Monday, 20 April 2015

MCHUNGAJI MSIGWA NA MKUU WA WILAYA YA IRINGA WASIKILIZA KILIO CHA MBOMIPA



Mchungaji Peter Msigwa akipokea kilio cha wanajumuiya hao, kushoto kwake ni Diwani wa Idodi, Onesmo Mtatifikolo



wanajumuiya wakimsubiri mkuu wa wilaya ya Iringa, nje ya ofisi yake

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Angelina Mabula

WAZIRI Kivuli wa Malisiali na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Angelina Mabula wamepokea kilio cha vijiji vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Mali Hai Tarafa ya Idodi na Pawaga (Mbomipa) na kuahidi kukifanyia kazi katika kipindi kifupi kijacho.


Wakati Mchungaji Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini (Chadema) ameahidi kupeleka kilio hicho katika bunge la Mei, mwaka huu, Mkuu wa wilaya ameahidi kuyafanyia kazi baadhi ya malalamiko ya wanajumuiya hao dhidi ya viongozi wao na mmoja kati ya wawekezaji wake, Kilombero North Safaris katika kipindi cha siku saba kuanzia jumatatu.(BONGOLEAKS)


Mbomipa ni eneo la hifadhi ya jamii ya wanyamapori linalopakana na hifadhi ya Taifa ya Ruaha, wilayani Iringa mkoani Iringa lenye wanyamapori wengi wanaoingia na kutoka katika hifadhi hiyo ya Taifa.


Katika eneo hilo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 776.4, Mbomipa imeingia mikataba na wawekezaji mbalimbali kwa ajili ya kujenga hoteli na kambi za kitalii, kufanya utalii wa picha na uwindaji wa wanyamapori kwa kuzingatia sheria ya wanyamapori.


Kwa kupitia wawekezaji hao, kila mwaka Mbomipa imekuwa ikipata ada na mapato mengine yatokanayo na uwekezaji huo, fedha wanazozitumia kwa maendeleo ya vijiji 21 wanachama na shughuli mbalimbali za jumuiya ikiwemo ulinzi wa eneo hilo.


Baadhi ya wajumbe wa jumuiya hiyo, walisafiri kutoka katika vijiji hivyo Alhamisi iliyopita hadi Iringa mjini na kufanikiwa kukutana na Mchungaji Msigwa Ijumaa, huku Mkuu wa wilaya wakikutana naye Jumamosi.


Kupitia kwa Diwani wa Kata ya Idodi, Onesmo Mtatifikolo, wana jumuiya hao wanamtuhumu mwenyekiti wao, Phillip Mkumbata kushindwa kuendesha jumuiya hiyo kwa kuzingatia katiba, kanuni na taratibu zingine za jumuiya, na kushindwa kuitisha mikutano ya kikatiba kwa miaka miwili.


Tuhuma nyingine waliyotoa kwa mwenyekiti huyo ni kubadili matumizi ya moja ya eneo la uwekezaji la jumuiya hiyo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa kambi na hoteli za kitalii na kuwa la uwindaji wanyamapori bila ridhaa ya mkutano mkuu.


Eneo hilo la kanda ya uwekezaji ya Lunda ambalo sehemu yake (kilomita mbili za mraba) lilitolewa kwa Kampuni ya Kilombero North Safaris kwa ajili ya ujenzi wa kambi na hoteli za kitalii, linadaiwa kutolewa kwa miaka kumi kwa kampuni hiyo bila kutangazwa ili kuruhusu ushindani kama sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009 inavyotaka.


Vile vile wanajumuiya hao wanamtuhumu mwenyekiti wao kushindwa kusimamia makusanyo na kutoa gawio kwa vijiji kila mwaka kama taratibu zinavyotaka huku akishindwa kukusanya mapato ya zaidi ya Sh Milioni 200 kutoka kwa mmoja kati ya wawekezaji waliopo katika hilo.


Akipokea malalamiko hayo Mchungaji Msigwa alisema; “nimesikia kilio chenu, katika hili niwahakikishie tupo pamoja, tutapambana pamoja ili mpate haki zenu; mbali ya kuyapeleka bungeni, nitayafikisha pia malalamiko yenu kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.”


Akizungumzia uwindaji katika eneo hilo, Mchungaji Msigwa alisema ni lazima ufuate taratibu, kanuni na sheria ya wanyamapori na kama mwekezaji huyo ameingia mkataba wa kienyeji ajue kabisa hiyo imekula kwake.


Mkuu wa Wilaya alisema katika kipindi cha wiki moja atakutana na bodi ya wadhamini, kupitia katiba ya Mbomipa na amemtaka mkaguzi wa ndani wa halmashauri ya wilaya ya Iringa kufanya ukaguzi wa mapato na matumizi ya jumuiya hiyo.


“Kwahiyo namtaka mkaguzi wa ndani aanze kazi hiyo Jumatatu, afanye ukaguzi ya mapato na matumizi ya kila mwaka ili nipate picha halisi ya fedha za jumuiya na matumizi yake,” Mabula alisema.


Kuhusu mkataba wa uwindaji unaodaiwa kutolewa kwa mwekezaji huyo, Mabula alisema ni jambo lisilokubalika kwa kuwa halina ridhaa ya wanajumuiya na linavunja katiba ya Mbomipa na sheria za nchi.


“Kwahiyo nataka ndani ya wiki moja mambo hayo yote yawe yamefanyiwa kazi na baada ya hapo sasa mkutano mkuu uitishwe kwa ajili ya kupeana taarifa na kuchukua maamuzi mengine,” alisema.


Akizijibu tuhuma hizo, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Phillip Mkubata alisema vyovyote itakavyokuwa yupo tayari kwa maamuzi yoyote yatakayofanywa na jumuiya hiyo kama itabainika amefanya makosa lakini akasihi tuhuma hizo zimalizwe katika meza ya majadiliano.


Mkumbata alisema yeye pamoja na kamati yake wanayo majibu watakayoyatoa endapo wataitwa na kutakiwa kufanya hivyo.


“Kwa kifupi kuhusu tuhuma hizo ni kwamba tunashindwa kufanya mikutano kwasababu ya hali mbaya ya kifedha inayotokana na mapato ya jumuiya kupungua kwasababu ya kutolipwa ada ya uwekezaji na mmoja wa wawekezaji kwasababu tuna mgogoro naye. Jumuiya yote inajua kwamba tuna mgogoro na kampuni ya Kilombero North Safaris na kwa miaka kadhaa sasa hajatulipa ada yetu na mapato mengine” alisema.


Kuhusu kubadili matumizi kanda ya uwekezaji ya Lunda, Mkumbata alisema; “Ni kweli tulikwenda Dar es Salaam, tukakutana na mwekezaji huyo na tukafika wizarani. Jambo hili halijakamilika, mchakato wake haujakamilika, kwahiyo watu wasizungumze jambo wasilo na uhakika nalo,”

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...