Amesema Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) imeanza kuchukua hatua
ya kukusanya kodi hizo kwa kuwa kamwe serikali haiwezi kuacha fedha za
wananchi kupotea.
Alisema hayo alipokuwa akichangia mjadala PAC kufuatia ukaguzi
maalumu uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) katika akaunti hiyo, bungeni jana.
Alisema suala la kodi hiyo limegawanyika katika maeneo matatu,
ikiwamo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), ambayo alisema kama ingekatwa
kwenye chanzo, leo kusingekuwa na mjadala wowote kwa wabunge.
Hata hivyo, alisema kufuatana na taratibu za kiutekelezaji, kodi hiyo haikukatwa hali, ambayo imesababisha kuzua mkanganyiko.
Hivyo, akasema TRA inashughulikia jambo hilo na kwamba, VAT ambayo ilikuwa haijakatwa ilikuwa ni Sh. bilioni 26.97.
Alisema baada ya TRA kugundua hilo, ilichukua hatua haraka na kukusanya Sh. bilioni 4.21, ambazo tayari zimelipwa serikalini.
Mwigulu alisema ukaguzi uliofanyika ni kwenye akaunti ya Tegeta
Escrow na siyo kwenye kampuni ya kufua umeme ya Independent Power
Tanzania Limited (IPTL) na kwamba, TRA inaendelea na utaratibu
kuhakikisha kodi hiyo inalipwa. "Na mimi niwatangazie Watanzania kwamba,
kodi hiyo lazima italipwa. Kodi iliyosalia lazima italipwa," alisema
Mwigulu.
Aliiagiza TRA kuendelea na utaratibu wa kuhakikisha kwamba, kodi
hiyo lazima inalipwa akisema haiwezekani Watanzania wakawa na mahitaji
mengi halafu ikatokea serikali kuacha kukusanya kodi.
"Hatuwezi tukaacha kodi kubwa namna hii. Mwenyekiti narudia tena,
hatuwezi tukaacha kodi kubwa namna hii kwa tajiri halafu tukakimbizana
na mama mjane anayeuza mchicha barabarani," alisema Mwigulu.
"Kwa hiyo, kodi hii lazima italipwa na anayehusika ajiandae kisaikolojia kwamba, kodi hii lazima italipwa."
Alisema kodi nyingine, ambayo taifa limeikosa ni ile iliyotokana na kukosewa kwa mahesabu na kusema lazima nayo pia ilipwe.
Alisema TRA tayari imeshaanza kuchukua hatua mbalimbali; ya kwanza
ikiwa ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo kuandika barua Novemba 19 ya
kusudio la kufuta hati na kwamba, baada ya hapo Novemba 27, mwaka huu,
Msajili wa Kampuni (Brela) walipewa barua inayofuta kodi ya ongezeko la
mtaji. Aliwataka Watanzania kutokuwa na shaka juu ya TRA, kwani hiyo
nitaasisi ya serikali, ambayo imefanya uchunguzi wake.
Alisema, uchunguzi huo wa TRA ndiyo uliokwenda kutolewa PAC na kwamba, hatua zimechukuliwa na serikali iko makini.
Alisema taifa lolote duniani lina watu waaminifu na wasiokuwa
waaminifu na kwa hiyo, kuna mtu nchini aliyepewa kazi, ambaye badala ya
kuandika dola za Kimarekani milioni sita ili kodi ikusanywe, akaandika
fedha za Kitanzania Sh. milioni sita.
Alisema mtu huyo aliyemwita kuwa ni 'msomi wa Kitanzania'
aliyesoma kwa kodi za Watanzania waliojinyima, pia ili kuandika dola za
Kimarekani milioni 20 ili kodi halisi ipatikane, aliandika fedha za
Kitanzania Sh. milioni 20.
Alimuagiza Kamishna wa TRA kuchukua hatua za ndani ya mamlaka hiyo
za kinidhamu dhidi ya mtu huyo na kusema kwenye hilo hakuna uchunguzi
juu ya uchunguzi.
