Sunday, 23 November 2014

Choo bora na Mikono safi kwa afya bora utu na usawa








Mkazi wa Kijiji cha Ifunda, Wilaya ya Iringa, mkoani Iringa Richard Ng’onda amesema vyoo bora katika kijiji chao itakuwa ni ndoto za mchana kutokana na ukosefu wa huduma ya maji safi na salama.


Amesema kuwa kutokana uhaba mkubwa wa huduma ya maji safi na salama wananchi wengi katika kijiji chao wanashindwa kutekeleza adhima ya serikali ya kila kaya kuwa na choo bora kwa sababu wanatumia maji ya visima vya jadi na ndoo moja ya maji huuzwa shilingi mia moja.

“Hatuwezi kujenga vyoo bora kwa kila kaya katika Kijiji cha Ifunda kutokana na uhaba mkubwa wa huduma maji safi na salama, tunalazimika kujenga vyoo kulinga na hali halisi ya maisha yetu. Ndugu mwandishi kuwa na vyoo bora kunahitaji kuwa na maji yakotosha tuaomba serikali angalau ituboreshee miundombinu ya maji kwa sababu bila maji tutaendelea kuwa na mazingira duni,” amesema Ng’onda mkazi wa kijiji cha Ifunda.


Kilele cha maadhimisho ya siku ya choo duniani, siku ya unawaji mikono na wiki ya usafi Tanzania kimefikia kikomo ambapo zaidi ya watu bilioni 4.5 tu ndio wanaomiliki na kutumia vyoo bora huku watu bilioni 2.5 duniani kote hasa maeneo ya vijijini hawana vyoo bora.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Dkt. Leticia Warioba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya usafi kimkoa uliofanyika katika Kijiji cha Ifunda amesema takwimu zinaonesha kuwa matumizi ya choo bora hupunguza magonjwa ya kuhara kwa asilimia 32 na kunawa mikono kwa sabuni hupunguza magonjwa hayo kwa asilimia 50.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeinisha kuwa watu wengi duniani wanapata au kumiliki huduma za simu za mikononi kuliko wanaopata huduma choo bora. Kati ya watu bilioni saba duniani kote watu bilioni sita wanamiliki au wanapata huduma ya simu na watu bilioni 4.5 tu ndio wanamiliki au kupata hudumaya choo bora.

Amesema kuwa lengo kuu la maadhimisho haya ni kuhamasisha jamii kuchukua hatua katika kukabiliana na changamoto za kukosa huduma za choo bora na unawaji mikono kwa sabuni na hatimaye kumaliza kabisa tatizo la kukosa huduma hizi muhimu na kuepuka magonjwa yanayoweza kuambukizwa kupitia kukosa huduma za vyoo naunawaji mikono usio wa kitaalam.

Amesema kuwa kunawa mikono kwa sabuni ni mojwapo ya njia rahisi na yenye gharama nafuu kuzuia maambukizi. Kauli mbiu ya maadhimisho haya mwaka huu inaendana na kauli mbiu ya siku ya choo duniani, ambayo ni “Usawa katika afya njema na utu kupitia huduma enedelevu za usafi wa mazingira.”

Tanzania imeandaa kauli mbiu yake ambayo inaendana na kauli mbiu ya kimataifa, “Choo bora na Mikono safi kwa afya bora utu na usawa”

Takwimu za utafiti wa afya ya uzazi na mtoto za mwaka 2010 nchini Tanzania zinaonesha kwamba ni mtu mmoja tu kati ya watano ambaye ananawa mikono kwa sabuni kabla ya kuandaa chakula; na mtu mmoja kati ya watanzania wawili hapati huduma maji safi na salama.

Aidha, kiwango cha matumizi ya vyoo bora ni asilimia 22 kwa mijini na asilimia 9 kwa vijiji na kwa mkoa wa iringa takwimu zinaonesha kuwa kaya zenye vyoo niasilimia 95.5 na idadi hii imejumuisha vyoo vya aina zote.

