Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga aliyevaa vazi la Kiislamu alipokuwa akitoa taarifa ya ujuio wa Kinana mkoani Iringa |
Hassan Mtenga, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa |
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM),
Abdulaman Kinana atawasili mkoani Iringa Oktoba 6 katika ziara yake ya siku
sita itakayompitisha katika majimbo yote ya mkoa wa Iringa.
Atakapowasili atalakiwa na viongozi
mbalimbali wa chama na serikali wa mkoa wa Iringa wakiwemo wabunge.
Akizungumza na wanahabari hii leo, Katibu
wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga alisema ziara ya Kinana itaanzia katika jimbo
la Isimani kabla ya kwenda jimbo la Kalenga siku inayofuata.
Alisema baada ya kutoka Kalenga,
atakwenda jimbo la Kilolo kisha kuelekea wilayani Mufindi atakakotembelea
majimbo yote mawili, Mufindi Kusini na Mufindi Kaskazini.
Ziara ya Kinana itahitimishwa Oktoba 11,
katika jimbo la Iringa Mjini linaloongozwa na Mchungaji Peter Msigwa wa
Chadema.
Mtenga alisema ziara ya Kinana inalenga
kuimarisha chama hicho, kusikiliza kero za wananchi na kutoa maelekezo muhimu
yatakayosaidia kukijenga chama hicho.
Rai ya Chadema
Katika mkutano wake uliofanyika katika
uwanja wa Kata ya Kihesa juzi, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji
Msigwa alilitaka jeshi la Polisi kupiga marufuku aina yoyote ya maandamano
itakayofanywa na wafuasi wa CCM wakati wa ziara yake hiyo.
Msigwa na viongozi mbalimbali wa chama
chake walitoa rai hiyo baada ya jeshi la Polisi kuzuia msafara wa pikipiki,
magari na maandamano yao yaliyokuwa yameandaliwa na wafuasi wa chama hicho
wakati wakimpokea Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana la Chadema
(Bavicha), Patrick Ole Sosopi.
“Tumetii
maelekezo ya Polisi, vijana wetu wa bodaboda wamezuiwa kutupokea; ili haki
itendekea tunataka Kinana na timu yake watakapoingia mjini Iringa, misafara yao
isiwe na maandamano ya watu, pikipiki wala magari,” alisema Mchungaji Msigwa
katika mkutano wao mkubwa uliofanyika katika kata ya Kihesa mjini Iringa.
Taarifa ya CCM
Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa alisema
katika ziara hiyo chama hicho hakina mpango wa kufanya maandamano kwa kuwa huo
sio utaratibu wake.
“Sisi sio watu wa maandamano, nanyi
mnajua hivyo; Chadema ndio chama kinachoepnda kuandamana kwa kila jambo hata
lisilo na maana kwa watanzania. Kinana anakuja Iringa ikiwa ni muendelezo wa
ziara anazoendelea kufanya katika mikoa yote nchini, anakuja kujenga chama,
atawakuta watu katika maeneo yao kwahiyo hatuna mpango wa kuwakusanya kwa
maandamano,” alisema.
Aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi
katika ziara hiyo inayotarajiwa kukiongezea nguvu zaidi chama hicho. CHANZO: BONGOLEAKS
No comments:
Post a Comment