Katibu wa CCM wa Manispaa ya Iringa, Elisha Mwampashi (kulia) akiongea na wanahabari kuhusu mchakato upigajikura za maoni kwa waombaji 13 waliojitokeza kutafuta ridhaa ya chama hicho ili wapeperushe bendera ya ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini jana. Kushoto ni Mweneyekiti wa CCM wa Manispaa ya Iringa, Abeid Kiponza.
WANACHAMA zaidi ya 18, 000 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Iringa Mjini leo wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi wao kuwapigia kura waombaji 13 waliojitokeza kutafuta ridhaa ya chama hicho ili wapeperushe bendera ya ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini.
Kura hizo za maoni zinafanyika baada ya wagombea hao kutumia siku 12 kuzunguka katika matawi 81 ya chama hicho kunadi sera zao ikiwa ni azma ya kila mgombea kutafuta kuungwa mkono ili achaguliwe kuwania ubunge katika jimbo hilo.
Ama zao ama zangu ya kura hizo inatarajiwa kujitokeza kwa wagombea hao ambao ni pamoja na Dk Augustino Maiga, Frederick Mwakalebela, Jesca Msambatavangu, Mahamudu Madenge, Nuru Hepautwa, Dk Yahaya Msigwa, Michael Mlowe, Addo Mwasongwe, Aidan Kiponda, Fales Kibasa, Frank Kibiki na Peter Mwanilwa.
Akizungumza na wanahabari hii leo, Katibu wa CCM wa Manispaa ya Iringa, Elisha Mwampashi alisema vituo 88 vitatumika kupigia kura hizo za maoni na matokeo ya kila kituo yatatangazwa vituoni ili kuepuka hofu ya kuwepo kwa mizengwe.
“Kila mgombea ameteua wakala wake ambao pamoja na wasimamizi wa kila kituo leo tumewapa mafunzo elekezi ya namna ya kuendesha kura hizo za maoni,” alisema.
Alisema vifaa kwa ajili ya kura hizo za maoni vimekamilika na kwamba vituo vyote vitafunguliwa kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 10 jioni,” alisema.
Alisema wanachama watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale watakaokwenda katika vituo hivyo wakiwa na kadi zao za uanachama na kitambulisho cha mpiga kura.
“Tunahitaji pia kitambulisho cha mpiga sio kwa maana ya kukichukua, ni kwa maana ya kujiridhisha kwamba mwanachama anayeshiriki kuchagua mgombea ubunge atapiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25,” alisema.
Alisema matokeo ya jumla ya kura hizo za maoni yatatangazwa rasmi Jumapili asubuhi katika zoezi litakaloshirikisha waalikwa mbalimbali wakiwemo wazee wastaafu wa chama hicho, makada mashuhuri, viongozi wa taasisi mbalimbali za chama na waalikwa wengine.
Alisema kuibuka mshindi katika kura hizo hakumuhalalishii mgombea kwamba ameteuliwa na CCM kupeperusha bendera ya chama hicho mpaka pale vikao halali vya uteuzi vitakapothibitisha kwamba ushindi wake haukuwa na hila yoyote.
Kwa miaka mitano iliyopita Jimbo la Iringa Mjini limekuwa likiongozwa na Mchungaji Peter Msigwa aliyechaguliwa katika uchaguzi mkuu wa 2010 kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
No comments:
Post a Comment