Monday, 1 February 2016

Mwenyekiti Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Iringa Mhekwa Azindua Maadhimisho ya Miaka 39 ya CCM

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Iringa, Ephram Mhekwa akihutubia wananchi wa Kijiji cha Lulanzi wilayani Kilolo, mkoani Iringa wakati sherehe za uzinduzi wa maadhimisho  kimkoa ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa CCM. (Picha zote na Friday Simbaya)











MAADHIMISHO ya kumbukumbu ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimkoa yamezinduliwa Januari 31, mwaka huu, na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Iringa, Ephraam Mhekwa katika Kijiji cha Lulanza wilayani Kilolo, Mkoa wa Iringa.

Aidha, kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kufanyika mkoani Singida, Februari 6, mwaka huu, na mgeni rasmi atakuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Iringa, Ephraam Mhekwa alisema mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho kimkoa mgeni rasmi atakuwa mlezi wa mkoa ambaye ni waziri mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Tanzania Mzengo Pinda.

Alisema pia kuwa kilele cha maadhimisho hayo kimkoa yatafanyika katika Jimbo la Isimani wakati mwaka jana yalifanyika katika Jimbo la kalenga wilayani Iringa.

Alisema kuwa mambo yanayotakiwa kuzingatiwa katika wiki hiyo ni pamoja na kuingiza wanachama wapya wa CCM na jumuia zake na kufanya shughuli zingine za kuimarisha Chama. 

“Shughuli nyingine inayotakiwa katika wiki ya maadhimisho ni kufanya mikutano ya kuwashukuru wana-CCM na wananchi kwa kuiamini CCM na kuhamasisha wananchi kufanya kazi za maendeleo,” alisema Mhekwa.

Aliongeza kuwa katika maadhimisho hayo yaliyobeba kaulimbiu ya ‘sasa kazi, kujenga nchi na kukijenga Chama’ ni pamoja na kushiriki katika ujenzi wa madarasa, vituo vya afya, zahanati, upandaji miti, uchimbaji wa mitaro ya maji na kufanya usafi wa mazingira.

Alisema kilele cha sherehe hizo zitafanyika Februari 6, mwaka huu, kwa kuwa Februari 5, ambayo ndiyo siku CCM ilianzishwa, itakuwa ni siku ya kazi. 

Pia, alitumia fursa hiyo kuwaomba wana-CCM, wadau na wananchi wengine kwa ujumla, kushiriki kikamilifu maandalizi na wahudhurie kwa wingi sherehe hizo.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Iringa, Ephraam Mhekwa amekabidhi jumla ya kadi 287 kwa wana chama wapya  wakiwemo UVCCM (60), kadi za wanachama (50), UWT (77) na wazazi (100).


Baadhi ya viongozi waliohudhuria maadhimisho ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Jowike Kasunga, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Selemani Mzee, Katibu wa CCM wilaya ya Mufindi Jimson Mhagama, Katibu wa CCM Wilaya ya Kilolo Clemence Mponzi, Katibu wa wazazi mkoa Geofrey Kavinga, Katibu Msaidizi Mkuu  CCM  Mkoa Agnes Kasela, Mchumi wa CCM Mkoa Lazaro Manila na wengine wengi.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...