Wednesday, 10 June 2015

LIGI YA UJIRANI MWEMA SAOHILL YAANZA KUTIMUA VUMBI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mahmood Mgimwa ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini akifungua mashindano ya Ligi ya  Ujirani Mwema yalioandaliwa kwa udhamini wa Shamba la miti Sao Hill mjini Mafinga wilayani Mufindi, mkoani Iringa jana. walioketi kutoka kushoto ni Meneja wa Shamba la miti Sao Hill Salehe Beleko na Mwenyekiti wa CCM (W) Mufindi ambaye pia Diwani wa Kata ya Makungu Yohanes Cosmas Kaguo

Meneja wa Shamba la miti Sao Hill, Salehe Beleko (kushoto) akisalimia na golikipa wa Timu ya Ihalimba Vijijini FC kabla ya mechi kuanza.


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mahmood Mgimwa (kulia) ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini akiwasili katika viwanja vya Ihefu kwa ajili ya ufunguzi wa Ligi ya Ujirani Mwema ya Sao Hill jana.




SAOHILL imeanzisha mashindano ya Ligi ya Ujirani Mwema kwa kushirikisha vijiji vinavyozunguka shamba hilo ili kulinda na kutunza rasilimali za misitu na nyuki.

Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo, Said Aboubakar alisema kuwa Ligi ya Ujirani Mwema itashirikisha timu nane ambazo ni Ihefu Misitu, Ihalimba Mseto, Ihefu Mseto, Mgololo Misitu, Mgololo Mseto, Irindi Misitu na Irindi Mseto zilizogawanywa katika makundi A na B.

Michuano ya Soka kwa wanaume ya Ujirani Mwema mechi ya ufunguzi, Timu ya Ihefu Misitu ilianza vyema baada ya kuibamiza goli 3-2 Timu ya Ihalimba Mseto, Kundi A Ligi ya Ujirani Mwema SaoHill yanayoendelea kufanyika Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa.

Michuano hiyo iliyoanza kutimua vumbi Jumamosi wiki iliyopita na ina fadhiliwa na shamba la miti Sao Hill kwa shirikiana na Chama cha soka Mufindi (MUDIFA).

Said alisema kuwa timu nne zimeundwa na wafanyakazi wa misitu ya SaoHill toka tarafa nne (divisions) za shamba na timu zingine nne kutoka vijiji vinavyozunguka shamba ambalo. 

Katika mchezo huo wa ufunguzi kati ya timu za Ihefu Misitu na Ihalimba Mseto, timu hizo zilikamiana vilivyo katika kipindi cha kwanza, lakini hakukuwa na timu iliyotikisa nyavu za mwenzake mpaka mapumziko.

Kilipoanza kipindi cha pili timu hizo zilianza kwa kasi kubwa ambapo kila mmoja alifanya mashambulizi ya nguvu na timu ya Ihefu ilipata goli la kwanza katika dakika 20 kipindi cha pili kupitia mshambuliaji wake Shadrick Nyinga jezi namba 19 mgongoni.

Timu ya Ihalimba Mseto nayo haikubweteka ikaanza mashambulizi na kusawazisha goli kwa kupitika winga wake Romanus Mwagala jezi nambari mbili mgongoni baada ya kuunganisha shuti ya moja kwa moja hadi golini.

Mfungaji mwengine kutoka timu ya Ihefu Misitu ni Nestor Sanga jezi namba nane mgogoni aliyefunga goli la pili na tatu.

Hata hivyo, timu ya Ihalimba ilipata penati baada ya beki wa Ihefu Misitu kumfanyia madhambi fowadi wa Ihalimba Mseto katika eneo la hatari na kufanikiwa kupata goli la pili, iliyopigwa na Lufunyo mwenye jezi namba 14 mgongoni.

Mechi mwingine katika Kundi A iliyochezwa Jumapili ni Ihefu Mseto ilioibuka na ushindi goli 3-2 dhidi ya Ihalimba Misitu. 

Wafungajikatika timu ya Ihefu Mseto ni Barnaba aliyefunga goli mbili na James alifunga goli moja na kwa upande wa Ihalimba Misitu wafungaji ni Siliri na Longo.

Kauli mbiu ya ligi hii ni, UTUNZAJI WA RASILIMALI ZA MISITU NA NYUKI NI JUKUMU LETU SOTE.

Kwa upande wake, Meneja wa Shamba la Miti la SaoHill, Salehe Beleko alisema lengo la mashindano hayo ni kujenga mahusiano mazuri baina ya vijiji vinavyozunguka mashamba ya SaoHili ili kushirikiana kulinda na kutunza rasilimali za misitu na nyuki. 

Aliongeza kuwa shamba hilo limegawanyika katika tarafa nne ambazo ni Ihefu, Ihalimba, Mgololo na Irindi ili kuleta ufanisi katika usimamizi.

Alisema mashindano hayo yatafikia kilele, yaani fainali siku ya nane nane mwaka huu ambapo itaundwa timu moja la shamba ya SaoHill. 

Naye, mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mahmood Mgimwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini alisema kuwa mashindano hayo yakitumika vyema yatasaidia kuibua vipaji mbalimbali vijijini na kutengeza ajira kwa vijana.

Michuano hayo yanashirikisha pia michezo mingine kama vile; mpira wa wavu (volleyball), mpira wa pete (netball) na mchezo wa drafti ili kupanua wigo mashindano na hatimaye kuweza kuibua vipaji mbalimbali.

Katika upande wa zawadi, naibu waziri huyo alisema kuwa mshindi wa kwanza katika upande wa soko atapatiwa shilingi milioni moja (1m/-), mshindi wa pili laki sita na wa tatu atapata shilnigi laki nne.

Kwa mpira wa pete mshindi wa kwanza atapata shilingi laki tano na mshindi wa pili atazoa laki tatu lakini hapata kuwepo na mshindi wa tatu. Mpira wa wavu mshindi wa kwanza atapewa shilingi laki tano na wa pili laki tatu.

Kwa upande wa mchezo wa drafti mshindi wa kwanza atapata laki tatu, wa pili laki moja na nusu na mshindi wa tatu shilingi 50,000/-.

Aidha, timu yenye nidhamu itazawadiwa laki mbili, mchezaji bora ataondoka na laki moja, mfungaji bora atapata shilingi laki moja na kipa bora naye atajipatia shilingi laki moja.


No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...