Hata hivyo, takwimu za awali za uhakiki wa usafi wa mazingira katika baadhi ya ya kata zinaonesha kuwa ni asilimia 26 tu ya kaya ndio wenye vyoo bora, asilimia 65 ya kaya wana vyoo visivyokidhi vigezo na asilimia 9 hawana vyoo kabisa.

Naye Ofisa wa Afya wa Mkoa wa Iringa, Khadija Haroun ameseam katika kuhakikisha nchi yetu inafikia lengo la Millenia na saba (7) ambalo ni kupunguza kwa nusu idadi ya watu amabo hawana huduma ya vyoo bora ifikapo mwaka 2015, Tanzania ilianzisha  rasmi kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira ambayo ilizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. Jakaya Kikwete tarehe 5 Juni, 2012.

Kampeni hii inalenga kuongeza ujenzi wa vyoo bora katika kaya 1,520,000 na shule 812 ifikapo mwaka 2015. Mkoa wa Iringa ulianza kutekeleza kampeni hii mwaka 2012 ambapo halmashauri mbili za wilaya ya iringa na Mufindi zilianza kutekeleza.

Ofisa wa afya mkoa ameongeza kuwa  katika mwaka 2013 Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na Halmashauri ya wilaya ya Kilolo zilianza utekelezaji na kufanya halmashauri zote za mkoa kuwa zinatekeleza kampeni hii.

Hadi kufikia Juni mwaka 2014 jumla ya kaya 7,651 ziliboresha vyoo vyake kupitia uhamasishaji shirikishi wa jamii na jumla ya shule 15 zimeanza kujenga vyoo bora kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo fedha maalum ya mfuko wa kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira.


Kimataifa Siku ya Kunawa mikono huadhimishwa kila tarehe 15 Oktoba na Siku ya Choo duniani huadhimishwa kila tarehe 19 Novemba. Tanzania kwa kuzingatia umuhimu wa uboreshaji wa huduma hizi, ilamua kutenga wiki inayoanzia tarehe 13 hadi 19 novemba kuwa ni wiki ya Usafi wa Mazingira yalioanza rasmi mwaka2013.

Katika maadhimisho haya Tanzania huadhimisha kwa pamoja siku ya choo duniani, siku ya kunawa mikono ulimwenguni na wiki ya usafi Tanzania.



Katika hotuba ya Katibu tawala wa mkoa wa Iringa, iliyosomwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt Robert Salim, ya kufunga maadhimisho hayo Kimkoa iliyofanyika Kijiji cha Ifunda, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa mwaka 2013, Umoja wa Mataifa ulipitisha tarehe 19 Novemba ya kila mwaka kuwa ni siku rasmi ya maadhimisho ya Siku y Choo Duniani, ambapo mwaka huo huo Tanzania ilipitisha rasmi tarehe 13-19 Novemba kuwa ni wiki ya usafi Tanzania pamoja na siku ya kunawa mikono Duniani sambamba na siku ya choo Dunia.


Takwimu zinaonyesha kuwa matumizi ya choo bora hupunguza magonjwa ya kuhara kwa asilimia 32 na kunawa nikono kwa sabuni hupunguza magonjwa hayo kwa asilimia 50, ambapo Takwimu za mwaka 2013 zinaonyesha kuwa watoto 1000 wanakufa kwa kila siku moja duniani kote kutokana na magonjwa ya kuhara.


Aidha baadhi ya taasisi zilipatiwa zawadi mbalimbali kutokana na uboreshaji wa huduma za maji, afya na mazingira ikiwa ni pamoja na shule ya msingi Nyololo, ambapo Manispaa ya Iringa ilipata zawadi ya kuweza kudhibiti uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya mkusanyiko, huku Kitongoji cha Mpwapwa kilichopo kijiji cha Kihanga kilipata zawadi ya kuwa kitongoji kisichotupa kinyesi ovyo.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...