Monday, 23 January 2017

ASKOFU MDEGELLA WA KKKT IRINGA AAGWA KWA KUZAWADIWA NYUMBA NA GARI


Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini, Isaya Mengele (kushoto) akimpongeza Askofu Dkt. Owdenburg Mdegella katika ibada maalum iliyofanyika katika usharika wa Kanisa Kuu (Cathedral) Iringa mjini leo. (Picha na Friday Simbaya)







KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa limemzawadia Askofu Dkt. Owdenburg Mdegella aliyemaliza muda wake wa uaskofu nyumba na gari vyenye thamani ya shilingi milioni 123. (123m/-).

Kanisa limeamua kumzawadia nyumba yenye thamani ya shilingi milioni 55/- iliyopo katika mtaa wa Kihesa-Kilolo Manispaa ya Iringa na gari aina ya Toyota Haice Pickup double cabin yenye thamani ya shilingi milioni 68/-.

Askofu Mdegella alizaliwa mwaka 1951 katika Kijiji cha Ipalamwa, Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa. 

Askofu huyo amekuwa askofu mkuu wa dayosisi ya Iringa ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania kwa miaka 38 kama mchungaji, na miaka 30 kama askofu .

Askofu huyo ameagwa leo (jumatatu) katika ibada maalum ya kustaafu kwa heshima iliyofanyika katika usharika wa Kanisa Kuu (Cathedral) Iringa mjini, ibada ambayo ilihudhuriwa na Mkuu wa Kanisa la KKKT, Askofu Dkt. Fredrick Shoo.

Akisoma hati ya kustaafu kwa heshima askofu dkt owdenburg mdegella kwa niaba ya kanisa la KKKT, Katibu Mkuu wa KKKT- Dayosisi ya Iringa, Nayman Chavalla alisema kuwa Askofu Mdegella alichaguliwa na Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Dayosisi ya Iringa tarehe 8 Oktoba mwaka 1986 kuwa askofu kwa mujibu wa katiba ya dayosisi ya Iringa ya kanisa la KKKT.

Chavalla alisema kuwa kwa niaba ya washarika wote 142,000 wa dayosisi hiyo, askofu huyo amestaafu rasmi na kwa heshima.

Alisema kuwa Askofu Mdegella aliwekwa wakfu kuwa askofu na kuingizwa kazini kuwa mkuu wa dayosisi katika ibada iliyofanyika uwanja wa samora, mjini iringa tarehe 27 januari, 1987.

Kwa upande wake, Askofu mstaafu Dkt. Mdegella kwa niaba ya Dayosisi ya Iringa amewapongeza washarika kwa zawadi na kumshukuru Mungu kwa utumishi wake.

Alisema kuwa kama mchungaji mara nyingi alikumbana na uasi, kupingwa, na kutishiwa maisha yake alipokuwa akitetea kweli ya injili, lakini kwa nguvu za Mwenyezi Mungu alishinda changamoto hizo.


Ibada maalum ya kustaafu kwa heshima Baba Askofu Dkt. Owdenburg Mdegella ilihudhuria na wageni mbalimbali kutoka Ujerumani, Sweden na Marekani pamoja na viongozi wa serikali ya mkoa wa Iringa na viongozi wa siasa na washarika wa Dayosisi ya Iringa.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...