Saturday, 13 June 2015

Membe azoa wadhamini Iringa


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amezoa wadhamini 380 mjini Iringa.

Wadhamini hao kutoka wilaya zote tatu za mkoa wa Iringa walianza kukusanyika katika ukumbi wa chama hicho mjini Iringa majira ya saa 7 mchana hadi saa 4 usiku, kumsubiri Membe akitokea mkoani Njombe.

Akiwashukuru wadhamini hao, Membe alisema; “miongoni mwa ngome zangu kubwa sana za kisiasa nchini ni mkoa wa Iringa. Katika Uchaguzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa, wajumbe wa mkoa wa Iringa walinipa kura zao zote.”

Alisema CCM ina utaratibu mzuri wa kuchuja na kupitisha viongozi wa kitaifa na kwa ukubwa wake ndio sababu kuna wagombea wengi wa urais wanaojitokeza kuwania nafasi hiyo.

“Watanzania msikiache chama hichi, tuna marafiki duniani kote, ni chama ambacho kimesaidia kupatikana kwa Uhuru kwa nchi zaidi ya nane barani Afrika.

Akizungumzia nafasi anayoiwania, Membe alisema; “urais haujaribiwi wala sio kazi ya kukurupuka, ni lazima uwe umejipanga na wenzako waamini kwamba wewe unaweza kugombea na lazima uwe na hekima na busara.”

Huku hotuba yake ikikatizwa mara kwa mara na shangwe na vifijo toka kwa wadhamini hao, Membe alisema uzoefu wa uongozi alionao ndani na nje ya nchi umemsukuma kuomba nafasi hiyo.

“Nikijaaliwa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, angalieni timu nitakayojenga, baraza la mawaziri nitakalochonga, litakuwa na vijana, wanawake na wazee kwasababu wazee ni dawa,” alisema.

Alisema anataka kuiondoa nchi hapa ilipo na kuipeleka kwenye uchumi wa viwanda vitakavyotegemea kilimo na akawaponda wagombea wasiojua nini wanatakiwa kufanya endapo watachaguliwa kwa kisingizio kwamba wanategemea vipaumbele vyao vipo kwenye Ilani.

Aidha, alisema akichaguliwa kuwa rais atahakikisha atajenga uchumi wa viwanda ili mazao ya kilimo yaweze kusindikwa nchini.

Alisema kuwa kwa muda mrefu nchini inasifika kuwa namba moja kwa kuzalisha malighafi ambayo inanufaisha nchi zingine ambazo zinapata faida kubwa kuliko sisi.

Alisema akiwa rais atahakikisha anafufua viwanda vikiwemo vya Iringa ili viweze kuajiri watu wengi na hatimaye kupunguza umaskini.

Alisema kuwa mgombea yeyote anayetumia nguvu ya fedha kuwanunua wananchi ataona haya kuwakemea wenzake wanaopatikana na hatia ya rushwa.

Mgombea mwingine aliyefika mkoani hapa ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli (CCM) aliyepokelewa na wanachama na mashabiki wengi na kujizolea wadhamini 680 waliotia saini kwenye fomu yake na hatimaye kuelekea mikoa ya Njombe na Mbeya.


Aliwaomba wananchi wa Iringa wampe ridhaa ya kuteuliwa na chama chake ili aweze kupeperusha bendera ya Jumhuri ya Muungano wa Tanzania. 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...