Sunday, 18 October 2015

Masenza: Orodha ya vituo imepungua toka 1,641 hadi 1,601


Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza amesema orodha ya vituo imepungua kutoka 1,641 hadi kufikia 1,601, sawa sawa na vituo 40 vilivyopungua, Nipashe imedhibitisha.

Alisema kuwa awali Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitoa orodha ya vituo 1,641 vitakavyotumika katika zoezi la upigaji kura kwa Mkoa wa Iringa kwa Halmashauri zote tano (5). 

Masenza alisema hayo wiki iliyopita wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu mwenendo wa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani. 

Alisema kuwa idadi hiyo imepungua kufikia vituo 1,601 baada ya uhakiki wa wapiga kura kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaoendelea kufanywa na Wasimamizi wa Uchaguzi.

Alisema kuwa halmashauri zote zimepokea vifaa kama masanduku, mifuniko, Tshirts, kofia, Vituturi, na fomu mbalimbali kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu. 

Aidha, alisema kuwa wasimamizi wanaendelea kufanya tathmini ili kujiridhisha endapo vifaa vilivyopokelewa vinakidhi mahitaji.

“Tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetoa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Halmashauri zote. Kazi inayoendelea hivi sasa ni uhakiki wa idadi ya wapiga kura kwa kila kituo,” alisema Masenza.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza alisema kuwa mkoa wake umejipanga vizuri kuhakikisha amani na usalama kwa kipindi chote cha kampeni za Uchaguzi na wakati wa zoezi la kupiga kura vyote vinafanyika vizuri kwa mujibu wa ratiba na kwa kuzingatia sheria za nchi ili Wananchi waendelee kuwa salama na kutekeleza majukumu yao. 

Alisema kuwa katika kuhakikisha mkoa unakuwa na utulivu kwa kipindi chote, amekutana na makundi mbalimbali kujadili suala la amani kuelekea Uchaguzi Mkuu. 

Makundi hayo ni viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa madhehebu ya dini, wazee na watu wenye ushawishi katika jamii na waandishi wa habari. 

Lengo ni kupata maoni na ushauri wa jinsi ya kufanikisha Uchaguzi Mkuu kwa amani na utulivu.

“Napenda kuchukua nafasi hii kuwathibitishia Wananchi wa Mkoa wa Irirnga kuwa, ulinzi utakuwepo wa kutosha katika kipindi chote cha kampeni na siku ya kupiga kura tarehe 25/10/2015,” alisema. 

Alisema kuwa Jeshi la Polisi limejipanga vizuri kuwalinda wananchi wote, hivyo, rai yake kwa wananchi ni kuwa jitokezeni kwa wingi siku ya kupiga kura mapema na baada ya kupiga kura rudini kwenye maeneo yenu kuendelea na shughuli nyingine. 

“Wananchi wasibaki kwenye vituo vya kupigia kura baada ya kupiga kura”.

Napenda kutoa rai kwa wananchi wote wa Mkoa wa Iringa kufahamu na kukubaliana kuwa yapo maisha na yataendelea kuwepo hata baada ya Uchaguzi Mkuu hapo tarehe 25 Oktoba, 2015. 

Hivyo, kila mmoja wetu lazima atimize wajibu wake katika kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kuwepo katika kipindi hiki chote ili tumalize zoezi hili tukiwa wamoja na wenye mshikamano mkubwa.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...