Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM),Abdulrahman Kinana akiulizwa swali na mmoja wanachama wa chama hicho mjini Iringa hivi karibuni. (PICHA NA FRIDAY SIMBAYA)
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), amekamilisha awamu
nyingine ya ziara zake mikoani. Katika awamu hii, alitumia siku 28
kutembelea mikoa ya Pwani, Tanga na Iringa.
Wapo ambao wanazibeza ziara hizi kwa sababu za
kisiasa, lakini kwa wanaozifuatilia kwa karibu, wameshagundua kuwa
zitakuwa na mchango mkubwa katika ushindi wa CCM katika uchaguzi ziku za
usoni.
Kuna mambo mengi ambayo Kinana na timu yake wanayafanya katika ziara hizo ambayo yanarudisha imani ya wananchi kwa CCM.
Siyo siri kuwa katika kipindi cha miaka michache
iliyopita, wananchi wengi walianza kupoteza imani na chama tawala kwa
sababu mbalimbali, kubwa ikiwa chama hicho kushindwa kutekeleza kile
inachokiahidi.
Hata Kinana anakiri katika hotuba zake kwenye ziara kuwa ni kweli CCM ilipoteza mwelekeo kidogo katika miaka ya hivi karibuni.
Akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM
Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, Kinana anasema ni kweli chama hicho
kiliingia mushkeli.
“Moja kati ya madhumuni ya ziara zangu mikoani ni
kukagua uhai wa chama na kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi…
hapa katikati CCM iliacha kufanya yale yanayostahili kufanywa na chama
tawala,” anasema.
Hata hivyo, Kinana haishii kukagua utekelezaji wa ilani tu.
Pale anapobaini makosa husema waziwazi na huwa hamwonei mtu yeyote aibu.
Anawakosoa kuanzia viongozi wa CCM wenyewe na
watendaji katika halmashauri za wilaya au hata serikali kuu pale
anapobaini wametenda makosa.
Ndiyo maana mara nyingi katika hotuba zake, ukimsikiliza Kinana wakati anahutubia, unaweza kudhani anayezungumza ni mpinzani.
Ile lugha ya kuwasema viongozi wa Serikali na CCM
ambayo kwa miaka mingi imezoeleka kutoka kwenye vinywa vya wanasiasa wa
upinzani, sasa inatolewa na Kinana, tena si kwa kificho, bali kwenye
mikutano ya hadhara. (CHANZO: MWANANCHI)
No comments:
Post a Comment