Thursday, 11 June 2015

ADAI FIDIA KWA MWAJIRI BAADA YA KUKATWA VIDOLE VINNE AKIWA KAZINI!


Aliyekuwa mfanyakazi wa Kiwanda cha FibreBoards 2000 Ltd Arusha, Tawi la Mafinga Jane Paschal Nziku (19) akionesha mkono wake wa kulia uliokatwa vidole vinne na kubakia na kidole gumba. Aliyemshika mkono ni kaka yake Omary Mbilinyi. (PICHA NA FRIDAY SIMBAYA)

KIWANDA cha Fibre Boards 2000 Ltd cha Arusha, Tawi la Mafinga kunadaiwa fidia na mfanyakazi wake ambaye alipata ajali akiwa kazini ambapo katika ajali hiyo alipoteza vidole vinne vya mkono wa kulia na kubakia na kidole gumba.

Mfanyakazi huyo, Jane Paschal Nziku (19) pichani mwenye elimu ya kidato cha nne na mkazi wa Mafinga alipata ajali ya kazini tarehe 24.12.2014 katika kiwanda kinachomilikiwa na Darshan Singh kilichopo mjini Mafinga wilayani Mufindi, mkoani Iringa.


Kiwanda hicho ambacho makao makuu yake hapo Arusha, kipo maeneo ya Kinyanambo C, Mafinga kinatengeneza singebodi (ceiling boards), kinadaiwa kutomlipa mfanyakazi wake huyo aliyekatwa vidole vyake vinne na mashine katika mkono wa kulia na kubakia na kidole gumba.

Kwa mujibu wa Mwanasheria wa Makesi ya wafanyakazi kuanzia Usuruwishi (CMA) hadi Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, Ignas Charaji alisema kuwa kisheria mfanyakazi akiumia akiwa kazini mwajiri anatakiwa kutoa taarifa ya ajali ndani ya siku saba (7) tokea ajali itokee katika ofisi ya kazi ya sehemu hiyo.

“Kwa mujibu wa sheria iitwayo Notification Ordinance ya 1952 na marekebisho yake ya 2008 iitwayo The Workers Compensation Act No. 20 of 2008, ambaye inamtaka mwajiri kutoa taarifa ya ajali ndani ya siku saba tokea ajali itokee ya mfanayakazi,” alifafanua mwanasheria huyo.

Charaji ambaye pia ni Katibu Mkuu wa mikoa ya Iringa na Njombe wa Chama cha kutetea masilahi za wafanyakzi viwandani (TUICO) alisema kwa bahati mbaya mwajiri huyu hakutoa taarifa, isipokuwa mfanyakzi mwenyewe ndiye aliyelazimika kwenda kumuona afisa wa kazi.
Alisema kuwa afisa wa kazi tarehe 29/05/2015 alimjazia mfanyakazi huyo fomu LD1 335 na fomu nyingine kutoka kwa dakatri aliyetimbu mfanyakazi ambaye anajua aliumia kiasi cha asilimia gani katika ajali.

Mfanyakazi huyo alipelekwa kutibiwa katika zahanati ya mtu binafsi ya Tumaini Dispensary na hatimaye kuhamishia katika hospitali ya Wilaya ya Mafinga.

Nipashe jana ilifunga safari kwenda kuonana na Mkurugenzi wa Kiwanda hicho, Darshan Singh ilikupata ukweli wa mambo na kubaini kwamba mfanyakazi huyu (Jane Paschal Nziku) hayupo kazini na bado hajalipwa fidia (compensation) ya kuumia kazini.

Mkurugenzi huyu alikanusha madai hayo ya kumfukuza kazi mfanyakazi huyo na kusema kuwa hajafukuzwa kazi na anatakiwa kurudi kazini baada ya kupona, lakini hadi sasa hajarudi kazini.

Alisema kuwa kampuni yake iligharamia matibabu yake baada ya kuumia kazini na wanasubiri kujua fidia ni kiasi gani anatakiwa kulipwa kutoka kwa mamlaka husika.

“Madai ya malipo kwa ajili ya fidia yamepelekwa Fibre Boards makao makuu Arusha, hivyo mfanyakazi huyo atalipwa fidia yake,” alisema mkurugenzi huyo.

Kwa upande wake, Afisa wa Kazi Mafinga  akiongea na Nipashe kwa njia ya simu amekiri kuwepo kwa taarifa ya aliyekuwa mfanyakazi Jane Nziku ambaye alikuwa anafanyakazi katika kampuni ya Fibre Boards, Tawi la Mafinga.

Alisema kuwa ofisi yake ilipata taarifa kuhusu kuumia kwa mfanyakazi huyo na mkushauri mkurugenzi wa kampuni hiyo ya FiberBoards kutomfukuza kazi mfanyakazi huyo kutokana na ulemavu wake.

Alieleza kuwa alimwambia Jane Nziku kuwa wakati akiendela na matibabu na baada ya kupona aendelee kwenda kazini na nikamwamuru pia mkrugenzi asimfukuze kazi kwa sababu ya ulemavu huo.

“Baada ya maagizo haya ya pande zote mbili hadi sasa J. Nziku hajafika kazini na nilipozungumza naye kwa simu kuwa kwa nini haendi kazini alinijibu kuwa anasubiri mkurugenzi wake (D.Singh) ampigie simu kumtaka aende kazini,” alisema afisa wa kazi huyo.

Aliongeza kuwa si kweli kuwa mwajiri amemfukuza kazi. Hata hivyo kisheria kama amefukuzwa kazi na mwajiri,  anatakiwa amufahamishe mteja wake huyu apeleke shauri lake hilo kwenye baraza la usuruhisho (CMA) wakati taarifa za kisheria zinachukuliwa kutekeleza malipo ya fidia ya kuumia kazini.

Naye, Mkurugenzi wa Kiwanda hicho cha Fibre Boards, Darshan Singh alikiri kutomlipa fidia na kukanusha kwamba hajamfukuza kazi mfanyakazi huyo na kukiri kwamba mpaka sasa kiwanda hicho hakijamlipa fidia ya kuumia kazini.

“Ndio Jane Nziku alikuwa mfanyakazi wetu hapa kiwandani na madai yake ya malipo yamepelekwa fibre boards makao makuu Arusha,” alisema.

Hata hivyo, mkurugenzi huyo amekanusha kuwepo kwa madai kwamba kampuni yake imemfukuza kazi mfanyakazi huyo.


“Sisi kama kampuni tulisimamia matibabu yake yote na na tunaendelea kumhudumia na tunasubiri maamuzi ya kulipa fidia kutoka mamlaka husika,” alisema Singh.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...