Katibu CCM Wilaya ya Mufindi Miraji Mtaturu
Katibu CCM Wilaya ya Mufindi Miraji Mtaturu kulia, akiwa na Mstahiki Meya Amani Mwamwindi (kushoto) na katikati ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa Mjini Abed Kiponza.
Na Mathias Canal
Chama cha Mapinduzi (CCM) Iringa Mjini kimenufaika kisiasa baada ya juzi kupata wanachama wapya 110.
Wanachama hao vijana, baadhi yao wakitokea katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) cha mjini Iringa, walikabidhiwa kadi zao na kuapa kuwa waaminifu
katika chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa stendi ya mabasi yaendayo vijijini ya Mlandege.
CCM iliamua kuutumia uwanja huo kikilenga kupima mwitikio wa wanachama na wapenzi wake ikiwa ni takribani wiki moja tu tangu viongozi wa kitaifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwemo Dk Wilbroad Slaa kufanya mkutano wao katika uwanja huo huo.(P.T)
Idadi ya watu waliojitokeza katika mkutano huo ilielezwa na Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Iringa, Abeid Kiponza kwamba ni ya kuridhisha pamoja na kwamba ulihutubiwa na viongozi wa mkoa na wilaya tofauti na ule wa Chadema uliohutubiwa na viongozi wa kitaifa.
Baada ya wanachama hao wapya kuapishwa, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Mufindi, Miraji Mtaturu alikabidi Sh 500,000 kwa wanachama hao wanaounda tawi la VETA.
"Huu ni mchango wa CCM kwa tawi lenu jipya, kama mlivyoainisha kwenye risala yenu, ni matarajio yetu kwamba mtatumia fedha hizo kuanzisha shughuli itakayowahamasisha muwe wajasiriamali," alisema.
Pamoja na tawi hilo kuchangiwa Sh 500,000; tawi la CCM la Mlandege linaloundwa na madereva taxi nalo lilikabidhi na katibu huyo Sh500,000.
"Haya ndio mambo ya CCM, tunaisimamia serikali kutekeleza Ilani na wakati huo huo tunachangia shughuli za maendeleo za wadau wetu wote na wakati mwingine bila kujali itikadi za siasa, tumefanya hivyo sehemu nyingi na tutaendelea kufanya hivyo" alisema Mtaturu.
Mtaturu alisema siasa ni maisha ya watu na kwa kupitia Ilani ya CCM serikali imeendelea kuzipatia suluhu kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Katika mkutano huo Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi alielezea kazi mbalimbali zilizotekelezwa na halmashauri yake kupitia Ilani ya CCM.
"Tumefanya mengi katika sekta ya afya, elimu, barabara, umeme, maji, biashara, ujenzi na nyingine nyingi. Nyie ni mashahidi," alisema.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu alitoa ufafanuzi wa vifungu mbalimbali likiwemo suala la muundo wa serikali na sifa za kupata wabunge na mawaziri kupitia Katiba Inayopendekezwa.
No comments:
Post a Comment