Nyalandu katika mkutano wake na wananchi wa kijiji cha Igowole, Mufindi Kusini, mkoani Iringa |
Alisistiza mengi |
WAZIRI
wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amesema haiwezekani kila mwananchi wa
wilaya ya Mufindi mkoani Iringa anayeomba kuvuna miti katika msitu wa Taifa wa
Saohill ulioko wilayani humo akapata kibali.
“Nitakuwa
muongo nikitoa ahadi hiyo; lakini niwaahidi tu kwamba tutazidi kuboresha kanuni
zinazotumika kutoa vibali kwa waombaji ili rasilimali hii inufaishe watu wengi
zaidi,” alisema.
Aliyasema
hayo juzi katika ziara yake aliyoifanya katika kijiji cha Igowole wilayani humo
akiitikia wito wa mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini, Mendrad Kigola aliyemuomba
waziri huyo kukutana na wananchi wa jimbo hilo ambao ni sehemu ya wadau wakubwa
wa msitu huo.
Kwa
kupitia risala yao iliyosomwa na Precious Nyalusi, wajasirimali wa jimbo hilo
walimwambia waziri huyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa
kijiji hicho kwamba walitegemea msitu huo ungewanufaisha zaidi watu wa Mufindi
tofauti na ilivyo sasa.
“Tulitegemea
tungekuwa wanufaika wa kwanza wa malighafi hii kwa kuwa umependwa katika meneo
yaliyoachwa kwa nia njema na wazazi wetu, cha kushangaza unanufaisha zaidi
matajiri, wakubwa na kampuni hewa” alisema.
Awali
Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini alimueleza waziri huyo kwamba msitu huo ni
sawa na mali ya wana Mufindi kwa kuwa wao ndio waliopanda na kuulinda hadi
kufikia hatua ya kuvuna hivyo kuna kila sababu
asilimia 50 ya kila mgao unaotengwa kwa ajili ya uvunaji kila mwaka
ikatolewa kwao.
“Mwaka
jana asilimia 52 ya mago ulitolewa kwa wazawa huku asilimia 48 zikitolewa kwa
wageni; Mwaka huu Mufindi Kusini tulichopata hakizidi asilimia tano,” alisema.
Kigola
alisema; “sina matatizo na jinsi Mamlaka ya Misitu Tanzania ilivyotoa mgao kwa
vijiji na baadhi ya wananchi, shida yangu iko kwenye mgao wa vikundi hasa vya
wilaya ya Mufindi,” alisema.
Alisema
wakati vikundi 12 vya jimbo la Mufindi Kusini ndivyo vilivyopata mgao, 36
vilivyobaki vimetoka katika jimbo la Mufindi Kaskazini linaloongozwa na Naibu
Waziri na Utalii, Mahamudu Mgimwa.
Katika
majibu yake Nyalandu aliwapongeza wananchi wa wilaya hiyo kwanza kwa kutoa
maeneo yao yaliyopandwa masitu huo na pili kwa kuulinda msitu wenyewe.
Alisema
ili kuwafanya watanzania wengi wanufaike na rasilimali hiyo, serikali iliamua
kusitisha maamuzi yake ya kuuza miti katika misitu yake kwa njia ya mnada na
kuendelea na mfumo wa sasa wa vibali.
“Zilikuwa
ni busara za Rais jaka Kikwete, vinginevyo rasilimali hii ingekuwa
inawanufaisha wenye uwezo mkubwa wa kifedha kwasababu katika mnada anayetoa zaidi
ndiye anayeuziwa,” alisema.
Alisema
kwa kupitia mfumo wa vibali, yapo baadhi ya maeneo yanahitajika kuboreshwa ili kuwafanya watanzania wengi zaidi na wale
wanaosaidia kulinda misitu wanufaike.
“Kama
nilivyosema haitawezekana kila mwana Mufindi au wadau wote wanaoomba mgao wa
kuvuna watapata kibali lakini tutakachofanya ni kuyakumbuka maeneo yote ambayo
wananchi wanatusaidia kulinda misitu,” alisema.
Aliiagiza
Mamlaka ya Misitu Tanzania (TFS) kuendelea kuboresha kanuni zinazotumika kutoa
vibali kwa waombaji wakizangatia maslai mapana ya Taifa.
“TFS
waangalie sehemu zote zinazotatanisha katika
mfumo wa mgao tunaotumia sasa, yaliyojitokeza yasipuuzwe, pitieni upya taratibu
za utoaji wa vibali ili makundi yote yanufaike; wananchi, viwanda vidogo, vya
kati na vikubwa, vikundi vijiji, taasisi na wadau wote kwa kadri itakavyowezekana wakumbukwe lakini
kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria,” alisema. CHANZO: BONGOLEAKS
No comments:
Post a Comment