye uwezo mkubwa kiuchumi hivisasa yanaoonekana ni ya kawaida kwa watu wa kawaida.
Yambesi alisema kutopima afya kuna athari nyingi hasa kupungua kwa nguvu kazi, kuongezeka kwa gharama za matibabu na kupungua kwa tija inayoathiri ukuaji wa pato la taifa.
“Ili kuepuka matatizo hayo kuna kila sababu ya kuhamasiha watumishi wa umma kujali afya zao na kupima ili wachukue hatua kama wahenga walivyosema kinga ni bora kuliko tiba,” alisema.
Alisema katika kutekeleza ya wahenga ni muhimu kupima afya mara kwa mara kunasaidia kuepuka maambukizi mapya na wale wenye VVU kupunguza athari ya kuambukizi wengine,” alisema.
Alisema kwa takwimu za mwaka 2013, Tanzania ina  watumishi wa umma zaidi ya 500,000 ambao ni sehemu muhimu ya nguvu kazi ya taifa hivyo wanaohitaji kuwa na afya bora ili watekeleze wajibu wajibu wao.
“Tumekwisha weka misingi mizuri ya kulinda afya zetu kwa kuandaa waraka kuhusu Ukimwi na magonjwa sugu yasio ya kuambukizaa. Ni muhimu kwa taasisi za serikali kutekeleza maelekezo yote ili watumishi wa umma wawe ni wale wenye afya bora,” alisema.
Alisema watumishi wanapaswa kuwa wazi baada ya kugundulika na maambukizi ya VVU ili waweze kupata huduma muhimu ikiwemo ya matumizi ya dawa za kupunguza makali ya VVU (ARVs).
Watumishi wawili wa idara ya afya ya halmashauri ya wilaya ya Njombe wenye maambukizi ya VVU, Anjela Kayombo na Hilda Kapanda walisema pamoja na serikali kusisitiza mara kwa mara kuwasaidia watu wenye matatizo hayo, ahadi hiyo imeendelea kuwa hewa.
“Tunajua serikali inayo sera inayolenga kuwasaidia wenye VVU kwa dawa, lishe na vitu vingine, lakini sisi hatujawahi pata chochote,” alisema Kayombo.
Kampeni hiyo inafanywa kwa pamoja na serikali na Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambalo katika uzinduzi huo liliwakilishwa na Getrude Sima ambaye ni Mratibu wa Ukimwi mahali pa kazi wa shirika hilo. (BONGOLEAKS)

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...