Waziri Pinda |
*Azindua jengo la kisasa la Mama Ngojea wilayani Urambo
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amewataka viongozi wa mkoa wa Tabora wajipange
vizuri na kuhakikisha kuwa wanajenga vituo vya afya katika kila kata za
wilaya ya Urambo kwa sababu bado iko nyuma.
“Hatua
hii itasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali ya
wilaya ya Urambo kwa sababu yenyewe imekuwa ndiyo kimbilio la kila
mgonjwa kwa sasa,” amesema.
Ametoa
agizo hilo jana wakati akizungumza na
mamia ya wakazi wa mji wa Urambo mara baada ya kuzindua jengo la Mama
Ngojea linaloitwa Mayu Lindila lililopo kwenye hospitali ya wilaya hiyo.
“Wilaya
yenu ina kata 16, ina vijiji 57 na zahanati 22 lakini ina kituo kimoja
tu cha afya. Na hii maana yake ni kwamba kuna vijiji havina zahanati
kabisa. Huu ni mtihani mkubwa na ndiyo maana kila mtu akiumwa
anakimbilia kwenye hospitali ya wilaya,” alisema Waziri Mkuu.
“Kisera
kila kata ni lazima iwe na kituo cha afya, kwa hiyo viongozi wa mkoa na
wilaya ni lazima mjipange kuona ni kwa namna gani mtaitekeleza sera
hii, na pia jengeni zahanati kwenye vijiji ambavyo havina zahanati,”
alisisitiza.
Akizungumzia
kuhusu umuhimu wa huduma ya Mama Ngojea, Waziri Mkuu alisema unasaidia
kuokoa maisha ya mama mjamzito anayetoka kata ya mbali ambaye
anakabiliwa na tishio lakini siku zake za kujifungua zinakuwa
hazijafika.
Alisema
kutokuwepo kwa majengo ya Mama Ngojea katika maeneo mengi ni changamoto
kubwa na hatari kwa akinamama wengi hasa waishio mbali na huduma za
tiba. “Hivi kama kata moja iko mbali na makao makuu ya wilaya, na mama
mjamzito mwenye tatizo hawezi kufika hospitali unadhani ataenda wapi? Si
ataenda kwa wakunga wa jadi au waganga wa kienyeji tu?”
Aliwasihi
akinamama wa wilaya hiyo wajitahidi kutumia huduma za hospitali kwa
sababu kwa wakunga wa jadi na waganga wa kienyeji hakuna wataalamu kama
waliopo hospitalini.
Alimtaka
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Bibi Fatma Mwassa afanye utaratibu ili kila
wilaya pawe na Mama Ngojea. “Hata kama hakuna hospitali ya wilaya lakini
pana kituo cha afya, ni vema pawe na jengo la Mama Ngojea ili kuokoa
maisha ya akinamama.
Akitoa
taarifa ya ujenzi wa jengo hilo, Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Kheri
Kagya alisema jengo hilo lenye uwezo wa kulaza wagonjwa 24 kwa wakati
mmoja, lilianza kujengwa Agosti 25, 2012 na lilikamilika Novemba 10,
2013 kwa gharama ya sh. milioni 198/-. Lina jiko, sehemu ya kulia,
mabafu, vyoo, eneo la kufulia na kupumzikia.
Lengo
la kujenga kituo hiki ni kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo
228 kwa kila vizazi hai 100,000 na kufikia vifo 90 kwa kila vizazi hai
100,000 au chini ya hapo ifikapo mwaka 2015. “Mwaka 2012 tulikuwa na
vifo 253 kwa kila vizazi hai 100,000 na mwaka jana tulikuwa na vifo 228
kwa kila vizazi hai 100,000. Nia yetu ni kupunguza kabisa vifo vya
akinamama kabla na wakati wa kujifungua,” alisema.
Aliwashukuru
Mbunge wa jimbo la Urambo ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki, Bw.
Samuel Sitta na mkewe Mama Margareth Sitta (ambaye pia ni Mbunge wa
Viti Maalum wa Mkoa huo) kwa kubuni wazo hilo na kutafuta fedha za
kujenga Mama Ngojea kwenye hospitali ya wilaya hiyo.
Wakati huohuo, Bwana na Bibi Sitta wamechangia mablanketi 300 na vyandarua 100 kwa ajili ya Mama Ngojea pamoja na hospitali ya wilaya hiyo.
No comments:
Post a Comment