Wednesday, 4 March 2015

WANANCHI WATAKIWA KUCHANGIA ELIMU


Mkurugenzi wa tigo nyanda za juu kusini, Jackson Kiswaga akikabidhi moja ya bati alizotoa kwa shule mbalimbali za jimbo la Kalenga wilaya ya Iringa.


NA DENIS MLOWE, IRINGA

WANANCHI wa jimbo la Kalenga wametakiwa kujenga utamaduni wa kuchangia maendeleo ya sekta ya elimu, badala ya kujikita kuchangia sherehe za harusi na mambo mengine yasiyokuwa na tija katika maendeleo ya jimbo hilo.

Hayo yamezungumzwa na mdau wa maendeleo, Jackson Kiswaga wakati akikabidhi mabati 50 na mifuko ya saruji 30 kwa shule ya sekondari ya Nyabula inayomilikiwa na kanisa katoriki parokia ya Nyabula katika sherehe ya kuchangia ujenzi wa maabara ya Shule hiyo iliyoko katika wilaya ya Iringa vijijini.

Kiswaga alisema kuwa urithi pekee kwa watoto ni elimu hivyo ni jukumu la wazazi kuchangia sekta ya elimu kuliko kusubiri serikali ambayo ina mzigo mkubwa kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo katika kukuza uwezo wa wanafunzi katika mambo ya masomo.

“Mzazi unaweza kumwachia kijana wako mali, lakini itakwisha, ukimwachia elimu hakika huu ndiyo urithi pekee watanzania wenzangu, tujitoe kuchangia sekta ya elimu kama ambavyo tunafanya katika sherehe na kumbuka maisha ya sasa bila elimu utasababisha mwanao awe katika maisha magumu hapo mbeleni hivyo tusisubiri serikali tuwe na utamaduni wa kuchangia katika sekta hii ya elimu ndugu zangu,” alisema Kiswaga.

Alisema kuwa juhudi za wananchi na mashirika pamoja na serikali zinahitajika ili kuwajengea wanafunzi mazingira bora ya kujifunzia na ili waweze kufaulu vizuri katika masomo yao hivyo kuchangia maabara itasaidia sana kukuza uwezo wa mwanafunzi katika masomo ya sayansi pindi yakikamilika.

Kiswaga aliongeza kuwa sekta ya elimu ni sekta muhimu sana kwa maendeleo ya nchi ambapo inabidi juhudi zaidi ziongezeke kuweza kuifanya elimu kuwa silaha bora itakayowasiadia vijana kuondokana na umaskini.

Naye Padri wa Parokia ya Nyabula Philipo Kindole alimshukuru Kiswaga kwa msaada wa mabati na saruji na kuwataka wananchi wengine kuiga mfano huo kwa maendeleo ya elimu katika mkoa wa Iringa.
…mwisho….

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...