Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam wa Kanisa la Anglikana, Dk valentino Mokiwa jana alishindwa kuendesha vikao viwili baada ya kundi la waumini kufika Usharika wa Ilala kwa lengo la kuzuia.
Askofu Mokiwa, ambaye anapinga uamuzi wa Askofu Mkuu wa Anglikana, Dk Jacob Chimeledya kumvua madaraka kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha, alikuwa aendeshe vikao vya kamati ya fedha na halmashauri kuu, lakini alilazimika kuviahirisha baada ya kundi hilo kufika eneo hilo.
Wakati waumini hao wakizuia vikao hivyo kufanyika, mashemasi, mapadri, wainjilisti na waumini wa dayosisi hiyo wametoa tamko la kumuunga mkono Dk Mokiwa wakipinga uamuzi wa mkuu wa kanisa hilo kumvua madaraka.
Askofu Mokiwa anapinga uamuzi wa kumvua madaraka akisema hauwezi kufanywa na mkuu wa kanisa, bali na halmashauri kuu ya jimbo ambayo anasema haikushirikishwa zaidi ya kutaarifiwa uamuzi huo.
Tukio la jana la kumzuia Dk Mokiwa kufanya mkutano lilitokea saa mbili asubuhi katika Kanisa la Mtakatifu Nicolau wilayani Ilala, ambako kuna ofisi ya Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam.
Mmoja wa watu walioshiriki kuzuia vikao hivyo, Haule Sylvester ambaye alijitambulisha kuwa kiongozi wa waumini wa Anglikana jijini Dar es Salaam, alisema walichukua uamuzi huo kwa kuwa Dk Mokiwa ameshavuliwa uaskofu.
“Huyu (Dk Mokiwa) hapaswi kufanya shughuli zozote za kanisa kwa sababu si askofu. Lakini amekuwa akiendesha vikao vya siri na mapadri wanaomuunga mkono,” alisema Sylvester.
“Jana (juzi) alifanya kikao cha siri. Leo (jana) alikuwa aongoze vikao viwili, kikiwamo cha bodi ya fedha ya dayosisi hii, ndiyo maana tumemzuia.”
Alifafanua kuwa baada ya kikao hicho cha fedha kilichokuwa kimepangwa kuanza saa 3:00 asubuhi, kikao ambacho kingefuata ni cha halmashauri kuu ya dayosisi ambacho kingefanya uamuzi wa mambo ambayo yangejadiliwa na bodi ya fedha.
Sylvester alisema kwa mujibu wa katiba ya dayosisi hiyo, vikao hivyo vyote vinatakiwa viongozwe na mwenyekiti ambaye ni askofu wa dayosisi.
No comments:
Post a Comment