Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa, Rosalia Mwenda |
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Iringa itaendelea kufuatilia kwa karibu matumizi ya mashine za kielektoniki za kutolea risiti kwa wafanyabiashara wa mkoani hapa wanaotakiwa kwa mujibu wa sheria kutumia mashine hizo.
Wafanyabiashara hao kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Menejea wa TRA Mkoa wa Iringa, Rosalia Mwenda ni pamoja na wale waliosajiliwa kwa ajili ya kukusanya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na wale wa awamu ya pili ambao mauzo yao kwa mwaka ni Sh Milioni 14 na zaidi.
Akizungumza na wanahabari kuhusu maadhimisho ya nane ya siku ya mlipa kodi (Novemba 11-21, 2014), Mwenda alisema wakati wafanyabiashara 533 wamesajiliwa kwa ajili ya VAT, wengine 1,240 wamesajiliwa awamu ya pili ya matumizi ya mashine hizo baada ya kutambuliwa kuwa na mauzo ya zaidi ya Sh Milioni 14 kwa mwaka.
“Katika awamu hii ya pili lengo letu ni kuandikisha zaidi ya wafanyabiashara 5,000; kumekuwepo na changamoto katika kufikia lengo hilo, pamoja na hayo yote tunaendelea na kazi hiyo ili tufikie lengo hilo,” alisema.
Alitaja moja ya changamoto iliyosababisha wasifikie lengo hilo kuwa ni pamoja na kuendelea kwa migomo ya baadhi ya wafanyabiashara walioko katika awamu hiyo ya pili ya kununu na kutumia mashine hizo.
“Wakati wafanyabiashara hao wanapinga kutumia mashine hizo, baadhi ya wale walioko katika kundi la VAT hawatumihi ipasavyo mashine hizo,” alisema.
“Tunapoadhimisha siku ya mlipa kodi ujumbe wetu kwa walipakodi wetu ni kuakumbusha kaulimbiu ya Risiti ni haki yako, asiyetoa anakwepa kodi,” alisema.
Akizungumzia hali ya makusanyo ya kodi katika kipindi cha 2013/2014, Mwenda alisema mkoa wa Iringa ulipangiwa kukusanya jumla ya Sh 37,575,300,000 hata hivyo haukuweza kufikia lengo hilo baada ya kukusanya Sh 35,845,879,036 ambayo ni sawa na asilimia 96.
Akiwasihi wapiga kura wa mkoani hapa, Afisa wa TRA mkoani hapa anayehusika na elimu kwa walipa kodi, Faustine Masunga alisema; “Watu wasiwaogope maafisa wa TRA na wala wasiogope au kukwepa kulipa kodi kodi kwasababu bila kodi nchi haiwezi kutekeleza mipango yake.”
Alisema TRA ilianza kusheherekea siku ya mlipakodi mwaka 2006 kwa lengo la kuwatunukua walipakodi ambao wapo mstari wa mbele katika kuweka kumbukumbu zao za biashara:
“Wanaolipa kodi zinazolingana na biashara zao, wanaojituma kulipa kodi kwenye tarehe zinazokubalika kisheria na wale wanaolipa kodi zao kwa hiari.
Masunga alisema kilele cha maadhimishi ya wiki hiyo ya mlipa kodi kitafanyika katika ukumbi wa IDYDC, Novemba 21, mwaka huu. (BONGO LEAKS)
No comments:
Post a Comment