I: UTANGULIZI
a) Masuala ya jumla
Mheshimiwa
Spika,
1.Leo
tunahitimisha shughuli za Mkutano wa Kumi na Sita na Kumi na Saba wa Bunge lako
Tukufu. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi
Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo.
Mheshimiwa
Spika,
2.Mkutano huu ulijumuisha kujadili kazi kubwa zifuatazo:
Kwanza:Mapendekezo ya Mpango
wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2015/2016;
Pili:Muswada wa Sheria ya Usimamizi
wa Kodi wa Mwaka 2014 [The Tax
Administration Bill, 2014];
Tatu:Muswada wa Sheria ya Kodi ya
Ongezeko la Thamani wa Mwaka 2014 [The
Value Added Tax Bill, 2014];
Nne:Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya
Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2014 [The Public Private Partnership (Amendment)
Bill, 2014]; na
Tano: Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya
Sheria mbalimbali wa Mwaka 2014, [The
Written Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2014].
Aidha, ni hivi mapema
leo Miswada 11 ya Sheria ya Serikali
kuhusu mambo mbalimbali ilisomwa kwa mara ya kwanza.
Mheshimiwa
Spika,
3.
Nitumie
nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kushiriki katika Kamati ya
Mipango hapa Bungeni kwa kujadili kwa kina mapendekezo yaliyowasilishwa na
Serikali kuhusu Mpango wa Maendeleo wa
Taifa wa mwaka 2015/2016. Maoni na Ushauri tuliopokea kutoka kwa
Waheshimiwa Wabunge tutauzingatia wakati wa maandalizi ya Bajeti ya mwaka
2015/2016. Vilevile, niwashukuru kwa kujadili na kupitisha Miswada ya Sheria
niliyoitaja hivi punde.
b)
Maswali
Mheshimiwa
Spika,
4.
Katika
Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa
ya kuuliza maswali ya kawaida na yale ya Papo Papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Jumla ya maswali 241 ya msingi na 662 ya nyongeza yameulizwa na
Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali.
Aidha, Maswali 18 ya msingi
na 13 ya nyongeza yaliulizwa na
kujibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
c) Kauli
za Mawaziri
Mheshimiwa
Spika,
5.
Waheshimiwa
Wabunge watakumbuka kuwa tarehe 17 Novemba, 2014 nilipata fursa ya kutoa Kauli
ya Serikali kuhusu Mgogoro kati ya Wakulima na Wafugaji Wilayani Kiteto. Aidha,
baadhi ya Waheshimiwa Mawaziri walipata nafasi ya kutoa Kauli mbalimbali za
Serikali kama ifuatavyo:
i) Kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa kuhusu taarifa zilizotolewa na Vyombo vya Habari za shutuma
dhidi ya Serikali za China na Tanzania kujihusisha na Biashara Haramu ya Pembe
za Ndovu na ile inayohusu Kuridhia Mkataba wa Umoja wa Afrika kuhusu
Demokrasia, Uchaguzi na Utawala wa Mwaka 2007;
ii) Kauli ya Waziri wa Afya na Ustawi wa
Jamii kuhusu Hali ya Dawa Nchini na Matibabu ya Saratani Nchini; na
iii) Kauli ya Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika kuhusu Mwenendo wa Soko la Nafaka na Mpango wa Ruzuku ya Pembejeo za
Kilimo.
Maazimio
Mheshimiwa Spika,
6.
