Mkoa wa Iringa wameamua kuadhimisha Kumbukumbu ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwa shughuli ya upandaji Miti.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza alisema hayo leo kuwa watu wanatakiwa kutambua umuhimu wa miti katika maisha yao.
“Mkoa umeona ni muhimu kutumia maadhimisho haya kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kutunza Mazingira hasa upandaji wa Miti, ulindaji na utunzaji wa Vyanzo vya Maji,” alisema mkuu wa mkoa huyo.
Kumbukumbu ya Maadhimisho ya Miaka 51 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yaliyofanyika tarehe 12 Januari, 1964.
Katika maadhimisho hayo mkoa ulilenga kupanda miti 3,500 ya mbao na vivuli lakini walipanda miti 1,500 na miti iliyobaki mkoa umeandaa utaratibu maalumu kwa kuzipatia halmashauri kwa kushirikiana wananchi wapande katika maeneo yao.
Aidha, mkuu wa mkoa huyo aliwakumbusha kuwa Upandaji Miti na Usafi wa Mazingira ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2010. Ilani hiyo inaelekeza umuhimu wa kutunza Vyanzo vya Maji na kuhamasisha Usafi wa Mazingira.
Pia inasisitiza kuwahamasisha wananchi kudhibiti matumizi mabaya ya rasilimali kama Misitu na kuhamasisha utunzaji wake.
Kutokana na umuhimu wa Misitu katika maisha ya Mtanzania, Sera ya Taifa ya Misitu ya Mwaka 1998 na Sheria ya Misitu Na. 14 ya Mwaka 2002 na Kanuni za Uendeshaji wa Misitu za Mwaka 2004, zimesisitiza uhifadhi na ulinzi wa Misitu nchini.
Aidha, ushiriki wa wananchi na wadau umehimizwa katika kuhifadhi Misitu iliyopo, kupanda Miti na kuitunza.
Aliongeza kuwa kutokana na umuhimu na misingi hiyo Mkoa umeona ni busara kuyatumia Maadhimisho haya ya Kumbukumbu ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kuwahamasisha wananchi na kushiriki kwa vitendo katika zoezi la upandaji Miti pamoja na kutoa elimu ya juu ya matatizo yatokanayo na kutokuwa na Misitu.
Katika Sekta ya Kilimo, alisema kuwa ni muhimili katika kukuza uchumi wa Kaya na Mkoa kwa ujumla. Sekta hii inaongoza na inategemewa na zaidi ya asilimia 80 ya wananchi, ikiwa ina changia katika utoaji wa ajira kwa asilimia 85 ya wakazi wa Mkoa wa Iringa.
Aidha, Wilaya ya Mufindi ndiyo inaongoza kwa kuwa na Kaya nyingi ikiwa na Kaya 64,392 sawa na asilimia 41 zinazojishughulisha na Kilimo.
Lengo la Mkoa ni kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa na chakula cha kutosha, kipato cha Kaya kinaongezeka na Kilimo kunaendelea kuchangia na kuwa muhimili mkuu wa uchumi. Aidha, Kilimo kinachangia zaidi ya asilimia 75 ya Pato la Mkoa.
“Napenda kuwakumbusha wananchi kuwa msimu wa Kilimo umefika. Hakikisheni mnatumia vizuri mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Mufindi na Mkoa kwa ujumla kwa kupanda mazoa,” alisema.
Pia aliwashauri wakulima kuakikisha wanatumia mbegu bora katika kupanda ili kujihakikishia mazao mazuri. Matumizi ya mbolea wakati wa kupandia na kukuzia ni muhimu sana katika Kilimo.
Alisema kuwa Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya Kilimo hasa cha umwagiliaji maji ili wananchi waweze kuwa na uhakika wa kupata mavuno zaidi, na maeneo yanayokabiliwa na upungufu mkubwa wa mvua, kulima mazao yanayovumilia ukame hasa zao la Mtama.
Katika upande wa lishe, mkuu huyo alisema Hali ya Lishe katika Mkoa wa Iringa si yakurudhisha pamoja na ukweli kuwa Mkoa unazalisha chakula kwa wingi.