Alisema uchunguzi juu ya mtu huyo umekwishafanyika, kwani ameandika
shilingi za Kitanzania badala ya dola za Kimarekani na hivyo kuikosesha
nchi mapato kwa makusudi.
"Kwa hiyo, mimi niagize wafuate taratibu za ndani ya Mamlaka ya
Mapato, lakini na yeye atafute kazi nyingine ya kufanya inayomtosha
kutafsiri dola za Kimarekani kuwa sawa sawa na shilingi za Kitanzania,"
alisema Mwigulu.
Alisema kwa kukosekana kodi hiyo, tafsiri yake ni kwamba, kuna watu
waliopoteza maisha kutokana na kukosekana kwa dawa hospitalini na
watoto wa maskini waliofaulu vizuri waliostahili kuendelea mbele na
masomo wamekosa mikopo.
Mwigulu alisema alishawahi kusema kuwa mtu aliyesababisha hasara,
aliyeiba na aliyetumia kodi vibaya, akiwajibishwa kwa kujiuzulu peke
yake ni sawa na kumpa likizo ya kwenda kutumia fedha alizoiba.
Hivyo, aliiagiza Takukuru na vyombo vingine kuchukua hatua inayostahili kwenye jambo hilo ili iwe funzo kwa wengine.
Kuhusu fedha za akaunti ya Tegeta Escrow, alisema wote waliopokea
mgao wanatakiwa walipie kodi ya mapato kabla ya Desemba 31, mwaka huu na
baada ya hapo TRA itawashukia, kwani huo ni utaratibu wa kawaida
kisheria.
Kuhusu fedha zilizopakiwa kwenye sandarusi, lumbesa, magunia na
maboksi, Mwigulu alisema amefuatilia na kuambiwa kuwa zilitoka kwa
kufuata utaratibu za kutoka benki.
Hata hivyo, alisema taratibu za kisheria zinasema kuwa ikishazidi
Sh. milioni 10 hairuhusiwi kutoka hata kwa hundi, badala yake inatakiwa
ifanyike kwa kutumia mfumo wa kieletroniki.
"Kwa hiyo, walichofanya ndiyo maana wengi wale walifungua kwenye
Benki ya Mkombozi, walienda kufungua pale halafu ikafanyika internal
transfer ambayo ya kielektroniki, na zingetoka kwa magunia tusingejua
hata nani kachukua. Kwa hiyo, utaratibu wa kibenki unazuia mtu kubeba
kwa gunia kwa sababu akibeba kwa gunia huwezi ukajua hizo fedha
zimeingizwa kwa nani," alisema Mwigulu.
Hata hivyo, aliwaagiza watendaji wakuu wa benki za Stanbic na
Mkombozi zilizotajwa katika kashfa hiyo, kutoa matamko kama walitoa
fedha hizo kwa magunia au kwa taratibu za kawaida na Gavana wa BoT
asimamie jambo hilo kuhakikisha taasisi hizo zinatekeleza agizo hilo ili
kuwaweka wazi wananchi na kuwaondolea wasiwasi.
Alisema kuna kuongea na kuchukua na kwamba, jambo la msingi, ambalo Watanzania wanalisubiri ni kuchukua hatua.
Mwigulu alisema wengi wamekuwa wakifurahia hatua za kuwashughulikia
wanasiasa enzi hizi, kama vile wataalamu waliosoma kwa kodi za
Watanzania hawawajibiki popote na taifa.
KAFULILA
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alisema
katika Benki ya Stanbic tayari mhusika aliyefungua akaunti kwa ajili ya
kampuni ya PAP iliyopokea fedha za Escrow amefukuzwa kazi na kurudi kwao
Uganda.
SENDEKA
Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, amemshambulia
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, akisema alipewa
na kampuni ya (IPTL) dola za Marekani milioni 95 ofisini kwake na
kusema kitendo chake cha kuwa mtu wa kati ya Harbinder Singh Sethi
na James Rugemalira, kinaonyesha kuwa hakikuwa tu cha udalali, bali
ukuwadi.
