Meneja mauzo na usambazaji wa Darbrew Fred Kazindogo (kulia)
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Bia za asili ya
Darbrew (TBL) kupitia bia yake ya asili ya Chibuku super imetangaza kudhamini
mashindano ya mbio ndefu za Uhuru ‘Uhuru Marathon’ kwa kiasi cha Sh. milioni 6.
Akitangaza udhamini huo jana
jijini Dar es Salaam, Meneja mauzo na usambazaji wa Darbrew Fred Kazindogo, alisema,
wameona ni vyema kudhamini mbio hizo kwa sababu zina lengo la kuimarisha umoja,
amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Alisema huu ni mwaka wa
pili kudhamini mbio hizo ambapo mwaka jana kampuni hiyo ilitoa kiasi cha
milioni 5 na zilifanyika kwa mafanikio.
Alisema kuwa baada ya
kuona malengo yametimia , Darbrew iliamua kuendelea kudhamini mbio hizo
zinazoshirikisha wanariadha kutoka sehemu mbalimbali ndani ya nje ya nchi.
“Baada ya mwaka jana mbio
hizi kufanyika kwa mafanikio makubwa, mwaka huu Kinywaji chibuku super
kimeongeza udhamini wake kwa asilimia 15% ambazo ni ongezeko la milioni 1,’’
alisema kazindogo.
Ukweli ni kwamba taifa
lolote duniani linapigania kuwa na uchumi imara na pasipokuwa na amani hakuna
uchumi utakaoweza kukua, hivyo Darbrew kama kampuni inayotengeza bidhaa za hapa
nyumbani imeona ni muhimu kuungana na Watanzania wenzetu wote kuhakikisha kuwa
mbio hizi zinafanyika katika hali ya mafanikio makubwa na kuwa za kufana zaidi.
Aliongeza kwa kuyataka makampuni
mengine ya ndani na nje ya nchi kujitokeza na pia kuendelea kutoa chochote
walichonacho ili kufanikisha mbio hizi zenye kubeba dhima ya Taifa letu lakini
pia wajitokeze kwa wingi kushiriki mbio hizi.
Naye mratibu wa Uhuru
Marathon, Innocent Melleck, aliwaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki
mbio hizo ambazo zina nia kubwa ya kutukumbukusha wajibu wetu wa kutunza na
kulinda amani, umoja na mshikamano miongoni mwetu.
Alisema zawadi kwa mshindi
wa kwanza inatarajiwa kuwa Sh. 2,500,000 kwa wakimbiaji wa kilomita 21 hii ni
kwa upande wa wanawake na wanaume.
Mshindi wa pili kwa mbio
hizo iwe kwa upande wa wanawake au wanaume kwa kilomita 21 au ataondoka na Sh
1.500,000 wa tatu Sh 1,000,000 wanne Sh 500,000 watano apata Sh 250,000 na wa
sita hadi kumi sh 100,000 kila mmoja.
Pia mwaka huu kutakuwa na
zawadi za ngao za heshima kwa shule za msingi na sekondari zitakazoshiriki mbio
za hizo ili kutambua ushiriki wao na tayari shule 25 zimethibitisha kushiriki mbio
kwa mwaka huu.
Mbio hizi zinatarajiwa
kufanyika jijini Dar es Salaam hapo Desemba 7, mwaka huu ambapo zitaanzia na
kumalizikia katika Viwanja vya Leaders club.
Mbio hizi zipo chini ya
ulezi wa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania na kwa mara nyingine tena
tunatarajia Mh Rais Jakaya Kikwete kushiriki mbio hizi,
Mbio hizo zimegawanywa
katika makundi makuu matatu ambayo ni kilomita 3 kwa ajili ya viongozi,
kilomita 5 kwa watu wote na kilomita 21 ambazo ni maalum kwa wakimbiaji nguli.
Wadhamini wengine wa mbio
hizo ni pamoja na Michuzi Media Group, Jambo Leo, Mwananchi Communication
Limited, CXS Africa, Kitwe General Traders, Faza Kidevu Blog, Habari Mseto Blog,
Blog ya Wananchi,TBC 1,TBC Taifa,Redio Uhuru,Clouds fm,Tindwa medical service.
No comments:
Post a Comment