“Niongelee uhusiano uliopo kati ya Lishe na maendeleo. Hali ya Lishe ya mtu ina uhusiano mkubwa wa maendeleo yake ya kielimu, kiuchumi kwa maana ya uwezo wake wa kuzalisha mali.”
Aidha, jitihada zikiwekwa katika kuboresha Lishe ya wananchi wetu kutasaidia kupunguza ulemavu, vifo na gharama za matibabu.
Katika kukabiliana na hali ya upungufu wa Lishe katika Mkoa wa Iringa, Mkoa wa Iringa unaendelea kutekeleza Mikakati ya kukabiliana na tatizo la Lishe.
Mikakati hiyo ni pamoja na:- Kuhakikisha wanawake kabla, wakati na baada ya ujauzito kupata ushauri wa lishe stahiki.
Unyonyeshaji sahihi na ulishaji wa vyakula vya nyongeza kwa wakati sahihi kwa mtoto.
Huduma za nyongeza ya matone ya vitamin “A” na uongezaji wa virutubishi kwenye vyakula.
katika upande wa sekta ya elimu alisema kuwa serikali itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kutoa na kuboresha elimu kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa.
Msimu huu ni msimu wa shule kufunguliwa. Baadhi ya shule zimefunguliwa na nyingine zinafungua wiki hii.
Nitoe rai kwenu wazazi na uongozi wa Wilaya zote kuhakikisha watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza Mwaka huu 2015 wanaripoti katika shule walizopangiwa katika muda uliopangwa.
Mkoa wetu unatambua kuwa elimu ni urithi mzuri zaidi kwa watoto na wananchi, hivyo tutaendelea kuwa wakali katika kuhakikisha suala la elimu linakuwa ni mkombozi kwa wananchi wetu wote.
Aidha, katika matokeo ya darasa la saba, Mkoa wetu umefanya vizuri na kushika nafasi ya Nne Kitaifa kati ya Mikoa 25 ya Tanzania Bara.
Ujenzi wa Maabara:
Suala la ujenzi wa Maabara ni endelevu. Nichukue nafasi hii kuwapongeza wananchi wote na uongozi wa Mkoa wa Iringa kwa kazi nzuri mliyoifanya ya ujenzi wa Maabara za shule za Sekondari.
Niwakumbushe tu kuwa zoezi hilo la ujenzi wa Maabara TATU kwa kila shule ya sekondari linaendelea kwa kasi ile ile. Hakuna kupumzika hadi zoezi hili litakapokamilika. Nimatumaini yangu kuwa ushirikiano huu mliouonesha katika ujenzi wa Maabara utaendelea ili kuhakikisha Maabara zote zinakamilika katika Shule za Sekondari Mkoani Iringa.
Maambukizi ya Ukimwi:
Hali ya maambukizi ya Ukimwi katika Mkoa wa Iringa bado ni kubwa. Mkoa unashika nafasi ya pili kitaifa kwa Maambukizi ya Ukimwi ukiwa na asilimia 9.1 ya maambukizi.
Wananchi wote kwa umoja wetu ni lazima tubadili tabia zinazopelekea maambukizi ya Ukimwi. Serikali kwa upande wetu tutaendelea kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi mapya ya Ukimwi kwa wananchi.
Tunaamini Mkoa wa Iringa bila maambukizi mapya ya Ukimwi inawezekana kwa kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake.
Ulinzi na Usalama:
Hali ya Ulinzi na Usalama ni shwali katika Mkoa wetu wa Iringa. Vyombo vya usalama vitaendelea kuwa makini kuhakikisha amani na usalama vinaendelea kuwepo ili wananchi wetu waweze kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Kila mwananchi lazima awe mlinzi wa mwenzake. Pale utakapoona mwenendo wa mwenzako unatia shaka ni vizuri kutoa taarifa kwa viongozi na vyombo vya usalama.
Tukifanya hivyo hakika Mkoa wetu utaendelea kuwa salama na wananchi wote tutakuwa salama na kuendelea na kufanya kazi za uzalishaji mali kwa amani na utulivu.
No comments:
Post a Comment