Tuesday, 5 May 2015

CCM WAZOA WANACHAMA WAPYA 200 MKWAWA



KATIBU wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Sixtus Mapunda amewataka vijana wa chama hicho kuwa wa kwanza kulinda amani hata pale chama chao kinapotukanwa bila sababu na wapinzani wao katika mikutano yao ya kisiasa.

Mapunda aliyasema hayo juzi kwenye mkutano wake wa hadhara alioufanya nje ya Chuo Kikuu cha Mkwawa, mjini Iringa katika ziara yake ya siku tano aliyofanya mkoani Iringa kukiimarisha chama hicho.

Kabla ya mkutano huo, Mapunda alifanya mikutano na uzinduaji wa matawi mapya ya UVCCM katika wilaya za Kilolo, Iringa Vijijini na Manispaa ya Iringa.

“Mkisikia wapinzani wanafanya mkutano wao, na mkahamasika kwenda kuwasikiliza, nendeni na kawasikilizeni kwa adabu, wakiwakwaza kwa maneno yao rudini nyumbani mkapumzike,” alisema.

Mapunda alisema watanzania wanapaswa kuendelea kuiamini CCM kwasababu ina dereva anayejua kazi yake tofauti na wale wanaotaka kujifunza kazi hiyo wakiwa Ikulu.

Aliwataka wananchi wa manispaa ya Iringa na vitongoji vyake kujiandikisha kwa wingi katika daftari la kudumu la wapiga kura ili watumie haki yao kutimiza wajibu wao wa kuirudisha tena CCM madarakani.

“Msema kweli ni mpenzi wa Mungu, mwaka 2010 mlitupa dhamana ya kuendelea kuongoza nchi hii kwa miaka mitano mingine, kuna maeneo mlitupa mamlaka kamili, na kuna maeneo kwa makusudi mlitupatia wapinzani,” alisema.

Alisema jimbo la Iringa Mjini ni moja ya eneo ambalo wananchi wa manispaa ya Iringa waliamua kumchagua mbunge toka upinzani huku kura za Rais na madiwani zikitolewa kwa wingi kwa CCM.

“Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, tusaidieni kututolea gunzi kwenye tochi ya CCM, gunzi hilo ni shiiida, linapinga bajeti, linapinga ujenzi wa maabara, linapinga katiba mpya, barabara na mengi yanayohusu maendeleo ya watu wa Iringa na Taifa,” alisema.

Alisema jambo kubwa linalosikitisha katika siasa za nchi ni kwamba wanaoamua kuwa wa kwanza kujipofusha ndio wale waliopata bahati ya kuona jua.

“Wanaokubali kujipofusha ni wale waliomaliza kidato cha nne, cha sita na vyuo vikuu. Siko tayari kuamini mwanafunzi wa chuo kikuu anawezaje kukubali kudanganywa, naloliona ni kama wanajidanganya wenyewe,” alisema.

Alisema baadhi ya wanafunzi hao wamekuwa vinara wa kushangilia na kupiga makofi wanapowasikia wapinzani wakiisema serikali ya CCM kwamba haijafanya kitu.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...