Monday, 27 October 2014

WANACHADEMA WAANZA KUJITOKEZA KUGOMBEA UONGOZI WA SERIKALI ZA MITAA

Frank Nyalusi Mwenyekiti wa ccm Wilaya ya Iringa akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye mkutano
Wananchi wakifuatilia mkutano kwa umakini.
Na Mathias Canal, Iringa

Diwani wa Kata ya Mivinjeni Frank Nyalusi (CHADEMA) amehamasisha wakazi wa kijiji cha Ifunda,Kata ya Ifunda, Wilaya ya Iringa, Mkoani Iringa, kujiandikisha katika daftari la mkazi ili waweze kupiga kura pasipo matatizo yoyote.


Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wakazi wa kijiji hicho waliojitokeza kwenye mkutano huo ambao lengo la mkutano huo ilikuwa ni kutoa elimu kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba 14 mwaka huu.

Nyalusi amewataka wapenzi wa CHADEMA kutoogopa kuchukua fomu kwani matatizo ya Ifunda yataweza kutatuliwa na viongozi makini ambao wanapatikana kwenye chama hicho.
Nyalusi amesema maisha ya mtanzania yanaendelea kudidimia huku akitoa mfano wa mahindi ambayo yanauzwa shilingi 25,000 kijini hapo huku miaka miwili iliyopita yalikuwa yanauzwa shilingi 70,000 kwa gunia.

"Hatuichukii CCM kwa sababu ya jembe na nyundo, bali tunaichukia CCM kwa sababu ya usanii wao," alisema Nyalusi.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wameulalamikia uongozi wa kijiji kwa kutowasomea mapato na matumizi jambo ambalo linawafanya wananchi kutojua fedha zilizopo na matumizi yake kwa ujumla.

Aidha Nyalusi amewakumbusha wananchi kwamba wanapaswa kusomewa mapato na matumizi kwani hilo ni jambo la wazi na linahitaji kufanyika kila baada ya miezi mitatu.

Nyalusi alitumia nafasi hiyo kumpongeza Beatrice Miyamba, Mwenyekiti wa kitongoji cha Kibaoni B-Ifunda (CHADEMA) kwa kuamua kujitokeza kugombea nafasi ya uenyekiti wa kijiji cha Ifunda.

Akizungumzia maamuzi ya kugombea nafasi ya mwenyekiti wa kijiji Beatrice alisema anaamini atashinda na kushirikiana na wajumbe pamoja na mtendaji wa kijiji ambaye atakuwa chini ya mwenyekiti wa kijiji.

"Nimeumia sana kutokana na wananchi kuteseka kwa sababu ya daraja linalounganisha kijiji cha Iganga na Ifunda kwenda kijiji Utengilinyi ambapo fedha zilizopatikana ilikuwa ni shilingi milioni moja iliyotengwa na serikali ambayo inasemekana kuwa zimetumiwa na wachache ambao ni viongozi wa serikali." alisema Beatrice.

Beatrice alisema kuwa pamoja na kwamba familia anayotoka inaongozwa na CCM lakini ameamua kufanya mageuzi kwa kuachana na chama hicho kwa ajili ya kupambana na ufisadi ili kuwakomboa watu wa Ifunda na taifa kwa ujumla.

"Mimi nategemea ushindi lakini kama ikitokea nikashindwa sitegemei kulalamika wala kubadilika bali nitaonyesha ushirikiano na yule atakayeshinda," alisema Beatrice


No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...