Mwanzoni mwa Mwezi Februari Baba Mtakatifu Francisko alimteua Monsinyori Liberatus Sangu kutoka Jimbo Katoliki la Sumbawanga, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Tanzania ambapo baadaye Jumapili iliyopita (tarehe 12/04/2015) aliwekwa wakfu na kusimikwa jimboni humo.
HISTORIA FUPI YA SKOFU MTEULE, LIBERATUS SANGU
Alizaliwa Februari 19, 1963 katika kijiji cha Mwanzye Jimbo Katoliki la Sumbawanga.
Baada ya kumaliza masomo ya Falsafa katika Seminari Kuu Kibosho Jimbo Katoliki Moshi na Teolojia katika Seminari Kuu ya Segerea Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, alipewa Daraja la Upadri Julai 9, 1994.
Katika maisha yake kama Padri, Askofu Mteule Sangu amewahi kuwa Mlezi wa Seminari ndogo ya Kaengesa Jimbo Katoliki la Sumbawanga kuanzia mwaka 1994 hadi mwaka 1995. Akateuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Matai kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 1996.
Mwaka 1996 hadi mwaka 1999 alikuwa Roma kwa masomo ya elimu ya juu na shahada ya Uzamili katika (Teolojia) taalimungu ya Sakramenti za Kanisa, katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Anselmi kilichoko mjini Roma.
Kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2000, aliteuliwa kuwa Msimamizi wa Parokia ya Mwanzye.
Kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2007 akateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Miito Jimbo Katoliki la Sumbawanga, mlezi katika mwaka wa malezi na Mkurugenzi wa Utume wa Vijana Jimbo Katoliki Sumbawanga.
Kunako mwaka 2007 hadi mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Paroko wa muda Parokiani Sopa. Kuanzia mwaka 2008 hadi uteuzi wake, amekuwa akitekeleza utume wake kama Afisa Mwandamizi Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu mjini Vatikani.
Itakumbukwa kwamba, Jimbo Katoliki la Shinyanga, kuanzia mwaka 2012 limekuwa wazi kufuatia kifo cha Askofu Aloysius Balina.
Historia fupi ya Jimbo Katoliki Shinyanga
Juni 24 mwaka 1950 Jimbo hilo lilikuwa Vikarieti Apostoliki ya Maswa, ilipofika Machi 25 mwaka 1953 likawa Jimbo Katoliki Maswa. Ilipofika Agosti 9 mwaka 1956 jina la jimbo hilo likabadilika likawa Jimbo Katoliki Shinyanga hadi leo.
MAASKOFU WALIOWAHI KUONGOZI JIMBO HILO
Askofu Edward Aloysius MC Gurkin, M.M. kuanzia Julai 4 mwaka 1956 hadi Januari 30 mwaka 1975 alipostaafu.
Askofu Castor Sekwa aliyeteuliwa Januari 30, mwaka 1975 hadi Juni 4, mwaka 1996 alipofariki.
Askofu Aloysius Balina aliyeteuliwa Agosti 8 mwaka 1997 hadi Novemba 6 mwaka 2012 alipofariki.
Askofu Mteule Liberatus Sangu aliyeteuliwa Februari 2 mwaka 2015.
(CHANZO: Radio Vatican)
No comments:
Post a Comment