Tarehe 7 Novemba, 2014 Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya
kujadili na kupitisha Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Anne Semamba
Makinda (Mb.), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa
Mabunge ya Nchi
Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-PF). Aidha, katika Mkutano huu
Waheshimiwa Wabunge walipata pia fursa ya kujadili na kuridhia Maazimio mengine yafuatayo:
i)
Azimio la Bunge kuhusu Itifaki ya
Kuanzishwa kwa Tume ya Utafiti wa Afya, Jumuiya ya Afrika Mashariki;
ii)
Azimio la Bunge la Kufuta na Kusamehe
Madai au Hasara itokanayo na Upotevu wa Fedha na Vifaa vya Serikali kwa Kipindi
Kilichoishia tarehe 30 Juni, 2011;
iii) Azimio la Bunge
la kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu Ushirikiano katika
Masuala ya Kiulinzi [The East African
Protocol on Cooperation in Defence Affairs]; na
iv) Azimio la Bunge
la Kuridhia Itifaki ya Uzuiaji wa Vitendo Haramu dhidi ya Usalama wa
Miundombinu ya Kudumu iliyojengwa chini ya Bahari katika Mwambao wa Bara ya
Mwaka 1988 [The Protocol for the
Suppression of Unlawful Acts Against the Safety of Fixed Platforms located on
the Continental Shelf – SUA, 1988].
e) Taarifa Maalum za Kamati
Mheshimiwa Spika,
7.
Mwisho, lakini siyo kwa umuhimu,
Waheshimiwa Wabunge walipokea Taarifa Maalum ya Kamati ya Hesabu za Serikali (Public Accounts Committee - PAC)
Kuhusiana na Miamala iliyofanyika katika Akaunti ya “ESCROW” ya TEGETA pamoja na umiliki wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Mheshimiwa Spika,
8.
Naomba nitumie fursa hii, kwanza
kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika kwa kuruhusu Kamati ya Hesabu za Serikali
(PAC) kuwasilisha Taarifa hii Maalum kwenye Bunge lako Tukufu kwa mujibu wa
Kanuni za Bunge. Aidha, niwashukuru Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Kamati kwa
uchambuzi wao wa kina na Mapendekezo yao kama yalivyowasilishwa katika Mkutano
huu. Nitumie fursa hii pia kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri waliozungumza kwa
niaba ya Serikali nzima kutoa maelezo yaliyolenga kutoa ufafanuzi wa hali
halisi ya suala hili la Akaunti ya ESCROW
ya TEGETA na pia kujibu baadhi ya Hoja za Kamati.
HAPA
AMEONGELEA MASUALA YA ESCROW ACCOUNT.
UCHAGUZI
WA SERIKALI ZA MITAA
a)
Maandalizi ya Kupiga
Kura tarehe 14 Desemba, 2014
Mheshimiwa
Spika,
9.
Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa
Tanzania Bara unatarajiwa kufanyika tarehe 14 Desemba, 2014. Uchaguzi huo ni wa
kawaida na unahusisha Uchaguzi wa Wenyeviti
wa Vijiji, Vitongoji, Mitaa, Wajumbe wa Halmashauri za Vijiji na Wajumbe wa
Kamati za Mitaa. Taarifa nilizonazo ni kwamba hadi sasa maandalizi ya
Msingi kuwezesha Uchaguzi huo kufanyika yamekamilika.
Mheshimiwa Spika,
10.
Ili
kuhakikisha kuwa Uchaguzi huo unafanikiwa, maandalizi ya Kanuni za Uchaguzi
yalifanyika kupitia Vikao vya Wadau mbalimbali ili kupata maoni, mapendekezo na
ushauri ambao umesaidia katika kuboresha Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa. Wadau walioshirikishwa ni pamoja na Viongozi wa Vyama vya Siasa vyenye
Usajili wa Kudumu; Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za
Serikali za Mitaa na Asasi Zisizo za Kiserikali (AZAKI).
b)
Uandaaji wa Kanuni za
Uchaguzi za Mwaka 2014
Mheshimiwa
Spika,
11.
Katika
maandalizi ya awali, orodha ya Vijiji, Mitaa na Vitongoji iliandaliwa na
kuchapishwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 22 Agosti, 2014 lenye Tangazo
la Serikali Namba 300 kwa
Halmashauri za Miji na Tangazo Namba 301
kwa Halmashauri za Wilaya. Orodha hiyo imejumuisha Kata, Vijiji na Mitaa.
Katika Uchaguzi wa mwaka huu, jumla ya Vijiji 12,443, Vitongoji 64,616
na Mitaa 3,741 vitahusika kwenye
Uchaguzi.
