MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa imewahukumu kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya Sh Milioni 1.5 kila mmoja, dereva Hansi Mwakyoma (28) na tingo wake wake Alex Adam (32) baada ya kukamatwa na kukiri kusafirisha wahamiaji wasio na vibali 83 kutoka nchini Ethiopia ambao pia wamehukumiwa kwenda jela miaka 3 au kulipa faini ya Sh Milioni 1.
Kwa kutumia gari aina ya Scania lenye namba T478 DFE mali ya Frola Mwambenja wa Mbeya, Januari 16, mwaka huu; dereva huyo na tingo wake walikamatwa katika kijiji cha Ruaha Mbuyuni wilayani Kilolo mkoani Iringa, barabara kuu ya Iringa Mbeya wakiwasafirisha watu hao kuelekea Kyela ambako ni mpakani mwa Tanzania na Malawi.
Akitoa hukumu hiyo leo Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Iringa Endrew Scout alisema ameridhika na maelezo yaliyotolea na wakili wa serikali pamoja na vielelezo likiwamo gari lililotumiwa na watuhumiwa hao kusafirisha watu hao kutoka Kongowe Dar es Salaam kuelekea Kyela Mbeya.
Baada ya kusoma hukumu hiyo, baadhi ya raia hao wa Ethiopia waliangua kilio mahakamani hapo na kusababisha watu waliokuwa karibu na jengo hilo kusogea ili kujionea kulikoni.
Mkalimani wa wahamiaji hao ambao hawazungumzi Kingereza wala Kiswahili zaidi ya lugha ya kwao, Emanuel Yeb Mtaltisili ambaye ni mtangazaji wa kituo cha redio ya Ebony FM cha mjini Iringa alisema; “walichokitarajia wahamiaji hao ni kupewa hukumu ya kurudishwa kwao baada ya kukiri kosa hilo.”
Awali akisoma maelezo ya kosa la watuhumiwa hao baada ya watuhumiw a wote kukiri kosa mbele ya mahakama hiyo, Wakili wa Serikali kutoka Idara ya Uhamiaji Godfrey Ngwijo alisema ilikuwa Januri 16 mwaka huu katika eneo la Ruaha Mbuyuni watuhumiwa hao walipokamatwa wakiwa ndani ya gari hilo lenye bodi lililofunikwa wakisafiri kutoka Kongowe Jijini Dar es Salam kwenda Malawi kinyume na sheria ya uhamiaji ya mwaka 2002 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2015.
Alisema katika tarehe isiyojulikana, watuhumiwa 83 raia wa Ephiopia waliingia nchini kwa kutumia kwa njia zisizo halali na kuelekea jijini Dar es Salaam walikoanzia safari yao ya kuelekea Kyela mkoani Mbeya ili waingie nchini Malawi.
Alisema walipofika eneo la Ruaha Mbuyuni walikamatwa na Askari wa kikosi cha Usalama barabarani ambaye aliwataka wafungue mlango wa nyuma ya gari na kukuta kuna watu hao huku baadhi yao wakiwa hoi.
Alidai mara baadaya kukuta watu aliwaamuru kwenda kituo cha Polisi cha Ruaha Mbuyuni ambako dereva na msaidizi wake walikiri kosa wakidai walikubali kuwasafirisha kwa makubaliano ya kupata kiasi fulani cha fedha na kwamba walipoona mzigo mkubwa waliomba waongezwe na kukubaliana na mwenye mzigo kuwa wangeongezewa mara baada ya kufika walikokuwa wanakwenda.
Mara baada ya maelezo hayo ya wakili hakimu aliwataka watuhumiwa wote pamoja na kukiri kosa kuhojiwa kama wanayakubali maelezo hayo ili haki iweze kutendeka na walipoulizwa wakikiri kuwa maelezo yote yaliyotolewa na wakili wa serikali ni ya kweli
No comments:
Post a Comment