Sendeka alisema taarifa ya PAC imeeleza ukweli usio na shaka
kwamba, Profesa Muhongo alifanya kazi ya udalali kwa kuiwakilisha
Kampuni ya PAP kwenye mazunguzo na IPTL na kupewa dola za Marekani 95
ofisini kwake.
Alisema hayo huku akinukuu ukurasa wa tano kati ya PAP na VIP katika mkataba.
PROFESA MUHONGO
Baada ya kusoma kipengele hicho cha mkataba, ghafla alisimama
Profesa Muhongo na kuomba mwongozo wa Mwenyekiti na kusema kuwa
alichokisema mzungumzaji siyo sahihi. Hata hivyo, muda wote Waziri
Muhongo alikuwa akibabaika, huku akijikuta akizongwa na makelele ya
wabunge wa pande zote ndani ya Bunge.
Hali hiyo ilimlazimu Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, kusimama na
kulieleza Bunge kuwa alichokisema Sendeka ni sahihi siyo kama alivyosema
Waziri Muhongo kwenye maelezo yake.
Baada ya maelezo hayo ya Zitto, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu,
alimruhusu Sendeka kuendelea na mchango wake na kusema aliyoyasema
hayatoi kichwani mwake, bali kwenye mkataba uliosainiwa na Waziri
Muhongo ofisini kwake, ambao ameshiriki.
"Siku ile kwenye mkutano wa Bunge lililopita nilileta nyaraka,
ambazo Profesa Muhongo aliziita ni nyaraka za kufungia maandazi. Leo hii
tena na hizi alizozileta CAG ni za kufungia maandazi? Hakuna mashaka
kwamba Profesa Muhongo katika dili hili alikuwa dalali," alisema
Sendeka.
“Na ninataka niwaombe eti alisimama hapa kutoa utetezi wa serikali
alikuwa anatoa utetezi dhidi yake na uhalifu wake na wahalifu walioko
chini yake, katika hili ninawaomba mwacheni Waziri Mkuu kwani hausiki na
jambo lolote ila kwa suala la Lowassa kwa sababu aliingia ndio maana
aliwajibika." Sendeka alisema Bunge lina wabunge wa CCM asilimia 78 na
asilimia 22 ni wabunge wa vyama vya upinzani.
“Kama CCM yenye asilimia 78 ikiamua kuwakumbatia wahalifu, ikiamua
kuwalinda wahalifu kwa namna yoyote ile maana yake Bunge lako tukufu
litakuwa limeamua kuwalinda na Bunge lako tukufu litakuwa limewalinda,"
alisema Sendeka.
Aliongeza: “CCM tujipambanue na uhalifu huu, Serikali ya CCM
ijipambanue na uhalifu huu, kashfa hii si ya Serikali si ya CCM ni ya
wachache waliopewa dhamana katika ofisi hizo za umma."
Alisema kutokana na hali hiyo, hakuna uwajibikaji wa pamoja katika
Baraza la Mawaziri na kupongeza kauli ya Nchemba kwa kusimamia ukweli
siku zote.
“Wahalifu hao ni lazima wabebe msalaba na wavune
walichokipanda...Mwekezaji anakuja na dola za Marekani 300,000
akastahili kulipwa mtambo wa mabilioni na bilioni 306,” alisema Sendeka.
Wakati akiendelea kuchangia, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mariam
Kisangi, aliomba kutoa taarifa kuwa mchangiaji asilipotoshe Bunge
kwamba, hakuna aliyesema ripoti ya CAG kuwa ni ya Uongo."
Akijibu taarifa hiyo, Sendeka alisema Kisangi siyo 'saizi' yake na
hana haja ya kubishana naye na kumrushia kijembe kuwa ni mmoja wa watu,
ambao wanafanya biashara ya mafuta na hata kuisimamia Kamati ya Bunge ya
Nishati na Madini.
NKUMBA
Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba (CCM), alisema katu haungi mkono
wizi wa fedha hizo, huku akitaka kujua wema wa Mkurugenzi wa kampuni ya
VIP Engeering, James Rugemarila kwa kugawa fedha kwa viongozi wenye
majina makubwa.
