Waziri Mkuu Mizengo Pinda
Na Elias Msuya, Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali imetiwa doa na kashfa ya IPTL ambapo zaidi ya Sh bilioni 200 zinadaiwa kuchotwa kwenye akaunti maalumu ya ‘Tegeta Escrow’, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Pinda ambaye yupo jijini London, Uingereza kuhudhuria mkutano wa viongozi wa Afrika na wawekezaji wa Ulaya, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza kwenye kipindi cha Dira ya Dunia kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) .
Alisema madai hayo yametia doa Serikali kwa kuwa tayari wahisani wameshakata misaada waliyoahidi kuitoa kwa ajili ya bajeti ya 2014/15.
Pinda alisema Serikali inafanya uchunguzi kupitia Takukuru na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Madai haya yanatia doa kwa maana yamesemwa na vilevile wanaweza (wahisani) kukata kutoa misaada, ni mbaya sana. Kwa bahati mbaya sana wakuu wamechukua hatua (kukata misaada) kabla hata matokeo yenyewe hayajajulikana,” alisema.
Pinda alipotakiwa kusema kama pamoja na kashfa hiyo wawekezaji ambao atakutana nao London watamwelewa, alisema: “Itategemea uchunguzi unaoendelea, jambo hili limejitokeza kama tuhuma na tulichofanya kama Serikali tumekiagiza chombo kinachohusika na rushwa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali mara moja kufanya uchunguzi wa tuhuma hizo.”
Alisema Tanzania ni kati ya nchi zinazojitahidi katika mapambano dhidi ya rushwa.
Mbali na Tanzania, nchi nyingine zilizohudhuria mkutano huo ni Nigeria, Ghana, Uganda, Rwanda na Togo.
Hivi karibuni nchi wahisani zilitangaza kuikatia misaada Serikali ya zaidi ya Sh trilioni 1 kutokana kashfa ya fedha za mradi wa kuzalisha umeme wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL).
Hivi karibuni, Balozi wa Finland ambaye pia ni mwenyekiti wa wadau wa maendeleo nchini, Sinikka Antila, alithibitisha nchi za Ulaya hazijatoa pesa yoyote kati ya dola za Marekani milioni 558 milioni sawa na Sh bilioni 937 zilizoahidiwa katika bajeti ya mwaka 2014/15.
Antila alisema kuwa watazitoa fedha hizo endapo wataridhishwa na matokeo ya uchunguzi wa malipo ya fedha za IPTL kwa Pan African Powers Solution Tanzania Ltd (PAP).
ATANGAZA KUGOMBEA URAIS KIMYA KIMYA
Akizungumzia suala la kugombea urais, Pinda alikiri kuwa mmoja kati ya makada wa CCM waliojitokeza kugombea.
“Kwahiyo ndiyo umetangaza kugombea urais?” aliuliza mtangazaji wa kipindi hicho, Salim Kikeke na ndipo Waziri Mkuu Pinda alijibu: “Rasmi bado, lakini ile kimya kimya ile imekuwa ikiendelea.”
Kisha akaulizwa tena: “Kwahiyo umetangaza kimya kimya?”… “Ndiyo,” alijibu Pinda.
Awali Kikeke alimuuliza kuhusu mtu anayefaa kubeba mikoba ya Rais Jakaya Kikwete baada ya kustaafu.
Huku Pinda akionekana kuzunguka swali hilo, alieleza utaratibu wa kumpata rais tangu kwenye chama na Serikali hadi kweye Uchaguzi Mkuu.
“Mikoba yake inaweza kuvaliwa na yeyote ambaye ataonekana mwisho wa safari na utaratibu ndani ya chama na Serikali yenyewe kama nchi atakayekuwa amepatikana kuwa anafaa,” alisema Pinda na kuongeza:
“Waliojitokeza hadi sasa ni wengi na mimi nawaunga mkono,” Kisha alikatishwa na swali la Kikeke kama na yeye yumo…
“Umesikia kuwa nimo? … Basi kubali na yeye yumo. Lakini wote waliojitokeza pamoja na Waziri Mkuu…”
Jibu la Pinda lilikatishwa tena na Kikeke akisisitiza jibu la moja kwa moja kama kweli atagombea. Lakini Pinda aliendelea kukwepesha.
“Hawa wote waliojitokeza ni katika jitihada za kusema hebu Watanzania nitazameni je, mnaona nafaa au hapana, fanyeni hivyo kwa mwingine na mwingine na mwingine,” alisema Pinda na kuongeza:
“Mwisho wa yote, kura zitakazopatikana kwenye mkutano mkuu kama ni kwa chama kinachotawala na hatimaye, Watanzania watakaojitokeza kupiga kura Oktoba mwakani kutokana na wagombea watakaokuwa wamepatikana kwa vyama mbalimbali, huyo ndiyo atapata urais.”
Wagombea ambao wamejitokeza wazi ndani ya CCM ni mbunge wa Nzega, Khamis Kigwangallah na Naibu Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia, January Makamba.
Wanaozungumziwa lakini hawajangaza rasmi ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, Waziri Ofisi ya Rais, Stephen Wasira, Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
KATIBA
Kuhusu Katiba inayopendekezwa iliyokabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete na Dk. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Pinda alipinga hoja kwamba imeegemea upande wa CCM peke yake bali imezingatia Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Si kweli kwa sababu unajua Katiba ile kama ambavyo tumeieleza, sehemu kubwa ya maoni yametokana na ya Tume ya Warioba (Jaji Joseph) kama yalivyo. Michango yote iliyoingizwa pale ni asilimia 20 tukayaingiza kwenye Tume ya Mzee Warioba,” alisema Pinda na kuongeza:
“Kwahiyo kudai kwamba yaliyomo mle ni ya upande mmoja si kweli. Ndiyo maana nikasema jambo hili limekuwa likiwekwa kwa namna ambayo inawafanya watu wachanganyikiwe bila sababu ya msingi.”
Huku akisisitiza kuwa taratibu za kisheria zilifuatwa, Pinda alisema inawezekana kura ya maoni kuhusu Katiba mpya ikafanyika Machi na kisha Uchaguzi Mkuu ifikapo Oktoba mwakani.
“Nchi iko tayari kwa kura ya maoni na Uchaguzi Mkuu… inawezekana Oktoba,” alisema Pinda.
CREDIT: MTANZANIA
No comments:
Post a Comment