Mlinzi wa kampuni hiyo (wa pili kutoka kulia) ambaye hakutaka kutaja jina lake akiongea na waandishi hivi karibuni ambapo alisema kuwa kampuni hiyo ina jumla ya walinzi watatu, lakini wana miezi miwili na siku 20 bila malipo.
Mpishi Mkuu wa Kampuni ya ujenzi ya Canopies International, Agape Mgongola akiendelea na kazi yakuwapikia wafanyakazi wa kampuni hiyo bila malipo kwa miezi minne sasa.
Na MARTHIAS KANALI,
Iringa
Wakazi wa Kitongoji cha
Msosa mkoani Iringa wameilalamikia kampuni ya Canopies International (T) Ltd kutoka
Mwananyamala jijini Dar es Salaam ambayo inajishugulisha na ujenzi wa barabara
kutoka njia panda ya Kalenga kuelekea Tosamaganga kutokana na kushindwa
kuwalipa fedha zao takribani miezi minne sasa.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti na THE SCOOP kijijini hapo wafanyakazi hao wamesema kuwa familia zao
zimekuwa hazina msingi mzuri wa kimaisha kutokana na malimbikizo ya mshahara
ambayo yawezekana wakalipwa ama wasilipwe kabisa, kwani mradi huo upo katika
hatua za mwisho za ujenzi wa barabara hiyo.
Kwa upande wake mpishi
mkuu Agape Mgongola ambaye ana miaka miwili tangu ameanza kufanya kazi na
Kampuni hiyo tangu ilipoanza ujenzi wa barabara inayokwenda Kalenga hajawahi
kupata usumbufu kama huu ambao anaupata kwa sasa. Agape alisema kuwa ni miezi
miwili na wiki moja hajapatiwa malipo ya aina yoyote jambo ambalo ni la kustaabisha
na kuathiri familia yake kiuchumi.
Aliongeza kuwa katika
mkataba wake alipaswa kulipwa shilingi 35,000 kwa wiki, lakini hadi kufikia
hivi sasa anadai jumla ya shilingi 315,000 kitendo ambacho kimekuwa tofauti na
makubaliano ya malipo kabla ya kuanza kazi.
Akizungumzia adha
wanayoipata kutokana na kutolipwa, mlinzi wa kampuni hiyo ambaye hakutaka
kutaja jina lake alisema kuwa kampuni hiyo ina jumla ya walinzi watatu, lakini
wana miezi miwili na siku 20 bila malipo, hivyo kila mmoja anadai laki nne.
"Sisi walinzi wa kampuni makubaliano yetu yalikuwa ni kwa mwezi, lakini
hii ni miezi miwili na siku 20 sasa hakuna malipo hivi unadhani tunajikomboaje
katika wimbi la umasikini kwa unyanyasaji na unyama tunaofanyiwa" alisema
mlinzi huyo.
Mlinzi huyo alisema kuwa
mwajiri wao amekuwa na dharau kwa watumishi hao, lakini hawana namna ya
kujikwamua katika unyanyasaji, hivyo amaiomba serikali kuingilia kati na
kutataua adha hiyo.
Wafanyakazi wa kampuni
wanatoka sehemu tofauti tofauti hapa Tanzania ambapo wengine ni kutoka Dar es Salaam,
Songea, Makambako na wengine wanatoka Iringa mjini. Wafanyakazi hao walisema
kuwa unyanyasaji wanaofanyiwa na kampuni hiyo kuanzia kwenye malipo hadi
wanapolala ni utumwa, kwani chumba kimoja wanalala watu zaidi ya 10.
THE SCOOP ilimtafuta
Msimamizi wa malipo Ismail Joseph, ambapo majibu aliyatoa hayakuwa ya
kuridhisha kwani alisema kuwa baadhi ya wafanyakazi hawatambui na wala hawezi
kuwalipa.
Hata hivyo leo asubuhi
nilipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kama kiongozi wa Mradi huo wa
barabara, ambaye alikiri kutowalipa wafanyakazi hao kama ambavyo wanalalamika.
Maungumzo kwa njia ya
simu kati ya mwandishi na kiongozi huyo yalikuwa hivi; Mwandishi: Habari yako?
Kiongozi: Nzuri natumai naongea na Mwandishi uliyefika jana ukafanya mahojiano
na wafanyakazi wangu. Mwandishi: Ni kweli haujakosea, nikusaidie nini?
Kiongozi: Taarifa uliyoipata jana kuhusu malipo ya wale watu ni kweli lakini
hatujawalipa na hatutegemei kuwalipa hadi pale TANROADS. Kwa upande wake Meneja
wa TANROADS Mkoa wa Iringa, Paulo Lyakurwa alisema kuwa kutolipwa ama kulipwa
wafanyakazi hao sio jukumu la TANROADS, bali ni jukumu la kampuni hiyo.
"Sisi tuliingia mkataba na Kampuni ya Canopies kwa hiyo, kampuni hiyo
inapofanya kazi na vibarua ama wafanyakazi hawatuhusu sisi, tunapaswa
kuhakikisha serikali imemlipa mkandarasi malipo yake kwa wakati japo kuna
wakati malipo yao huchelewa, lakini sio sababu ya yeye kushindwa kuwalipa"
alisema Lyakurwa.
Hata hivyo alisema kuwa
atahakikisha anasimamia swala la malipo ili wafanyakazi hao waweze kulipwa kwa
wakati.
No comments:
Post a Comment