“Nimeangalia jambo lote hili na kuna chembe ya uchafu upo. Kitendo
cha kuaacha watu waliohusika na kuwachanganya wasiohusika utaleta utata
katika maamuzi. Ninasema kutoka moyoni, ninavyoangalia mchakato wote na
jambo hili," alisema Nkumba.
Alisema Sikonge kuna watu masikini, Kagera pia kuna watu masikini lakini fedha zinapelekwa kwa watu ambao wameshatosheka.
GHASIA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia,
alisema katika suala hilo watu wote waliohusika wachukuliwe hatua kwa
mujibu wa sheria bila kumuonea mtu.
LAIZER
Mbunge wa Longido, Lekule Laizer (CCM), alisema anashangazwa na
kitendo cha Bunge kumpa nafasi Waziri Muhongo kujitetea kwa niaba ya
serikali hali ya kuwa kitendo kama hicho hakijawahi kufanyika huko
nyuma.
“Hili jambo ni kubwa na ni lazima tujitafakari, halina itikadi
lakini inakuaje eti mtu analeta utetezi mbele ya Bunge … mbona hakufanya
huko nyuma? Kama ndiyo hivyo maana tulichukua hatua huko nyuma ni
lazima
aje hapa mbele Lowassa (Edward), Kagasheki na Mathayo pamoja na
wengine tuwaombe radhi, maana wao tuliwachukulia hatua bila kuwapa
nafasi ya kujitetea,” alisema Laizer.
MNYIKA
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alisema fedha kwenye
akaunti hiyo zilichotwa wakati aliyekuwa Waziri wa Fedha, marehemu Dk.
William Mgimwa, akiwa amelazwa na kwamba, baadhi ya watu wamehusisha
kifo chake uporwaji wa fedha hizo.
SERUKAMBA
Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba, alisema hoja kwamba,
mwekezaji ameshusha bei ya umeme haina msingi, kwani gharama za
uendeshaji bado ziko juu na kushauri anyang'anywe mitambo ya IPTL na
kulikabidhi Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ili kuijengea nchi
heshima.
Pia alishauri Benki ya Stanbic iandikiwe barua kuibana kurejeshwa kwa fedha hizo.
CHEYO
Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo, aliipongeza PAC kwa kazi nzuri.
WASSIRA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen
Wasira, aliviagiza vyombo vinavyohusika kuchunguza waliobeba fedha
kwenye magunia, viroba, sandarusi na maboksi akisema jambo hilo haliwezi
kuvumiliwa.
PROFESA MWANDOSYA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark
Mwandosya, alisema fedha za Escrow zilikuwa ni za umma kwa kuwa zilikuwa
zikihifadhiwa BoT.
ZITTO
MWENYEKITI wa PAC, Zitto Kabwe, jana alihoji bungeni kuwa kama
Ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti wa Fedha (CAG) Mamlaka ya Mapato (TRA) na
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) zinasema fedha za
Akaunti ya Escrow ni za umma nani mwingine mwenye mamlaka hayo.
Alisema ripoti zote hizo zinaonyesha kuwa fedha za Akaunti ya
Escrow ni za umma na kwamba hakuna mtu mwingine anayeweza kulipinga.
MAAZIMIO YA BUNGE
Baadhi ya maazimio yaliyopendekezwa na Wabunge ni kufanyika kwa
uchunguzi kwa wote waliotajwa kuhusika katika sakata la fedha za Akaunti
ya Escrow uendelee na kisha wafikishwe mahakamani.
Azimio la pili: Wote waliotajwa katika sakata hilo wavuliwe nyadhifa zao zote watakapobainika kuwa walihusika.
Azimio la tatu: Walionufaika na mgawanyo wa fedha wanatakiwa kutaja
zawadi walizopata na kuchukuliwa hatua mahususi kwa mujibu wa sheria.
Azimio la nne: Kamati inazitaka mamlaka zinazohusika ikiwano Benki
Kuu kuchukua hatua za kisheria dhidi ya benki zote zilizohusika na
miamala ya Akaunti ya Escrow
Azimio la tano: mikataba ya makampuni yote yanayozalisha umeme ipitiwe upya.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment