Kamishna Msaidizi wa Polisi toka ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Hussein Kashindye amesema kati ya mwaka 2006 na 2015 kulikuwa na matukio 56 yanayohusisha walemavu wa ngozi kuuawa au kujeruhiwa.
“Katika matukio hayo, 43 yalihusisha watu kuuawa na 13 kujeruhiwa. Katika kipindi hicho watu 12 walihukumiwa kunyongwa kwa makosa hayo na kesi nyingine 12 zipo kwenye hatua ya upelelezo huku nyingine zikitupiliwa mbali baada ya kukosekana kwa ushahidi” alisema.
Akiwasihi watanzania wote kushiriki katika mkakati wa kuwanusuru walemavu hao, Kashindye alisema suala la kuwalinda albino linatakiwa kuzingatia polisi jamii kwa kuanzia ngazi ya familia, kata, tarafa wilaya na mkoa.
Hivi karibuni Chama cha Wataalamu wa Ustawi wa Jamii (TASWO) kimefanya kongamano kubwa mjini Iringa lililowajengea uwezo wataalamu wa ustawi wa jamii nchini katika utetezi, ulinzi wa haki na ustawi wa watu wenye ulemavu hususani walemavu wenye ualbino.
Kauli Mbiu ya kongamano hilo lililofunguliwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu ni “utetezi, ulinzi wa haki na ustawi wa watu wenye ulemavu hasa katika kuthibiti mauaji ya watu wenye ualbino na maambukizi ya virusi vya Ukimwi na Ukimwi.”
Kaimu Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Radikira Mushi alisema; “ni fikra potofu kuamini viungo vya watu wenye ualbino vinawawezesha kubadili maisha kwa kuwaondoa katika wimbo la umasikini.”
Naye, Katibu Mtendaji wa TASWO, Nicolaus Mshana alisema mbali na mauaji, walemavu hao wana changamoto za umasikini na maambukizi ya VVU na Ukimwi hali inayosababishwa na mazingira wanayoishi, aina yao ya uelemavu, uelewa mdogo wa VVU na Ukimwi na uwezo wa wataalamu katika kutoa huduma kwa kundi hilo hasa kwa wasioona vizuri.
Kwa upande wake mmoja wa viongozi wa chama cha walemavu wa ngozi mkoani Iringa, Hellen Machibya aliitaka serikali kuwapa kipaumbele walemavu wanapohitaji kupata huduma mbalimbali zinazowahusu.
Akizungumzia jinsi wanavyopata kwa shida huduma za afya, Machibya alisema wamekuwa wakitibiwa kama wagonjwa wengine pamoja na kueleweka kwa tatizo lao la ngozi.
Mbali na wawakilishi wa TASWO, kongamano hilo lililofanyika mjini hapa, lilishirikisha maafisa ustawi wa jamii, polisi, mashirika ya haki za binadamu, walemavu, Tacaids, ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali, shirika la JSI/CHSS na shirika la kitaalamu la NASW la Marekani.
No comments:
Post a Comment