Timu ya Simba ambayo imeshuka dimbani mara tano kwenye ligi kuu Tanzania Bara msimu huu na kutoka sare michezo yote huku ikiwa imefunga goli tano na kufungwa idadi hiyo, inashika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Kocha wa timu ya SIMBA Mzambia Patrick Phiri, aliutumia mchezo wa jana kama maandalizi,huku akiwatumia wachezaji wengi wa kikosi cha vijana cha timu hiyo.
Timu ya SIMBA ilianza mchezo taratibu na kuifanya timu ya Lipuli kutawala kipindi cha kwanza ambapo hadi mapumziko timu hizo zilikuwa hazijafungana.
Kipindi cha pili Simba walionekana kubadilila na kuanza kulishambulia kwa kasi lango la lipuli hatimaye ilifanikiwa kupata goli ambalo lilifungwa na mshambuliaji hatari Elias Maguli ambae alitumia makosa ya mabeki wa Lipuli waliochelea kuondoa mpira kwenye eneo lao la hatari.
Kuingia kwa bao hilo kuliufanya mchezo kuchangamka huku timu zote zikishambuliana kwa zamu lakini mpaka mwisho wa mchezo Simba waliibuka kifua mbele.
Baada ya kumalizika kwa mechi hiyo kocha mkuu wa Wekundu wa msimbazi akiongea na Waandishi wa habari alitamba kuibuka na ushindi kwenye mechi dhidi ya Mtibwa akisema vijana wake wameahidi kushinda mchezo huo.
Kuhusu kupewa mechi mbili na uongozi wa timu hiyo kocha uyo alisema yeye kwa sasa anaangalia namna ya kushinda michezo yote iliyobaki.
Pia kocha huyo aliimwagia sifa timu ya Lipuli na kusema ni timu nzuri na wametoa upinzani mkali kwa vijana wake.
Kwa upande wake Rais wa timu ya Lipuli Jesca Msavatavangu alisema vijana wake walicheza vizuri huku wakionekana kucheza kwa hali na mali, hivyo kutoa burudani kwa wakazi wa Mjini Iringa na viunga vyake.
Msavatavangu alisema hiyo ilikuwa ni nafasi kwa vijana wake kuonekana kwa wakazi wa Iringa ikiwa ni pamoja na kuonyesha kiwango cha soka, kwa kucheza na timu kubwa zinazoshiriki ligi kuu.
No comments:
Post a Comment