Mheshimiwa
Spika,
12.
Ili
kufanikisha Uchaguzi huo, Serikali imekwishaandaa na kuchapisha Vipeperushi,
Fomu za Wagombea, Rejesta ya Wapiga Kura, karatasi za kuonyesha Vituo vya
Kupigia Kura, Mabango na Matangazo mengine kuhusu Elimu kwa Mpiga Kura. Tayari
vifaa hivyo vimepelekwa Mikoani na vingine vinaendelea kupelekwa. Aidha,
Masanduku ya Kupigia Kura yameshanunuliwa na tayari yameshasambazwa katika
Mikoa yote Tanzania Bara.
Mheshimiwa
Spika,
13.
Kwa
vile siku zilizobakia kufikia tarehe ya Kupiga Kura ni chache, natoa Wito kwa
Wananchi ambao hawajajiandikisha katika Rejesta ya Wapiga Kura wafanye hivyo bila
kukosa. Aidha, Viongozi wa Vyama vya Siasa wawahimize Wanachama wao na Wananchi
kwa ujumla wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na hatimaye wajitokeze siku ya
Kupiga Kura. Aidha, Wasimamizi wa Uchaguzi wahakikishe vifaa vya Uchaguzi
vinafika kwenye maeneo yao kwa wakati.
Mheshimiwa
Spika,
14.
Napenda
nitumie nafasi hii kutoa Rai kwa Viongozi wa Vyama vya Siasa waendeshe kampeni
kwa amani na kuepuka maneno ya uchochezi, kubaguana kwa misingi ya ukabila,
rangi, udini ama hali ya mtu mambo ambayo yanaweza kusababisha vurugu na
uvunjifu wa amani. Aidha, nawaomba Viongozi wa Vyama vya Siasa na Wanachama wao,
wakishapiga kura wasiendelee kukaa katika Vituo vya Kupigia Kura, bali watawanyike
na kusubiri muda wa matokeo.
HITIMISHO
Mheshimiwa
Spika,
15.
Leo
nimeona nizungumzie masuala muhimu yanayochangia kusukuma Gurudumu letu la
Maendeleo. Kabla sijahitimisha hotuba yangu, naomba nitumie nafasi hii
kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha Mkutano huu. Kipekee nikushukuru wewe
Mheshimiwa Spika, pamoja na Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri. Niwashukuru Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri
ya kuongoza vikao vya Bunge lako Tukufu.
Aidha, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri na kwa
michango mbalimbali wakati wa Mkutano huu.
Mheshimiwa
Spika,
16.
Naomba
pia nimshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake wote pamoja na Wataalam wote
wa Serikali na Taasisi zake ikijumuisha Taasisi za Sekta Binafsi, kwa misaada
ya Kitaalam na huduma mbalimbali za kufanikisha Mkutano huu. Niwashukuru pia
Waandishi wa Habari kwa kazi nzuri walizofanya kuhakikisha kuwa taarifa za
majadiliano na maamuzi mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia Wananchi. Niwashukuru
Madereva kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuwasafirisha kwa usalama Waheshimiwa
Wabunge, Viongozi mbalimbali, Wataalam na Wasaidizi wote walioshiriki katika
Mkutano huu.
Mheshimiwa
Spika,
17.
Nimalizie
kwa kuwatakia wote safari njema mnaporejea kwenye maeneo yenu ya kazi na katika
majimbo yenu. Aidha, niwatakie mapumziko
mema ya Sikukuu ya Christmas na Mwaka Mpya wa 2015. Ninaamini kwamba, Mwenyezi
Mungu atatulinda na kutuvusha salama sote kama tulivyo hadi kuuona Mwaka Mpya wa
2015. Baada ya kusema hayo, naomba sasa
kutoa Hoja kwamba, Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 27 Januari, 2015 saa 3:00 Asubuhi litakapokutana katika
Mkutano wa 18 kwenye Ukumbi huu hapa
Dodoma.
Mheshimiwa
Spika,
18.
Naomba
kutoa Hoja.
No comments:
Post a Comment