Na Friday Simbaya, Mufindi
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mufindi, Saada Malunde amesema makusanyo ya mapato yameongezeka kutoka zaidi ya shilingi bilioni 2,192,830,130/- mwaka 2010/2011 na kufikia zaidi ya shilingi bilioni 4,146,583,199/- mwaka 2014/2015.
Mkurugenzi Mtendaji huyo alitoa taarifa hiyo hivi karibuni baada ya kuvunjwa rasmi Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi lililodumu kwa muda wa miaka mitano na kuoanisha mafanikio kadhaa yaliyofikiwa tangu kuundwa kwake mnamo mwaka 2010.
Akisoma taarifa ya mafanikio ya halmashauri hiyo, kwenye kikao maaluum cha kuvunjwa kwa baraza, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mufindi, Saada Malunde alitaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, kuongezeka kwa makusanyo ya mapato kutoka zaidi ya shilingi bilioni 2,192, 830,130/- mwaka 2010/2011 na kufikia zaidi ya shilingi bilioni 4,146,583,199/- mwaka 2014/2015.
Malunde alisema kuwa lengo la halmashauri ya wilaya katika shule za sekondari ni kuhakikisha wanafunzi wote wanaojiunga na kidato cha kwanza wanahitimu na kufaulu kidato cha nne.
“Tumepata mafanikio katika mwaka wa 2014/2015 kwani idadi ya shule za sekondari imeongezeka toka shule 18 hadi kufikia shule 57 mwaka 2015, idadi ya wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza imeongezeka kutoka wanafunzi 2,880 mwaka 2010 hadi kufikia 4,926 mwaka 2015. Pia idadi ya walimu wa shule za sekondari imeongezeka kutoka walimu 81 mwaka 2010 hadi kufikia walimu 887 wakiwemo wanaume 586 na wanawake 301 mwaka 2015, ” alisema Malunde.
Alisema kuwa halmashauri ya wilaya imeunganishwa na grid ya Taifa na kuwa na uhakika wa umeme unaotokana na nguvu ya maji na mwaka wa fedha 2014/2015.
Na kuongeza kuwa vijiji 13 na kitongoji kimoja kimepata huduma ya umeme unaozalishwa na kampuni ya Mwenga “Hydro Power” katika Kata ya Ihanu.
Aidha, mradi huo una mpango wa kuongeza huduma ya umeme katika vijiji 18 vya Tarafa ya Kibengu.
“Tunao mradi unaosimamiwa na wakala wa umeme vijijini (REA) ameanza kusambaza na kusimika nguzo kuanzia hapa Mafinga hadi kata ya Sadani, Isalavanu na Igombavanu na kuanzia Makambako hadi Malangali, Ihowanza kupitia Kata ya Mbaramaziwa kwa hiyo vijiji vitakavyopata umeme vitaongezeka kwenye Tarafa ya Sadani na Malangali mara mradi utapokamilika,” Malunde aliongeza.
Mkurugenzi huyo mtendaji aliyataja mafanikio mengine kuwa ni uwepo wa mtandao mzuri wa barabara unaofikia kilometa 1,558.3 sanjari na kufanikiwa kutengeneza barabara kwa kiwango cha lami kwa umbali wa kilometa kumi (10) katika Mji wa Mafinga na kuboresha upatikanaji wa maji.
Alisema kuwa hivi sasa idadi ya watu wanaopata maji safi na salama imeongezeka kutoka asilimia 40 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 64 mwaka 2014/2015 kwa wa kazi wa mjini, wakati vijijini ongezeko imepanda kutoka asilimia 56 hadi kufikia asilimia 62.3.
Awali akitoa salamu za Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa (RAS), Wamoja Ayubu, amewataka watumishi chini ya mkurugenzi wa halmshauri hiyo, kuzingatia maelekezo ya TAMISEMI wakati wa kufanya maamuzi hususan yanayohusiana na fedha kwa kipindi chote ambacho halmashauri itakuwa chini ya uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment