Friday, 24 April 2015

DKT. MAHIGA: SIJAKUBALI WALA KUKATAA USHAWISHI WAKUGOMBEA URAIS



Balozi Dkt. Augustine Mahiga ni mmoja wa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotajwa kuwa nyuma ya kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwamba kuna watu wanauwezo wa kurithi nafasi yake, lakini hawajajitokeza.

Balozi wa kudumu katika umoja wa mataifa huyo amesema kuwa bado hajakataa wala kukubali ushawishi unaofanywa na makundi ya watu juu ya kuwania nafasi ya urais kupitia CCM katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Akizungumza na waandishi mara baada ya kumalizika kwa mahafali kuongea na wanafunzi wa Shule ya sekondari ya Tosamaganga iliyopo wilaya ya Iringa, Balozi Mahiga alisema tangu Rais Kikwete atamke tamko la kimapinduzi kule Songea na gazeti la Raia Mwema kuandika watu wamekuwa wakijitokeza kumshawishi kuwania nafasi hiyo kupitia CCM.

Pamoja na balozi Dk. Mahiga wengine wanaotajwatajwa nyuma ya kauli ile ni pamoja na aliyekuwa Jaji mkuu Augustine Ramadhani.
Alisema kushawishiwa kuchukua fomu kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo nyeti kwa taifa ni jambo moja, jingine ni mchakato mzima wa kukamilisha masharti ya chama ikiwemo kuzunguka mikoa 10 kupata wadhamini na tatu ni kazi ya chama.

“Nimepata makundi ya watu na mtu mmoja mmoja wakinishauri  nichukue fomu ya kuwania urais baada ya Rais Kikwete kutoa kauli kule Songea mkoani Ruvuma, lakini bado sijakubali wala kukataa ushawishi huo”, alisema Balozi Dk. Mahiga.

Aidha alisema kumekuwepo na hali ya wanaowania nafasi ya urais kutumia fedha jambo ambalo litalifikisha taifa mahali pabaya kwa kumpata mtu asiyestahili.

Alisema endapo ikitokea akachaguliwa Dk. Mahiga alisema ni vema rais ajaye akawa na sifa zinazoenea na kuelezeka ili kuweza kupokea kijiti kutoka kwa Rais wa sasa na kulipeleka mbele taifa katika kipindi cha miaka mingine.

Alizitaja sifa za rais ajaye kuwa ni pamoja na kuwa na uwezo wa kuzitatua changamoto ambazo hazijaweza kutatuliwa kwa sasa ikiwemo ya ugaidi, usafirishaji wa binadamu (human trafficking) na mashabulizi dhidi ya wageni (xenophobia).

Nyingine ni kuwaunganisha watanzania kuwa kitu kimoja, muadilifu na mwenye mtazamo wa mbali kwa watanzania na taifa.

Dkt. Mahiga alisema pia kutambua matatizo ya msingi ya watanzania, uwajibikaji na kuonesha mfano kwa watumishi wa umma.

Dkt. Mahiga amepata kuwa Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban ki Moon, nchini Somalia na pia nchini Liberia wakati wa Vita ya wenyewe kwa wenyewe wakati huo yeye akifanya kazi ya kuongoza shughuli za Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la (UNHCR).

Mahiga amepata pia kuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika kipindi cha kati ya mwaka 2003 hadi 2010, ambapo alirejesha heshima ya Taifa hili kiasi cha kufikia kuwa mojawapo ya zilizounda Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Katika kipindi cha kati ya mwaka 1980 hadi mwaka 1983, Mahiga alikuwa Kaimu Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, nafasi ambayo ilimpa fursa ya kuifahamu Tanzania nje na ndani.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...